Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 28
UTANGULIZI
“Sasa wewe nenda, siku yoyote ukiona una mpango wa kupata mtu nipigie simu”
“Sawa. Sasa utakapoifanya hiyo kazi utahitaji kiasi gani?”
“Hii kazi ni kubwa na kima changu ni shilingi milioni mojananusu”
“Mbona ni kiasi kikubwa sana?”
“Ndiyo kima changu na ni kwa sababu nina uhakika kwamba utapata utajiri kwani wengi wamefanikiwa”
SASA ENDELEA
“Naona una uhakika na kazi yako. Nitakutafutia hiyo pesa kisha nitakupigia simu kukujulisha kama nimepata mtu.”
“Sawa.”
Amon akarudi Marerani na kuwaeleza wenzake mpango huo wa kutoa mtu kafara ambao wenzake walikubaliana nao.
Baada ya siku tatu, mdogo wake Amon, aliyetoka Mwanza na kwenda Dar kumtafuta kaka yake na kumkosa, aliwasili jijini Arusha baada ya kuambiwa kuwa Amon alihamia Arusha.
Ili twende pamoja vizuri, hebu tujikumbushe Frenk alivyofika Dar na kisha kwenda Arusha baada ya kuambiwa kaka yake Amon yuko Arusha.
…..Daladala ilipomshusha Kariakoo, aliamua kwenda Ilala kwa miguu. Aliutafuta mtaa aliotajiwa. Alipoupata, aliitafuta nyumba ya Amon ambayo namba yake alikuwa ameikariri. Akaipata.
Alipoiona nyumba aliyokuwa akiitafuta, alipata furaha iliyochanganyika na mshituko. Alipata furaha kwa sababu aliiona nyumba aliyokuwa akiitafuta, lakini alipata mshituko kuona nyumba yenyewe ilikuwa ya kawaida na si ya kifahari kama alivyoambiwa na baadhi ya watu huko Mwanza.
Alibisha kwenye mlango. Mlango ukafunguliwa na kijana mmoja ambaye alikuwa akitoka na hamsini zake.
Frenk akamsalimia. Baada ya salamu, akamuuliza.
“Sijui nimemkuta Amon?”
“Amon nani?” kijana akamuuliza.
“Amon Marwa.”
“Oh! Amon aliondoka kwenda Arusha.”
“Alienda lini?”
“Mh! Muda kidogo, inafika miezi sita.”
“Mke wake yupo?”
“Alipoondoka, alimuacha mke wake, lakini alishindwa kulipa pango ikabidi aende kwao.”
“Kwani Amon alikwenda kufanya nini huko Arusha?”
“Siwezi kujua, lakini kuna watu walisema walikuwa wanamkuta kwenye gesti moja jirani na stendi ya mabasi pale Arusha.”
Ndoto ya kumpata kaka yake ikayeyuka kichwani mwake kama bonge la barafu lililotiwa kwenye ndoo ya maji.
“Kwani hapa Dar alikuwa akifanya shughuli gani?” akamuuliza yule kijana kwa sauti ya kukata tamaa.
“Alikuwa akifanya biashara ya duka, lakini alifilisika. Nafikiri labda aliamua akatafute maisha huko Arusha.”
Yule kijana akaondoka na kumuacha Frenk akiwa ameduwaa kando ya mlango.
Jirani na hapo palikuwa na gesti. Frenk akajikuta akitembea kwa mwendo wa taratibu kuelekea katika gesti hiyo, ambapo alipanga kuchukua chumba cha kulala baada ya kumkosa kaka yake.
Asubuhi kulipokucha, Frenk akapata uamuzi wa kwenda Arusha kuendelea kumtafuta Amon. Alikuwa na imani kuwa huenda alikuwa amefanikiwa huko Arusha na mahali pa kwanza pa kumtafuta ni hapo gesti ambapo aliambiwa alikuwa akionekana.
Alipanda basi la asubuhi sana kwenda Arusha. Karibu safari nzima alikuwa akimuwazia kaka yake. Alijiambia endapo atafanikiwa kuonana naye, atakuwa ametimiza lengo lake.
