Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 29
UTANGULIZI
Yule mtu aliirudisha simu yake mfukoni akachutama na kufungua lile begi. Alitoa furushi la kamba akawapa wenzake.
“Mfungeni kamba miguuni na mikononi. Jamaa anakuja sasa hivi”
Watu hao wakachukua lile furushi la kamba na kulichakua. Zilikuwa kamba nyingi ambazo zilikuwa vipande vipande.
Walichukua vipande hivyo vya kamba wakamfunga Frenk mikononi na miguuni.
“Sasa tusubiri hapa hapa” Yule aliyekuwa akiendesha gari aliwambia wenzake.
SASA ENDELEA
Alitazama saa yake kisha akatoa sigara na kujiwashia.
Baada ya kupita kama nusu saa hivi simu yake ikaita. Aliitoa mfukoni na kuipokea.
“Sasa mpakieni kwenye gari, muje naye chimboni. Mganga amesema kafara lake ni lazima lifanyike kwenye chimbo na huu ndio muda muafaka” Sauti ikasikika kwenye simu.
“Sawa”
Mtu huyo aliirudisha simu mfukoni akawambia wenzake wambebe yule kijana na kumpakia kwenye gari.
“Kwanini?” mmoja akamuuliza.
“Amesema kafara lake linatakiwa lifanyike chimboni”
“Yaani tutakwenda naye huko huko?”
“Hakuna tatizo. Hivi sasa ni saa nane usiku, kila mtu amelala. Nani atatuona?”
Walimbeba Frenk wakampakia katika siti ya nyuma ya gari hilo. Mtu mmoja alikaa naye kwenye siti. Mwingine alikaa siti ya mbele pamoja na aliyekuwa akiendesha gari hilo.
Gari likawashwa moto na kuondoka. Baada ya mwendo wa dakika kadhaa gari hilo likaingia katika viunga vya eneo la Marerani.
Lilisimama karibu na chimbo moja lililokuwa karibu na kibanda kimoja kilichojengwa kwa miti.
Aliyekuwa akiendesha alishuka na kwenda kwenye kile kibanda ambako kulikuwa na watu wawili waliokuwa wamekaa.
“Tumekuja naye” Mtu huyo aliwambia watu hao.
“Amezinduka?” Mmoja kati ya wale watu wawili waliokuwa wamekaa, akauliza.
“Hajazinduka na tumemfunga kamba”
“Sasa mtoeni kwenye gari. Mumburuze hadi pale kwenye chimbo. Fanyeni haraka. Hivi sasa watu wengi wamelala”
Mtu huyo alirudi tena kwenye gari akawambia wenzake wamtoe Frenk na kumburuza kwenye chimbo.
Wakati watu hao wakifanya hivyo, mtu aliyetoa agizo hilo alimuacha mwenzake amekaa, akaenda kwenye chimbo akiwa ameshika mfuko.
Alipofika kwenye chimbo hilo aliuweka chini ule mfuko akatoa pembe mbili zilizofungwa kwa vitambaa vyeusi na vyekundu.
Pia alitoa tunnguri mbili alizoziweka karibu na mlango wa chimbo hilo. Frenk aliletwa mahali hapo kwa kuburuzwa chini ambapo isingekuwa rahisi kwa mtu aliyekuwa mbali kumuona usiku huo kutokana na kutokuwepo kwa mwanga wa taa.
Frenk alilazwa kichali chali karibu na mlango wa chimbo. Yule mtu aliyetoa pembe na tunguri alichukua pembe moja na kumzunguka Frenk huku akimmwagia mavumba. Alimzunguka mara saba. Alipomaliza aliziweka zile pembe akachukua tunguri na kuzunguka nazo mara saba huku akitabana maneno ya kichawi.
Alipomaliza alivua nguo zake zote akafanya mauzauza kabla ya kuwambia wale watu kwamba wamchinje yule kijana. Mtu mmoja akamshika Frenk ili asifurukute na mwingine alitoa kisu na kukishika kichwa cha Frenk. Hapo hapo Frenk akazinduka.
