Sitaki tena Urais – Sehemu ya 07
UTANGULIZI
Baada ya kivuli hicho kutoweka watu waliondoka kwenye viti na kwenda kumpa Shanga mkono wa pongezi. Wengine walidiriki kumuita mheshimiwa rais. Wakati wote alipokuwa akipeana mkono na watu hao Shanga alikuwa akitabasamu.
Baada ya watu hao kupeana mkono na Shanga waliagana naye na kuondoka mmoja mmoja..
SASA ENDELEA
SHANGA aliondoka mwisho akiwa amefuatana na Osaka. Walitoka nje ya jumba hilo wakasimama kwa muda kando ya mlango wakizungumza na huku magari yakiendelea kuondka.
Watu walipokuwa wamepungua ndipo Shanga alipokwenda kulitoa gari lake na kuondoka.
Ingawa alikuwa na furaha na matumaini ya kupata urais, ahadi yake ya kumtoa mwanawe iliendelea kumtia hofu. Alihisi kama vile alikuwa amemuweka mwanawe rahani ili apate urais japo alijua kwa vyovyote vile asingeweza kumtoa.
Alijua fika ahadi aliyotoa ilikuwa ya uongo na isiyo ya maana. Hata hivyo alijiulza atakwenda kumueleza nini mke wake kuhusiana na pete iliyokuwa kidoleni mwake?
Atamueleza uongo gani mpaka aamini kuwa ilikuwa pete ya kawaida. Wakati wote akiendesha alikuwa akiitazama tazama. Ilikuwa pete kubwa ya bapa iliyokuwa na michoro ya ajabu, ambayo Shanga hakuwahi kuona mfano wake mahali popote.
Aliposimamisha gari mbele ya geti la nyumba yake Shanga aliitoa ile pete kidoleni na kuitia mfukoni.
Ni vyema nitafute uongo kwanza wa kumueleza mke wangu ndiyo niivae, Shanga alijiambia kimomoyo wakati akiliingiza gari ndani ya geti.
Wakati Shanga akiendelea na mafunzo yake ya kila jioni ambayo aliambiwa yangemchukua wiki moja, kampeni za uchagizi zikaanza.
Picha za mgombea urais kupitia chama cha UM pamoja na fulana za kampeni vilikuwa vimetawanywa katika mikoa yote kumi na mitano ya nchi ya Kamisa.
Katika mji mkuu wa Maloto picha hizo zilipachikwa katika kila kona ya jiji hususa kwenye magari ya mgombea urais, mgombea ubunge na mgombea udiwani.
Katika majumba ya starehe, zikiwemo nyumba za miziki na sinema. Kwenye masoko, mahoteli na nyumba za wageni, kulikuwa kumepachikwa picha za wagombea wa vyama mbalimbali wakiwemo wagombea wa chama tawala.
Juu na chini ya picha ya mgombea urais wa chama cha UM Max Shanga, kulikuwa na maandishi yaliyosomeka.
MCHAGUE SHANGA KUWA RAIS WAKO, CHAGUA UM.
Maandishi mengine yalisomeka.
SHANGA NI PEKEE, MCHAGUE AWE RAIS WAKO.
Maandishi mengine yalisomeka.
MCHAGUE SHANGA KWA MAENDELEO.
Akiwa ameajiri dereva maalum, gari la Shanga lilikuwa likizunguka mji mzima likiwa na kipaza sauti kilichokuwa kikimnadi Max Shanga. Kipaza sauti hicho kilikuwa kikiwataka wananchi kumchagua Max Shanga wa chama cha upinzani cha UM kuwa rais wa Kamisa.
Mkutano wa kwanza wa kampeni wa chama hicho uliotambulika kama uzinduzi wa kampeni ulifanyika saa kumi jioni katika kiwanja cha mpira kilichokuwa kando kidogo ya jiji hilo.