Alijua kuwa angeweza kumkuta akiwa na mafanikio au akisaga lapa kama yeye. Lakini kwa vyovyote itakavyokuwa, alijiambia, kule kukutana kwao tu kungeweza kuwa mwanzo wa mafanikio yao.
Alifika Arusha jioni. Aliposhuka kwenye basi, alikwenda kuitafuta gesti aliyoambiwa iliyokuwa jirani na stendi. Baada ya kuulizauliza wenyeji, alielekezwa gesti hiyo. Akaenda kuonana na mhusika.
Alipomuuliza kaka yake, aliambiwa walikuwa hawamfahamu.
“Alitoka wapi?” kijana wa gesti akamuuliza.
“Alitoka Dar kama miezi sita iliyopita. Niliambiwa alikuwa akionekana katika gesti hii.”
“Hapa kwetu wanafika watu wengi kutoka Dar, hatuwezi kujua ni nani mmojawapo.”
“Nimesema anaitwa Amon.”
“Amon wako wengi. Hatuwezi kujua ni Amon yupi unayemuuliza wewe.”
“Yeye ni Amon Marwa.”
“Yukoje?”
“Tuliachana Mwanza tukiwa wadogo. Sijui umbo lake lilivyo kwa sasa. Wakati huo alikuwa ni mwembamba.”
“Kwa kweli itakuwa ni vigumu kumtambua.”
Baada ya maelezo yake kutosaidia kumtambulisha aliyekuwa anamtafuta, aliamua kukodi chumba hapo hapo. Akajiambia atamtafuta kaka yake kwa siku mbili. Endapo hatafanikiwa kumpata, atarudi Mwanza.
Baada ya kupata chumba, akaoga, akabadilisha nguo alizokuwa amevaa, kisha akatoka kwenda katika mkahawa uliokuwa karibu kupata chakula.
Baada ya kula, alirudi gesti kulala. Hakukumbuka ilikuwa saa ngapi alipoamshwa usingizini. Kwanza alidhani alikuwa anaota baada ya kusikia mlango wa chumba alichokuwa amelala ukibishwa.
Baada ya fahamu kumrudia vizuri, aligundua kuwa hakuwa akiota, bali mlango ulikuwa unabishwa kweli. Akainuka kitandani na kwenda kuufungua.
Alimkuta kijana aliyempangisha chumba hapo gesti akiwa na mtu mmoja ambaye alimwambia alikuwa akimfahamu mtu aliyekuwa akimuulizia.
“Unamfahamu Amon?” Frenk akamuuliza yule mtu kwa mshituko.
“Ndiyo, namfahamu. Aliwahi kukaa hapa gesti kwa muda mrefu, hivi sasa yuko wilaya ya Simanjiro anafanya biashara.”
“Sasa nitampataje?”
“Mimi naenda huko huko. Kama unataka twende, nitakupeleka mahali aliko.”
“Kweli tutapata usafiri usiku huu?”
“Nina gari yangu binafsi, tunaweza kwenda tu.”
“Basi subiri nivae twende.”
Frenk akarudi ndani. Alivaa nguo haraka haraka, akachukua begi lake na kutoka. Yule mtu alikuwa akimsubiri ukumbini.
“Twenzetu,” akamwambia.
Walitoka nje ya gesti, ambapo palikuwa na gari aina ya Noah iliyoegeshwa.
Ndani ya gari hilo kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa amekaa siti ya nyuma.
Frenk aliambiwa akae siti ya mbele kando ya dereva. Akafungua mlango na kujipakia.
Yule mtu naye alikaa katika siti ya dereva, akaliwasha gari na kuanza safari ya kuelekea wilaya ya Simanjiro.
“Mimi naitwa Rafael, je, wewe mwenzangu unaitwa nani?” mtu huyo alimuuliza Frenk baada ya kimya kifupi.
“Mimi naitwa Frenk.”
“Huyu Amon ni nani wako?”
“Ni kaka yangu. Tuliachana zamani sana huko Mwanza.”
“Alikuja hapa Arusha miezi sita iliyopita. Hivi sasa anaishi Simanjiro na amefanikiwa sana kimaisha.”
