Sitaki tena Urais – Sehemu ya 11
UTANGULIZI
Ofisa usalama alitoka akimuacha Osaka akiketi kwenye sofa.
“Tumepotezana muda mrefu kidogo lakini tunajua ni kwa sababu ya majukumu” Osaka akamwambia rais uso wake ukiwa umepambwa kwa tabasamu.
“Ni kweli. Kama unavyojua ndiyo kwanza nimeanza kushika madaraka. Nilikuwa na kazi kubwa ya kuunda serikali yangu.”
SASA ENDELEA
“TUNAJUA. Hilo si tatizo. Leo ni jumamosi, tungependa angalau kwa leo ujumuike na sisi kwenye mafundisho yetu.
“Ndiyo umenifuata?” Shanga alijikuta akiuliza.
“Ndiyo mheshimiwa”
“Tunaweza kutoka. Nitatumia gari langu binafsi”
Dakika chache baadaye rais Shanga alikuwa kwenye gari lake akilifuata gari la Osaka.
Wakati anataka kutoka nyumbani kwake aliwambia maafisa usalama na walinzi wake kuwa anazunguka jiji kidogo kwa kutumia gari lake binafsi na hakuhitaji ulinzi.
Maneno yake yaliwashangaza walinzi wake. Kwa vile mwenyewe alilazimisha kuwa anataka atoke peke yake, walimuachia.
Shanga aliwaacha maafisa usalama wakiwa na wasiwasi. Wao ndio waliokuwa na jukumu la usalama wa rais. Lolote litakalomtokea rais, wao ndio watakuwa watu wa kwanza kuulizwa na kujieleza.
Si tu watanekana wazembe kwa kumuacha rais kutoka peke yake usiku ule, bali kama gari lake litapata ajali watakuwa na kosa la kujibu.
Hata kama isingetokea ajali, kama wataulizwa rais yuko wapi na wao kutojua mahali rais wao alipo, litakuwa na kosa vilevile.
Hata hivyo, walijiuliza, watafanyaje wakati rais mwenyewe alitaka atoke peke yake. Nani angeweza kumzuia au kumwambia anachofanya ni kosa.
Wakati maafisa hao wakiwa na wasiwasi, Shanga mwenyewe alikuwa akilifuata benz jeusi lililokuwa linaendeshwa na Osaka. Alikuwa kama mbwa aliyekuwa akijipeleka mwenyewe kumezwa na chatu.
Hakufikiria tena madaraka yake ya urais na wala hakufikiria tena kuwa alishaamua kujitoa katika kundi hilo. Alichokuwa akikifikiria ni kutekeleza kila alichoamriwa.
Wazo kuwa aliwadanganya kuwa atamtoa mwanawe halikuwemo ndani ya akili yake. Kwa hiyo hata hakufikiria atakwenda kuwajibu nini endapo ataulizwa kuhusu ahadi yake ya kumtoa mtoto wake.
Dakika chache baadaye gari la Osaka liliingia katika geti la jumba lao lililokuwa katika eneo la Osariver huku gari la Shanga likifuata nyuma.
Wakati wote Shanga hakuwa ametilia maanani juu ya kosa alilofanya kutoka ghafla katika nyumba yake na kukataa ulinzi wakati akiwa ni rais wa jamhuri aliyepaswa kulindwa masaa ishirini na nne.
Mara tu walipoyaegesha magari kwenye banda la magari lililokuwa na magari kadhaa ya kifahari, Osaka na Shanga walishuka na kuelekea kwenye lango la jumba hilo.
Wakati shanga akitembea na Osaka kuelekea kwenye lango hilo alionekana kama mtu wa kawaida na mwenyewe pia alijiona kama mtu wa kawaida ila alikuwa na wasiwasi.
Waliingia katika jumba hilo, wakaelekea kwenye ngazi ya kushukia chini. Walishuka chini na kutokea kwenye ukumbi uliokuwa umefurika wanachama wa kundi hilo.
Osaka na Shanga walikwenda kuketi katika viti vilivyokuwa msitari wa mbele.
