Sitaki tena Urais – Sehemu ya 06
UTANGULIZI
Baada ya utambulisho huo Shanga na Charly kila mmoja alisema amefurahi kumtambua mwenzake, wakapeana mikono na kuulizana hali.
SASA ENDELEA
“SASA mimi ninawaacha. Shanga utakuwa unapata mafunzo ya kila jioni katika darasa hili. Usijali kujiona uko peke yako” Osaka akamwambia Shanga.
“Sitajali. Ondoa shaka”
Osaka akatoka.
“Kwa vile tuko wawili tu unaweza kukaa kwenye moja ya hizi meza zilizo mbele” Charly alimwambia Shanga ambaye alikwenda kukaa kwenye moja ya meza hizo.
Charly alimuwekea daftari na kalamu.
Mafunzo ya kwanza aliyopewa Shanga yalihusu kuwa tambua freemaso, kutambua itikadi zao, kanuni zao na salamu zao.
Alikuwa akiandikiwa maelezo na maswali ubaoni na yeye alitakiwa kuandika kwenye daftari yake pamoja na kujibu maswali.
Kabla ya muda wa mafunzo kwisha Charly alimuuliza Shanga.
“Mke na mtoto nani unamthamini zaidi?”
“Wote ninawathamini,” Shanga akamjibu.
“Kama unalazimishwa kutaja mmojawapo utamtaja nani.
“Hapo ni pagumu sana.
“Jaribu kutathmini na kufikiria.
“Kwa kweli wote ninawathamini.
“Hebu tujaribu kuwatathmini kwa pamoja. Mtoto ni damu yako, ni mrithi wako na msaidizi wako wa baadaye. Mke mlioana, ni mwandani wako, amekuzalia watoto wako na ni mwenzi wako wa maisha ingawa pia mnaweza kuachana na ukapata mke mwingine.
“Unaona, kote kunakuwa na uzito unaolingana. Si rahisi kusema unamthamini mmojawapo kuliko mwingine.”
Charly aliposikia hivyo alicheka na Shanga naye akacheka. Charly akabadili mazungumzo.
“Kwa leo tumemaliza mafunzo yetu. Mafunzo yataendelea kwa muda wa siku saba”
“Daftari na kalamu nitandoka navyo?”
“Hapana, unaacha hapa hapa kwa ajili ya masahihisho”
Shanga akaondoka kwenye kiti na kumpa Charly daftari na kalamu.
“Kwa hiyo ninaweza kwenda zangu”
“Unaweza kwenda kwenye maktaba yetu kujisomea vitabu kama utapenda”
“Ninapenda kujisomea lakini kwa leo muda hautaniruhusu”
“Sawa. Ukipata muda siku yoyote unaweza kwenda kujisomea. Tuna vitabu vingi na vya aina mbalimbali”
“Nitajitahidi”
“Sasa ngoja nikutoe”
Charly alimtoa Shanga na kumpeleka katika chumba alichokuwa ameketi Osaka. Kilikuwa ni kile chumba kilichokuwa na TV zilizokuwa zimepachikwa kwenye kuta. Chumba hicho kilikuwa ghorofani.
Osaka alikuwa ameketi kwenye sofa akiangalia moja ya TV hizo iliyokuwa ikionesha darasa walilotoka Charly na Shanga.
Shanga alihisi kwamba kulikuwa na kamera iliyokuwa ikiwachukua na Shanga alikuwa akiwaona moja kwa moja walipokuwa kwenye chumba hicho cha darasa.
“Mmemaliza mafunzo yenu?” Osaka aliwauliza huku akijiweka sawa kwenye sofa. Uso wake ulikuwa umeunda tabasamu la fadhaa. Pengine ni kwa sababu hakupenda Shanga agundue kuwa alikuwa akiwaangalia kwenye TV walipokuwa katika chumba hicho cha darasa.