“Kitu gani?” akauliza kwa mshangao.
Hakukuwa na aliyemjibu.
“Niko wapi hapa na kwanini nimeshikwa hivi na kufungwa?” akaendelea kuuliza.
Aliyekuwa amemshika alimshika vizuri. Yule aliyeshika kisu akaanza kumchinja harakaraka huku yule aliyevua nguo akisaidia kumshikilia asifurukute.
Kisu kilipoanza kukata koo, Frenk alianza kukoroma. Alijaribu kufurukuta lakini waliomshika walikuwa wamemdhibiti sawasawa.
Damu ikaanza kumwagika. Dakika tatu tu baadaye kichwa kilikuwa kimetenganishwa na kiwiliwili.
Ile damu iliunda mchirizi na kuchirizikia kwenye
Mlango wa chimbo.
Mwili wa Frenk uliendelea kushikiliwa mpaka ulipotulia kabisa.
Ndipo yule mtu aliyekuwa amekaa kwenye kile kibanda alipoinuka na kwenda mahali hapo.
“Tayari?” akauliza.
“Tayari” Mtu mmoja akamjibu.
“Sasa mrudisheni kwenye gari mwende mkamzike” Yule mtu aliyevua nguo alisema huku akivaa suruaIi yake.
Watu hao walishika miguu ya Frenk wakamburuza hadi kwenye gari. Wakafungua boneti la nyuma na kuutia mwili huo. Mmoja alirudi kufuatia kichwa cha frenk ambacho pia alikitia ndani ya boneti.
Aliyekuwa akiendesha gari hilo alikuwa amesimama akizungumza na yule mtu waliyemkuta hapo pamoja na yule mganga.
“Mtamzika mahali mbali na hapa. Mtakwenda kuchimba shimo refu ili mwilli wake usifukuliwe na fisi. Si mmesema hafahamiki?” Mtu huyo alimuuliza yule aliyekuwa akiendesha gari.
“Hafahamiki.Tumeambiwa kwamba alifika leo pale gesti, anamtafuta ndugu yake”
“Alitokea wapi?”
“Alitokea Dar es Salaam.”
“Atakuwa ni mgeni. Hakuna anayemfahamu. Sasa nendeni mkachimbe kaburi mumzike. Tukutane asubuhi”
“Sawa” aliyekuwa akiendesha gari alisema kisha akaondoka kuelekea lilikokuwa gari hilo. Alifungua mlango akajipakia na kuliondoa gari.
Mganga alikuwa akiitia michanga ile damu ya Frenk ili isionekane. Alipomaliza alimsogelea yule mtu aliyekuwa naye ambaye alikuwa amesimama kando yake.
“Naona kazi imekwisha. Sasa zingatia vile nilivyokueleza. Asiingie mtu kwenye chimbo hili mpaka baada ya siku tatu. Wataingia watu watatu tu wakiwa uchi. Umenielewa?”
“Nimekuelewa vizuri”
“Hawatafukua umbali mrefu watakuta mwamba ambao watautoboa. Huo mwamba una mali za majini ambazo huwezi kuzipata mpaka ufanye kafara la roho kama tulilolifanya hapa”
Mganga huyo aliendelea kumwambia Amon.
“Wakishapata hizo mali watatoka wakiwa uchi. Watavaa nguo watakapotoka. Sijui kama unanielewa vizuri?”
“Nakuelewa vizuri”
“Mali watakayopata itatosha kukupa utajiri katika maisha yako yote na hutakiwi kurudia mara ya pili. Ukishapata hiyo mali nenda katafute biashara nyingine ufanye, ukirudia mara ya pili utakufa”
“Sawa mzee”
“Kingine ninachotaka kukukumbusha ni kuwa katika utajiri wako kila mwaka ukazamishe baharini fedha za mapato yako ambazo ni sawa na theluthi moja ya mapato yako. Hiyo ni zaka ya majini waliokupa mali”
“Kama kweli nitafanikiwa nitafanya hivyo. Lakini ningependa kujua hizo fedha niziweke kwenye nini kabla ya kuzizamisha baharini”
“Swali zuri sana. Hizo pesa utazitia kwenye mfuko mweupe. Utashona mfuko mweupe. Utaweka na jiwe ili ziweze kuzama chini. Unaweza kukodisha boti ikupeleke mbali kidogo”
“Sawa. Nimekuelewa”
************
Kilichotokea ambacho Amon hakukijua ni kuwa wale watu aliokuwa akishirikiana nao waliyempelekea kijana ambaye alikuwa ni ndugu yake aliyekwenda Arusha kumtafuta yeye.