Uzinduzi huo ambao ulikuwa ni wa kitaifa kwa chama hicho ulifuatana na muziki wa ngoma za kiasili. Wakereketwa wa chama hicho walikuwa wamevalia fulana za chama hicho wake kwa waume isipokuwa mgombea urais mwenyewe aliyekuwa amevaa suti nyeusi kama alivyoagizwa.
Pete aliyovalishwa na Osaka alikuwa akiivaa anapotoka nyumbani kwake na anaporudi huivua ili mke wake asiione.
Katika mkutano wake wa kwanza mahudhurio ya wananchi yalikuwa makubwa japokuwa kulikuwa na mkutano mwingine wa chama tawala katika kiwanja kingine.
Sanga akiwa amepata moyo alizungumzia mengi kuhusu mustakabali wa nchi ya Kamisa. Kwanza alieleza ni kwanini anagombea urais. Akaeleza sababu tatu. Ya kwanza uwezo wa kuongoza alikuwa nao.
Ya pili ni dhamiri yake ya kuleta maendeleo. Na ya tatu mabadiliko ya kisiasa yalikuwa yanahitajika nchini humo.
Akaeleza kwamba chama chake kilikuwa na sera thabiti za kuleta maendeleo nchini humo.
Aliwambia wananchi katika kiwanja hicho endapo watamchagua kuwa rais atahakikisha kuwa nguvu ya serikali inaelekezwa katika elimu na afya na atafanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa serikali.
Shanga hakuacha kuikosoa serikali iliyokuwa madarakani kwamba imeongeza umasikini kutokana na kutokuwa na sera za kumkwamua mwananchi.
Wakati wote Shanga alipokuwa anazungumza alikuwa akishangiliwa kwa nguvu na wananchi.
Baada ya kumaliza hutuba yake alianza kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo na kuwataka wananchi wamchague kuwa mbunge wao.
Mkutano huo ulimalizika saa kumi na mbili jioni ambapo Shanga alijipakia kwenye gari yake na kurudi nyumbani.
Kabla ya kufunguliwa geti alikumbuka kuivua pete yake na kuitia mfukoni. Mara tu alipoingia ndani mke wake alimuuliza.
“Mkutano umekwendaje?
“Mkutano ulikuwa mzuri, ulikuwa mzuri sana.
“Watu wmehudhuria wengi?
“Watu walikuwa wengi kuliko nilivyotarajia
“Wacha….
“Kweli kabisa. Tena kulikuwa na mkutano mwingine wa chama tawala lakini watu walimiminika kwa wingi kwenye mkutano wetu.
“Ni ishara ya kukubalika kwa wananchi.”
Walikuwa wamesimama sebuleni, Shanga akaketi kwenye sofa.
“Wananchi wametukubali. Kwa jumla tumeanza vizuri,” Shanga alisema.
Joyce naye aliketi kando yake.
“Na kwa upande wa sera zenu, mmejinadi vizuri?
“Tumejinadi vizuri sana. Binafsi nimezungumza viuri. Uwezo wa kuzungumza ninao.
“Mmevikumbuka vyombo vya habari?
“Kivipi?
“Waandishi wa habari ni muhimu, ilitakiwa muwaalike kutoka vyombo mbalimbali ili waandike habari zenu.
“Ni kweli, umenikumbusha kitu muhimu lakini ninaamini waandishi walikuwepo. Umati ulikuwa ni mkubwa. Ila kuanzia sasa tutakuwa tunawaalika”
“Muwaalike pia waandishi wa televisheni.
“Nadhani waandishi wa televisheni walikuwepo. Niliona kamera nyingi.
“Kama walikuwepo tutaona kwenye taarifa ya habari ya saa moja.
Baada ya maongezi hayo Shanga alinyanyuka na kuingia chumbani. Alioga, alibadili nguo na kutoka tena.
“Njoo haraka!” alisikia sauti ya mke wake ikimuita sebuleni.
