Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sitaki tena Urais – Sehemu ya 12

RAIS 12 Pict

UTANGULIZI

Wakati akiliwaza tukio la kula nyama ya binaadamu, simu yake ya mezani iliyokuwa pembeni mwa sofa iliita. Shanga alinyoosha mkono na kuunyakua mkono wa simu.

“Rais Shanga hapa”  Shanga alijitambulisha alipouweka mkono wa simu sikioni.

“Mheshimiwa tumepokea taarifa ya kusikitisha sasa hivi kutoka Canada. Jimmy alipata ajali ya gari jioni ya leo na amefariki dunia….”

SASA ENDELEA


“Jimmy mtoto wangu?” Shanga aligutuka.

“Ndiyo mheshimiwa. Ni habari ya kusikitisha sana”

“Sasa mawazo ya Shanga yalikwenda katika ile nyama waliyokula na wenzake.

“Hebu nieleze sawa sawa. Ilikuwaje?”

“Taarifa ya awali iliyokuja imesema Jimmy Shanga amepata ajali na amefariki wakati anakimbizwa hospitali. Lakini jambo la ajabu lililotokea ni kwamba maiti yake imetoweka baada ya kuwekwa mochwari”

“Unasemaje? Maiti yake imetoweka?”

“Balozi wetu aliyeko Canada alipotakakuhakikisha tukio hilo mwili wa marehemu haukuonekana ulipowekwa na haijajulikana imetoweka vipi!”

“Mtoto wangu ndiye yule tuliyemla!” Shanga alijisahau na kusema kwenye simu.

“Unasemaje mheshimiwa?”

Shanga akagutuka baada ya kuulizwa swali hilo. Alihisi msemaje wa upande wa pili alikuwa amemsikia.

“Hakuna kitu. Ninasikitika tu. Ninahitaji nipate taarifa kamili. Ni nani anayeshugjulikia suala hilo?”

“Ni balozi wetu aliyeko Canada. Anaendelea kufuatilia na ameahidi kutulete taarifa kamili haraka iwezekanavyo”

“Sawa”

Shanga alipoirudisha simu alijikuta akiwa ameduwaa, akiwa hajui afanye nini. Aliyataka mwenyewe! Alishajua kuwa mwanawe ndiye aliyeliwa nay eye alishiriki kumla. Alijua pia kuwa maiti yake isingeweza kupatikana kwani kifo chake kilikuwa ni cha miujiza. Na mwili wake ndio ule aliooneshwa ukiwa mifupa mitupu.

Aliahidi mwenyewe kumtoa mwanawe kwa kutaka urais. Awali alidhani kuwa alikuwa mjanja kutoa ahadi ambayo asingeitekeleza. Kumbe wenzake walikuwa wajanja zaidi.

Sasa aliyakumbuka maneno ya Osaka alipomwambia “Miaka mitano mengine tutadai tena” Na alikitambua alichokusudia Osaka. Alikusudia kwamba watataka mtoto wake mwingine baada ya kipindi chake cha urais cha miaka mitano kumalizika na kuanza kipindi kingine.

Shanga alitikisa kichwa kusikitika alipojiambia “Urais wangu wa bure umenigharimu roho ya mwanangu!”

Hakuwa akijua kwamba alipaswa alie kwa kumpoteza mwanawe, au afurahi kwa kupata urais aliokuwa anautaka au afanye nini? Shanga hakuwa na jibu.

Akajiuliza amlaumu nani?. Ampigie simu Osaka na kumlaumu wakati kila kitu kinachotokea walikubaliana wote.

“Siwezi kumlaumu Osaka” akajiambia. “Zaidi nitajilaumu mwenyewe. Kitendo cha kukubali kujiunga na watu wale kilikuwa cha kipumbavu. Pengine ningeweza kupata urais bila ya wao”

Aliendelea kujiambia tukio limeshatokea, sasa kinachotakiwa ni kuganga yaliyopo na yajayo.