Mhudumu wa pale gesti alipofikia alishaambiwa akipata mtu ambaye ataweza kutolewa kafara kwenye machimbo atapewa shilingi milioni mbili. Alipomuona Frenki alikuwa mgeni na alikuwa akimtafuta mwenyeji wake ambaye hakuwa akifahammika ndipo alipowapigia simu kina Amon na kuwambia waje usiku kumchukua Frenk.
Jamaa hao wakafika usiku na kumwambia Frenk kuwa wanamfahamu kaka yake aliyekuwa anamtafuta na kwamba wanaweza kumpeleka aliko. Wakaenda kumchinja bila Amon kujua kuwa aliyechinjwa alikuwa ni ndugu yake aliyekwendaArusha kumtafuta.
Kama walivyoambiwa na mganga baada ya kafara hilo walilofanya, Amon alipata madini yaliyompatia fedha nyingi. Akafuata masharti ya mganga kwamba asiendelee tena kuchimba. Akaondoka Marerani na kurudi Dar.
Alirudi Dar akiwa na ugomvi na wenzake waliokuwa wakidai aliwapunja pesa, mmojawapo akiwa Mosha aliyewahi kukamatwa na polisi wilayani Kibaha kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watoto wa Almasi kutokana na uhasama waliokuwa nao.
Kutokana na fedha alizopata, Amon aliweza kujenga nyumba ya kifahari pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara. Baadaye akanunua kiwanda cha maji safi kutoka kwa mfanyabishara mmoja mwenye asili ya kiasia.
Kiburi cha pesa kikamfanya Amon alibadili jina lake na kujiita Almasi. Baada ya kupata utajiri Amon sasa akiwa na jina la Almasi akawa mcha Mungu akitubu makosa yake lakini siku moja moja akinywa pombe.
Katika mwaka wake wa kwanza wa utajiri, Almasi alitimiza lile sharti aliloambiwa la kumwaga robo ya mapato yake baharini. Ilimpa usumbufu mkubwa kufanya mahesabu ili kupata robo ya pesa alizokuwa nazo. Pia alipata usumbufu kupata sarafu za mamilioni ya shilingi ambazo alitakiwa akizimwage baharini.
Alipofanya hivyo mara ya kwanza akaona ulikuwa upuuzi kuendelea na zoezi hilo. Mbali ya usumbufu alioupata kubadili pesa zake katika sarafu, pia aliona alikuwa akipoteza pesa zake bure kuzimwaga baharini.
Hakutaka kuamini kuwa kulikuwa namajini chini ya bahari waliokuwa wakihitaji pesa hizo. Alichotaka kukiamni ni kuwa masharti mengine ya waganga si lazima yafuatwe, mradi ameshapata utajiri hakukuwa na haja tena ya kuendelea kutekeleza masharti ambayo yalikuwa yanamtia hasara. Akaacha.
Miaka kadhaa ikapita.
Mwisho akasahau kabisa kama kuna masharti alipewa na ameacha kuyatekeleza.
Ndipo siku moja mtoto wake wa kwanza aliyemuita Martin alipovamiwa na watu watatu wa ajabu, akachinjwa na kunyang’anywa mkoba wa pesa….
Sasa Almasi akiwa kwa mganga waliyemwendea yeye na Maria alitingisha kichwa chake taratibu baada ya kuwaza.
“Nimekumbuka kitu…” akamwambia mganga kwa sauti iliyonywea.