“Nitafurahi sana kumuona kaka yangu. Uliniambia kuwa mnafahamiana?”
“Tunafahamiana na tunahisi jirani. Wewe hujawahi kufika hapa Arusha?”
“Sijawahi kufika.”
“Na huko Simanjiro ndiyo hukujui kabisa?”
“Kwa kweli huko sikujui.”
“Basi leo utakujua.”
“Nitafurahi.”
Safari ikaendelea. Gari hilo liliwasili Simanjiro saa nane usiku. Lilisimama mbele ya nyumba moja, ambapo aliyekuwa akiendesha alishuka akaenda kubisha mlango.
Baada ya muda kidogo, mlango ulifunguliwa, mtu huyo akaingia ndani.
Haikupita muda mrefu, akatoka akiwa na mwenzake aliyekuwa ameshika begi. Mwenzake alijipakia katika siti ya nyuma. Akakaa na Frenk.
“Vipi bwana?” akamuuliza Frenk.
“Salama tu.”
Gari likawashwa moto na kuendelea na safari.
“Hivi sasa tunakwenda nyumbani kwa Amon,” aliyekuwa akiendesha alimwambia Frenk.
“Nimbali sana kutoka hapa?”
“Hapana. Ni karibu tu.”
Baada ya mwendo mfupi, walivuka daraja, wakaingia katika barabara za vichochoro. Walitokea katika eneo ambalo lilikuwa na pori. Baada ya kulipita pori hilo, gari likasimama ghafla karibu na kichaka.
Aliyekuwa akiendesha alisonya kisha akafungua mlango.
“Hili gari limeshaanza matatizo. Limezima ghafla,” alijisemea kabla ya kushuka na kwenda mbele ya gari hilo, ambapo alifungua boneti la mbele.
Wenzake waliokuwa katika siti ya nyuma nao walishuka na kumfuata.
Frenk alipoona amebaki peke yake ndani ya gari, naye alishuka. Alikwenda mbele ya gari hilo kulikokuwa na wenzake waliokuwa wakilikorokocha gari hilo.
“Lina tatizo gani?” Frenk akauliza.
Mtu aliyekuwa karibu yake aligeuka ghafla na kumpiga kwa kitu kizito kichwani. Frenk alipiga yowe akaanguka hapo hapo akiwa amepoteza fahamu.
Mtu aliyempiga aliinama, akamshika mikono na kumburuza kwenye kichaka kilichokuwa pembeni mwa njia. Alimuingiza ndani ya kichaka hicho, akamlaza chini.
Wenzake walimfuata. Yule aliyekuwa akiendesha gari alikuwa ameshika begi ambalo aliliweka chini.
Alitoa simu kutoka mfukoni mwake akaipiga. Baada ya muda kidogo, simu yake ilipokelewa.
“Tumeshampata yule mtu na tuko naye hapa njia panda ya kuja Marerani. Sasa njoo mara moja tumshughulikie,” akasema kwenye simu.
“Ni kijana?” sauti ikauliza kutoka kwenye simu.
“Bado ni kijana sana na ana umbile lililotakiwa.”
“Mmemfunga sawasawa?”
“Samueli amempiga kichwani kwa kitako cha bastola, amezirai.”
“Sasa mmemfunga? Akizinduka anaweza kuleta usumbufu.”
“Sawa, tutamfunga kamba mikononi na miguuni.”
“Mkishamfunga, mnisubiri hapo hapo.”
“Sawa.”
Yule mtu aliirudisha simu yake mfukoni, akachutama na kufungua lile begi. Alitoa furushi la kamba, akawapa wenzake.
“Mfungeni kamba miguuni na mikononi. Jamaa anakuja sasa hivi.”
Watu hao wakachukua lile furushi la kamba na kulichakua. Zilikuwa kamba nyingi ambazo zilikuwa vipande vipande.
Walichukua vipande hivyo vya kamba, wakamfunga Frenk mikononi na miguuni.
“Sasa tusubiri hapa hapa,” yule aliyekuwa akiendesha gari aliwambia wenzake.