Kwa upande mwingine Shanga alijiuliza atamueleza nini mke wake kuhusu tukio la mwanawe. Amueleze ukweli wa makosa yake au aendelee kumficha” alijiuliza.

Kumueleza ukweli haitawezekana, akajiambia. Bora nimfiche tu ajue mwanawe alikufa kwa ajali na si vinginevyo.

Kilichoko nyuma ya pazia kitabaki kuwa ni siri yangu, aliendelea kuwaza.

Wakati akiwaza alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa. Tukio la kifo cha mwanawe na tukio la kula nyama yake vilimchanganya. Aliona alikuwa amebeba jukumu kubwa mbele ya Mungu. Akajikuta akiwalaani kina Osaka.

Alipozinduka hapo aliona aanze kutoa taarifa kwa watu mbalimbali akiwemo mke wake. Alimpigia simu mke wake aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi katika mkoa mwingine na kumuita. Bila kumueleza nini kimetokea alimtaka arejee haraka Maloto.

Aliwasiliana na maafisa wake wa ikulu na kuwaagiza wahakikishe kuwa helikopta ya jeshi la polisi inakwenda kumchukua mke wake na kumpeleka Maloto usiku ule.

Yapata saa saba usiku mke wake aliwasili Maloto. Ndipo Shanga alipomueleza kilichotokea.

“Nilichokuitia ni kwamba kuna tukio la msiba limetoke jioni ya leo huko Canada”

“Msiba wa nani?” Joyce alimuuliza kwa sauti iliyoonesha kufadaika.

“Msiba wetu. Tumetokewa na kipindi cha huzuni kubwa. Inabidi tukabiliane na suala hili kwani bwana ametoa na ndiye aliyetwaa. Sisi tushukuru tu”

“Naomba unifafanulie ni nani amekufa?”

“Ni mtoto wetu Jimmy. Alipata ajali ya gari jioni ya leo huko Canada”

“Jimmy ndiye aliyefariki?”

“Ndiyo mke wangu”

Joyce akaangua kilio.

“Unatakiwa ujikaze mke wangu. Usianze kulia”

Joyce aliendelea kulia

“Umewasiliana na mdogo wake Otis?” Joyce akamuuliza Shanga kwa kigugumizi.

“Sijawasiliana naye. Muda wote nilikuwa nawasiliana na maafisa wangu ili kupata taarifa kamili”

“Sasa nani amethibitisha kifo chake?”

“Balozi wetu aliyeko Canada”

“Ulizungumza naye wewe mwenyewe?”

“Amezungumza na maafisa wa ikulu”

“Ilitakiwa umpigie ili kuthibitisha”

“Maafisa wa ikulu hawawezi kusema uongo”

“Ngoja nimpigie Otis….”

Joyce alikwenda kwenye simu akampigia Otis moja kwa moja.

Shanga alitambua kosa lake jingine la kutompigia balozi au mwanawe Otis na kupata ukweli. Ilitokana na kule kuchanganyikiwa.

“Otis hebu nieleze nini kimetokea huko?” Joyce alimuuliza mwanawe mara tu alipopokea simu.

“Jimmy amefariki dunia. Alipata ajali ya gari jana jioni akakimbizwa hspitali. Wakati mimi na balozi tunafika hospitali tulikuta ameshafariki na amepelekwa mochwari. Lakini jambo la ajabu ni kuwa mwili wake umetoweka ukiwa mochwari”

“Umetoweka vipi?”

‘Haijulikani mama. Ulipelekwa kuhifadhiwa, tulipokwenda sisi mwili hauonekani!”

“Sasa mmethibitishaje kuwa ni yeye wakati mwili wake hamkuuona”

“Ni yeye. Alipigwa picha wakati anapata ajali. Pia kitambulisho chake na vitu alivyokuwa navyo mfukoni nimekabidhiwa”

“Sasa huo mwili wake umekwenda wapi?” Joyce alimuuliza mwanawe Otis.