Baada ya kumalizika kile walichokiita mafundisho Shanga alipatwa na wasiwasi kwamba angeulizwa kuhusu ahadi yake ya kumtoa mwanawe. Alishapanga kueleza kuwa mwanawe asingepatikana kwa sababu yuko masomoni nje ya nchi.
Lakini hakukuwa na yeyote aliyemuuliza chochote, badala yake alisikia tangazo likitolewa kwamba kungekuwa na karamu kabla ya watu kuondoka.
Baada ya muda kidogo zilipitishwa sahani kwa kila mwanachama. Kila mwanachama alipewa sahani yake. Kwenye kila sahani kuliwekwa vipande saba vya nyama ambayo Shanga hakuweza kutambua kama ilikuwa mishikaki au nyama iliyokaushwa au iliyokaangwa. Mbali na vipande hivyo vya nyama kulikuwa na uma wa kulia na bilauli ya kinywaji.
Shanga alipoona watu wanakula na yeye alikita kipande cha nyama na kuanza kula. Alisukumia na kinywaji kilichokuwa baridi.
Wakati anamalizia chinyango ya saba ndipo Shanga alipoanza kukumbuka kwamba alihitaji kurudi haraka nyumbani kwake kwani aliondoka kinyume na taratibu.
Alimshukuru Osaka na kumwambia alihitaji kuondoka.
“Asante mheshimiwa. Tunakushukuru sana kwa kuhudhuria mafundisho yetu ya leo. Ni heshima kubwa sana kwetu” Osaka alimwambia Shanga na kunyanyuka kwenye kiti. Shanga naye alinyanyuka.
“Twenzetu” Osaka akamwambia Shanga.
Wakati wanaelekea kwenye ngazi walitokea watu wawili waliokuwa wamebeba kitu kilichokuwa katika kichanja cha chuma. Kitu hicho kirefu kilikuwa kimelazwa kwenye kichanja hicho na kufinikwa shuka nyeupe.
Watu hao walikwenda hadi mbele ya Shanga na Osaka wakasimama. Shanga na Osaka nao wakasimama.
Osaka akamtazama Shanga.
“Unajua karamu yetu ya leo ilikuwa ni ya nani?”
Shanga hakuelewa swali akatikisa kichwa.
“Sijui”
Osaka alifunua ile shuka iliyofinikiwa kile kitu. Iliyokuwa imefinikwa ilikuwa mifupa ya binaadamu ikiwa na kichwa chake. Ilikuwa mifupa ya miguu, mikono na ya kifua iliyokuwa imeungana na kichwa.
“Hii ndiyo karamu tuliyokula leo” Osaka akmwambia Shanga.
Shanga alikunja uso wakati akiitazama ile mifupa. Kilichomtaharukisha zaidi ni kile kichwa ambacho hakikuwa kimechunwa. Kilikuwa na sura yake pamoja na nywele.
Alipokiangalia vizuri kichwa hicho Shanga aliitambua sura ya mwanawe Jimmy aliyekuwa anasoma nchini Canada.
Shanga alishangaa. Imekuwaje?
Leo nimekula nyama ya mtu na mtu mwenyewe ni mwanangu! Akajiuliza.
Hata hivyo alijipa moyo kuwa mwanawe Jimmy alikuwa akisoma Canada. Isingewezekana kuwa ndiye yule.
Ile hisia kuwa alikula nyama ya binaadamu ilimfanya apate kigegezi. Akajisikia kuteuka.
“Umeona?” Osaka akamuuliza.
“Nimeona” Shanga alimjibu kwa sauti nzito.
“Miaka mitano mengine tutadai tena”
Shanga hakuelewa alichoelezwa kuwa miaka mitano mengine watadai tena. Licha ya kutoelewa hakuona umuhimu wa kuliza. Umuhimu aliouona ulikuwa ni wa kuondoka mahali hapo haraka iwezekanavyo kabla ya maafisa usalama kumfuatilia.
Baada ya kumaliza kula kile kilichotajwa kuwa ni karamu, Shanaga alikuwa kama aliyezinduka na kufahamu kuwa akiwa kama rais wa nchi alifanya kosa kubwa kufika mahali hapo yeye mwenyewe.