Shanga aliharakisha kwenda sebuleni akamkuta Joyce akitazama TV.
Shanga naye akapeleka macho yake kuangalia alichokuwa anakitazama mke wake. Akaona taarifa ya mkutano wa chama chake ikitangazwa.
Mtangazaji alisifia umati wa watu ulivyofuria katika mkutano huo. Shanga alioneshwa akiwa kwenye jukwaa akinadi sera za chama hicho.
“Kumbe mume wangu ulipendeza!”
“Nilipendeza?”
“Ulipendeza sana. Ninajuta ni kwanini sikufuatana na wewe. Halafu watu walikuwa wengi kweli kweli!”
“Umeona mwenyewe”
“Nimeona. Kwa kweli inatia moyo”
“Unaonaje mkutano wa kesho tukitoka pamoja?”
“Tutoke. Nitakuwa ninapata uzoevu”
Simu ya mkononi ya Shanga ikaita. Hakukuwa na namba yoyote iliyotokeza kwenye simu. Shanga akaipokea.
“Osaka hapa. Nipo nje ya nyumba yako. Tafadhali tunakuhitaji kidogo” Sauti ikasikika kwenye simu.
Shanga alishituka kidogo aliposikia jina hilo na aliposikia watu hao wako nje ya nyumba yake.
“Sawa, ninakuja” Shanga akasema kabla ya kumwambia mke wake kuwa ana wageni wako nje wanahitaji kuonana naye.
Shanga kabla ya kutoka nje ya geti alitoa ile pete aliyokuwa ameiweka mfukoni mwake na kuivaa. Kulikuwa na benz nyeusi iliyosimama mbele ya geti. Shanga alipolisogelea gari hilo mlango wake wa nyuma ulifunguliwa. Akasikia sauti aliyokuwa akiifahamu ikimwambia.
“Karibu ndani”
Shanga akaingia ndani ya gari hilo. Osaka alikuwa amekaa peke yake katika siti ya nyuma. Katika siti ya dereva aliketi mtu ambaye Shanga hakumfahamu.
Osaka alimsamia Shanga kwa kumuonesha alama zao za vidole kabla ya kumwambia.
“Habari yako bwana Shanga?”
Shanga alijibu kwa kuonesha alama za vidole kama alivyofunzwa na Charly na kisha alisema.
“Nzuri bwana Osaka. Natumaini hamjambo nyote?”
“Hatujambo. Kwanza ninakupongeza kwa mkutano wako wa leo”
“Asante sana”
“Nakupongeza kwa sababu ni mkutano wako wa kwanza lakini ulifana sana kwa kuwa na idadi kubwa ya watu. Na pia uliweza kujinadi vizuri. Una kila ishara ya kukubalika kwa wananchi wa Kamisa”
Huku akitabasamu Shanga alisema.
“Asante sana. Kumbe ulikuwepo?
“Tulikuwepo. Wananchi wamekuelewa vizuri”
“Nashukuru kwa kunipa moyo.
“Jingine ni kwamba tunakukumbusha kwamba kesho ni jumnne, Unatakiwa kuanza kampeni saa nane mchana. Na vilevie tutakuwa na mafundisho ya usiku. Unatakiwa uhudhurie bila kukosa.”
Shanga alisita kidogo akawaza kabla ya kumjibu.
“Kuanza kampeni saa nane, tutatakiwa tuanze matayarisho tangu asubuhi.
“Ndiyo, itabidi muanze matayarisho asubuhi na hili jambo tulikubaliana kabla. Au umesahau?”
“Ninakumbuka. Ratiba yetu ilikuwa ni kuanza mkutano wetu saa kumi jionu lakini haidhuru tutabadili ratiba kesho asubuhi”
“Sawa”
“Na kuhusu mafunzo ya jioni kwa kesho sitaweza kufika kutokana na huo mkutano. Sitakuwa na muda saa kumi, isipokuwa nitahudhuria mafundisho ya usiku.”