“Tumemaliza,” Shanga ndiye aliyejibu na kuongeza “Nafikiri sasa ni muda muafaka kurudi nyumbani”
Osaka akanyanyuka kwenye kiti.
“Acha nikutoe nje.”
Huku akitangulia kwenye mlango walitka nje. Osaka alimsindikiza Shanga hadi kwenye gari lake na kuagana naye. Shanga akalitoa gari kwenye geti na kuondoka.
Siku iliyofuata Shanga alikwenda mapema zaidi ili kupata muda wa kujisomea katika chumba cha maktaba. Huko alitupia macho vitabu mbalimbali vyenye habari zao. Muda wa kuanza masomo ulipowadia alikwenda katika chumba cha darasa na kuendelea na mafunzo yake. Katika mafunzo ya siku ile Charly alimsisitizia sana Shanga kuepuka kuuliza uliza maswali.
“Ukiwa mwanachama wetu hutakiwi kuuliza uliza maswali, badala yake unangoja hadi utakapoelimishwa. Tuna maana kwamba kila kitu utakijua hata bila kuuliza” Charly alimwambia Shanga.
Shanga alimkubalia kwa kichwa. Baada ya mafunzo ya siku ile Charly alimwambia Shanga kuwa siku inayofuatia ni jumatano na alitakiwa kuhudhuria mafunzo ya jioni na mafundisho ya usiku.
“Nimeelewa” Shanga akamjibu.
Siku hiyo ya jumatano Shanga kama kawaida alihudhuria mafunzo ya jioni na alifika tena usiku kwa ajili ya mafundisho aliyoambiwa. Usiku huo alikuta watu wengi waliovalia suti nyeusi katika ghorfa ya chini.
Alichokuja kukigundua ni kwamba kile alichoelezwa kuwa ni mafundisho ilikuwa ni aina ya maombi au sala ambayo Shanga alihisi ilielekezwa kwa shetani.
Usiku huo Shanga alitambulishwa rasmi kama mwanachama mpya na mteule wa urais kupitia chama chake cha UM. Alikaribishwa na kushirikishwa katika maombi yaliyokuwa yakiongozwa na kivuli cha mtu kilichokuwa kwenye kioo.
Baada ya maombi kumalizika Shanga aliitwa mbele ya meza kuu. Alipokwenda mbele ya meza kuu sauti iliyotoka kwenye kivuli ilimuuliza kama kweli alikuwa tayari kuwa rais wa nchi ya Kamisa.
“Niko tayari” Shanga alijibu haraka.
“Tupe ahadi, kama utakuwa rais utatupa nani kati ya mtoto wako na mke wako?”
Swali hilo lilimshitua Shanga lakini alijikaza kiume asioneshe uoga. Akataka kuuliza mtoto wake au mke wake awape wao kwa ajili gani lakini alikumbuka kuwa alifundishwa kuepuka kuuliza maswali. Akanyamaza kimya huku akiwaza.
Alijiambia kwamba hata kama mtoto wake au mke wake watatakiwa kwa madhara na watu hao, asingeweza kukataa kwa sababu tayari alikuwa ameshajiunga na watu hao. Alijua kuwa jambo hilo hawakumueleza mapema kwa sababu waliona angekataa kujiunga.
Wakati akili yake ikitangatanga kutafuta jibu la ama kukataa ama kukubali kumsaliti motto wake au mke wake ili kupata urais, alipata wazo kwamba akubali kumtoa mwanawe. Ilikuwa ni kwa sababu watoto wake walikuwa wakisoma nje ya nchi. Ilikuwa si rahisi kutiwa mikononi na watu hao. Na pia aliona atakapopata urais atakuwa ikulu na hakutakuwa na yeyote atakayemlazimisha kutimiza ahadi yake ya kumtoa mwanawe. Aliendelea kujiambia kwa vile lengo lake la kujiunga na watu hao ni kupata urais, atakapoupata huo urais atajitoa kwenye kundi hilo na hakutakuwa na yeyote atakayemfuata ikulu na kumhoji kuhusu suala hilo.