Osaka alipomwambia Shanga “miaka mitano mengine tutadai tena” bila kumfafanulia sentensi yake aliifinika ile mifupa kwa ile shuka iliyokuwa imefinikiwa. Wale watu wakaondoka nayo. ‘Sasa twende zetu” Osaka akamwambia Shanga.
Walikwenda kwenye ngazi wakapanda na kutoka nje ya jumba hilo. Shanga alikwenda mwenyewe kunako gari lake akajipakia na kuondoka. Hakuonekana kuwa rais wala hakupata heshima yoyote ya urais.
Wakati anarudi na gari alikuwa anajilaumu kutokana na kosa alilofanya. Alijiuliza ni kitu gani kilimfanya akubali kuchukuliwa na Osaka usiku ule wakati alishaamua kujitoa katika kundi lao.
Nilichofanya ni uzembe kwa kuzingatia kuwa mimi ni rais wa nchi, alijiambia.
Lakini wazo lililomtia wasiwasi mkubwa ni ile mifupa ya binaadamu iliyokuwa na kichwa chenye sura kama ya mwanawe. Akajiuliza mtu yule ni nani, alitoka wapi na kwanini alifanana na mwanawe Jimmy.
Katika maisha yake hakutarajia kuwa kuna siku angekula nyama ya binaadamu mwenzake. Tukio hilo limemtokea kama mkasa ambao hatausahau maishani mwake.
Tena mkasa uliomdhalilisha akiwa rais!
Wakati anaendesha alishitushwa na mlio wa simu yake ya mkononi. Akaitoa kwenye mfuko wa koti lake na kuitazama. Ilitoka kwa mkurugenzi wa usalama. Badala ya yeye kuhofisha walio chini yake kama rais, Shanga alijikuta akipata yeye hofu baada ya kuliona jina la mkurugenzi huyo kwenye simu.
Shanga alitambua kuwa afisa usalama anayeratibu ulinzi wa nyumbani kwake alimpigia simu mkurugenzi wa usalama na kumjulisha juu ya kuondoka kwake na kwenda mahali kusikojulikana bila ya ulinzi wowote.
“Mheshimiwa tunahitaji kujua uko wapi na nini kinaendelea hapo?” Sauti ya mkurugenzi wa usalama ilisikika kwenye simu wakati Shanga alipopokea simu yake.
“Nilikuwa nazunguka kidogo kuliangalia jiji, sasa ninarudi” Shanga alijibu huku akiona wazi kuwa alitoa jibu la kipumbavu.
“Sawa mheshimiwa. Pia tunapenda kujua kama upo salama kwa sababu niliambiwa hukuondoka na walinzi wako”
“Nipo salama, msiwe na wasiwasi. Sikuhitaji ulinzi kwa sababu nilizungukazunguka tu katika maeneo ya karibu kuangalia jiji. Pia ninatumia gari binafsi si la serikali”
“Sawa mheshimiwa”
Shanga akairudisha simu kwenye mfuko.
Dakika chache baadaye aliliingiza gari kwenye geti la nyumba yake. Geti hilo lilikuwa likilindwa na askari wasiopungua wanne huku gar la askari hao likiwa kando ya geti hilo.
Alipoliegesha gari kwenye banda la magari, askari mmoja alimfungulia mlango. Shanga akashuka. Alikwenda moja kwa moja kwenye mlango wa nyumba hiyo akaufungua na kuingia ndani. Alikwenda kuketi sebuleni na kujiwazia.
Wakati akiliwaza tukio la kula nyama ya binaadamu, simu yake ya mezani iliyokuwa pembeni mwa sofa iliita. Shanga alinyoosha mkono na kuunyakua mkono wa simu.
“Rais Shanga hapa,” Shanga alijitambulisha alipouweka mkono wa simu sikioni.
“Mheshimiwa tumepokea taarifa ya kusikitisha sasa hivi kutoka Canada. Jimmy alipata ajali ya gari jioni ya leo na amefariki dunia….”