“Haijulikani. Ni tukio ambalo limemshangaza kilamtu.Tulihangaika sana na balozi Tulidhani labda mwili huo alipewa mtu mwingine kwa makosa lakini imebainika kwamba hakukuwa na mwili wowote uliotolewa jioni ile”

Wakati Joyce akizungumza na mwanawe, Shanga alikuwa akisikiliza. Alishajua kuwa mwili wa mwanawe ndio ule aliooneshwa na Osaka. Na huko hospitali usingepatikana tena.

“Sasa ngoja tumpigie balozi, atueleze amechukua hatua gani?” Joyce akamwambia Otis kwenye simu.

“Sawa mama mpigie umsikilize”

Joyce aliurudisha mkono wa simu chini na kumtazama Shanga.

“Mpigie balozi atueleze hatua alizochukua”.

“Ndipo Shanga aliposogea kwenye simu na kumpigia balozi huku akijiona kama mpumbavu mbele ya mke wake.

“Mimi ni Rais Shanga wa Kamisa. Tumepokea taarifa yako iliyotueleza kuhusu kifo cha Jimmy. Hebu tueleze imekuwaje?”

“Ilikuwa kama saa moja usiku hivi wakati Otis na polisi wawili pamoja na afisa mmoja wa chuo anachosoma Otis na marehemu walipokuja nyumbani kwangu na kuniarifu kuhusu tukio la ajali ya gari lililomtokea marehemu Jimmy” Balozi alimueleza  Rais Shanga.

“Ndiyo”

“Ilibidi tuondoke pamoja kwenda katika hospitali alikopelekwa. Tulipofika tuliuta Jimmy ameshafariki. Tukakabidhiwa vitu vyake na kupelekwa Mochwari kwenda kuoneshwa mwili wake. Lakini jambo la ajabu lililotokea ni kwamba mwili wake haukuonekana hadi sasa!”

“Haukuonekana!. Umekwenda wapi?”

“Haijajulikana. Hivi sasa uchunguzi unafanywa na polisi na wameahidi kunipa taarifa kesho”

“Haiwezekani kuwa mwili huo ulitolewa kimakosa kwa mtu mwingine?”

“Sina hakika lakini itajulikana baada ya uchunguzi huo wa polisi”

“Na taarifa hiyo ya ajali iliyomtokea marehemu inaoneshaje, marehemu alikuwa ndani ya gari au alikuwa…?”

“Alikuwa akitembea kwa miguu. Gari lililomgonga limekimbia na halijapatikana”

“Marehemu ameumizwa sehemu gani?”

“Tulivyoelezwa na madaktari ni kwamba ameumizwa sehemu za kifua na kichwa lakini lakini hakutoka damu hata kidogo. Mwili wake ulionekana uko sawa kabisa”

“Hapo kesho utakapopatiwa taarifa ya uchunguzi wa polisi utuwasilishie haraka”

“Sawa mheshimiwa”

Shanga akakata simu.

“Itakuwaje mwanangu afe halafu mwili wake usionekane?” Joyce akamuuliza Shanga. Sasa alikuwa ameacha kulia.

Jibu alikuwa analo Shanga lakini ilikuwa ni vigumu kulitoa.

“Balozi amenieleza kuwa polisi wanafanya uchunguzi na kesho watampa taarifa”

***************

Asubuhi kulipokucha Shanga alizuia taarifa ya kifo cha mwanawe isitolewe kwenye vymbo vya habari mpaka kwanza wapokee taarifa ya uchunguzi wa polisi wa Canada kuhusiana na kupote kwa mwili wa mwanawe hoyo.

Lakini vyombo vya habari vya nje vilianza  kuliripoti tukio hilo wakati ikulu ya Kamisa ikiwa kimya.

Mpaka inafika saa saba mchana Rais Shanga alipokea taarifa ya maandishi ya uchunguzi wa awali wa polisi wa Canada juu ya kupotea kwa mwili wa marehemu Jimmy ukiwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya serikali nchini humo.