“Shanga tunasubiri jibu lako” Sauti iliyotoka kwenye kivuli ilimshitua Shanga.
“Nitamtoa mtoto wangu,” Shanga alijibu haraka.
“Kumbuka kwamba hiyo ni ahadi na utalazimika kuitimiza utakapopata urais”
“Nitaitimiza.
“Vizuri. Suala la pili ni kwamba tunaihitaji wizara ya mambo ya ndani.
“Mnaihitaji kivipi?
“Yaani utakapokuwa rais uteue waziri wa mambo ya ndani kutoka kwetu.
“Hilo litawezekana.
“Kwa hiyo unatuahidi kuwa utateua waziri wa mambo ya ndani tutakayemtoa sisi?
“Ndiyo, mradi tu awe na sifa za uongozi.
“Sawa, suala la tatu katika utumishi wa ikulu tunataka uteue watu wetu wawili kuwa maofisa wako wa karibu utakapoingia ikulu.
“Hilo pia litapatikana.
“Sawa. Tunataka tupate uwakilishi ndani ya serikali yako.
“Hakuna tatizo, uwakilishi huo utapatikana nikiwa rais.
“Sasa kunja ngumi yako ya mkono wa kulia”
Shanga akakunja ngumi.
“Elekea kwenye meza kuu.
“Shanga alielekea upande uliokuwa na meza ndefu ambapo juu yake kulikuwa na mitungi mitatu iliyokuwa ikifuka moshi.
“Sema mimi Max Shanga ninaahidi.
“Mimi Max Shanga ninaahidi.
“Nitakapokuwa rais…
“Nitakapokuwa rais…
“Nitamtoa mwanangu kwenu.
“Nitamtoa mwanangu kwenu.
“Na nitawapa wizara ya mambo ya ndani.
“Nitawapa wizara ya mambo ya ndani.
“Na nitawateua wanachama wenzangu wawili kuwa maofisa wangu wa karibu nitakapokuwa ikulu.
“Vizuri. Sasa fungua mkono wako.
Shanga alikunjua kiganja chake alichokikunja ngumi na kushangaa alipokuta pete ikimeremeta kwenye kiganja chake!
“Ah! Kuna pete!,” akasema kwa kugutuka.
“Ni pete ya ushindi” Sauti ikamwambia kutoka kwenye kioo. Ikaongeza.
“Osaka mvalishe kwenye kidole chake cha pete cha mkono wa kushoto.
Osaka aliyekuwa amesimama karibu na Shanga aliichukua ile pete akaushika mkono wa kushoto wa Shanga.
“Nyoosha kidole chako cha pete.
“Shanga alinyoosha kidole hicho. Osaka akamvalisha ile pete.’
Watu waliokuwa kwenye viti walipiga makofi kistaarabu kumshangilia Shanga.
“Wakati wote wa kampeni hadi urais, hakikisha pete hiyo inakuwa kidoleni mwako. Utapata ushindi na utakuwa na dola yenye nguvu,” ilikuwa sauti iliyotoka kwenye kivuli kilichokuwa kwenye kioo.
“Nitahakikisha kuwa nitakuwa nayo wakati wote,” Shanga alisema akionyesha wazi kupatwa na kiwewe.
“Usiku mwema kwenu nyote” sauti ilimalizia kwenye kioo kabla ya kivuli hicho kutoweka.
Baada ya kivuli hicho kutoweka watu waliondoka kwenye viti na kwenda kumpa Shanga mkono wa pongezi. Wengine walidiriki kumuita mheshimiwa rais. Wakati wote alipokuwa akipeana mkono na watu hao Shanga alikuwa akitabasamu.
Baada ya watu hao kupeana mkono na Shanga waliagana naye na kuondoka mmoja mmoja.