Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 26

MAUAJI 26 Pict

UTANGULIZI

“Unajua kuna kuua kwa mdomo. Unaweza kumwambia mtu nitakuua na kesho akakutwa ameuawa kweli, basi muuaji utakuwa wewe”

“Mimi nilikuwa sijui. Nilisema kwa mzaha tu”

“Elias kamuweke ndani mpaka pale atakapokuwa tayari kutueleza anachokijua”

“Yesu wangu! Mnataka kuniweka ndani, kwani Almasi ameuawa?”

“Watoto wake wameuawa na umesema na yeye atauawa”

SASA ENDELEA


“Sasa ndiyo niwekwe ndani?”

“Ndiyo. Umesema Almasi atauawa. Tukikuachia halafu akaja kuuawa kweli, tutamlaumu nani?”

Mosha akatikisa kichwa kusikitika.

Elias alimchukua Mosha na kwenda kumweka ndani.

Baada ya mazishi ya Benjamin, mke wa Almasi alianza kuwa katika hali kama ya kuchanganyikiwa.

Mdogo wake wa kike aliyeitwa Maria, ambaye alikuwa akiishi Tegeta, alikwenda kumchukua na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji ambaye alikuwa akiishi huko huko Tegeta.

“Mna tatizo gani?” mganga aliwauliza.

“Tuna shida kubwa. Dada yangu amekuwa katika hali ya kuchanganyikiwa tangu mtoto wake alipouawa. Walianza kuuawa kaka zake mmoja baada ya mwingine…”

“Hao watoto wameuawa na nani?” Mganga akauliza.

“Kusema kweli ni matukio ya ajabu…”

Maria alimueleza mganga huyo mkasa mzima wa kuuawa kwa watoto wa dada yake, tangu alipouawa mtoto wa kwanza hadi wa mwisho, na kusababisha mama yao aanze kuchanganyikiwa.

Mganga, baada ya kumsikiliza kwa makini, alimwambia:

“Hebu subiri nimuite jini wangu.”

Wote walidhani kuwa mganga huyo angepandisha mashetani kama ilivyo kwa waganga wengine, lakini walimuona akisema peke yake kwa sauti ya chini. Alikuwa akiuliza maswali kisha akiitikia yeye mwenyewe, kama aliyekuwa akipewa majibu.

“Sasa subiri niwaeleze,” mganga akasema baada ya kusema peke yake kwa sekunde kadhaa.

Akamtazama Maria pamoja na mke wa Almasi.

“Mliwahi kuweka nadhiri hapo zamani?” akawauliza.

Maria akamtazama dada yake.

“Sisi hatujawahi kuweka nadhiri,” mke wa Almasi akajibu.

Mganga akaendelea kusema peke yake, kisha akamuuliza mke wa Almasi:

“Mume wako hakuwahi kuweka nadhiri?”

“Hakuwahi.”

“Hapa kuna nadhiri inamhusu mume wako. Huenda wewe hujui, lakini mume wako anajua. Aje yeye nizungumze naye.”

“Sijui kama atakubali kuja huku.”

“Hili tatizo bado lipo, halijakwisha.”

“Una maana gani?”

“Mauaji yataendelea.”

“Yataendelea kwa nani wakati watoto wote wamekwisha?” Maria akauliza.

“Yataendelea katika hii familia ya Almasi.”

Maria akatazamana na mke wa Almasi kwa taharuki.

“Sasa ngoja mke wake akajaribu kumshawishi ili aje akusikilize. Kwa maana hili tatizo limetutisha,” Maria akamwambia mganga.

“Sawa. Nendeni mkamueleze, kama atakubali kuja itakuwa vizuri,” mganga aliwaambia.

Maria na mke wa Almasi wakatoka. Gari likawarudisha nyumbani kwa Almasi.

Walimkuta Almasi amekaa sebuleni akipekua kurasa za Biblia, mguu mmoja akiwa ameuweka juu ya mwingine.

Wakamsalimia. Almasi aliwaitikia kisha akaiweka Biblia juu ya stuli iliyokuwa kando yake.

“Habari za huko?” akawauliza.

“Nzuri. Tulienda kwa mganga mmoja, naye ametupa maelezo ya kutisha,” mke wake akamwambia.

“Amewapa maelezo gani?” Almasi akamuuliza.

Mke wake akamueleza walivyoambiwa na mganga.

Almasi, baada ya kumsikiliza, alitikisa kichwa.

Alichukua ile Biblia akamuonyesha mke wake huyo.

“Mimi naamini hiki kitabu. Waganga ni waongo sana. Mara nyingi wanakuwa na maono ya kishetani. Wao na mashetani wanakaa nyumba moja. Ndiyo maana unaona kila mganga lazima awe na shetani. Mimi sijaweka nadhiri mahali popote. Huyo mganga ni mnafiki mkubwa. Alikuwa anataka kuwala pesa zenu tu.”

“Ni kweli, lakini ungekwenda kumsikiliza tu, shemeji. Kama utaona ni muongo, utaachana naye,” Maria akamwambia.

“Sitathubutu kuinua mguu wangu kwenda huko. Kama ni watoto wangu wameshakufa wote, sasa nani tena atauawa na kwa kosa lipi?”

“Hata hali ya dada si unaiona si nzuri?”

“Dada yako amechanganyikiwa kutokana na haya matukio. Ninaamini baadaye atakaa sawa tu. Kila Jumapili anafanyiwa maombi. Msiwe na wasiwasi.”

Juhudi za Maria na mke wa Almasi kumshawishi Almasi aende kwa mganga zikakomea hapo hapo.

Almasi aliendelea kusoma Biblia yake kwa utulivu. Baada ya nusu saa hivi, alimuaga mke wake akamwambia kwamba anakwenda kumuona mchungaji.

Akatoka na gari lake na kuelekea katika ofisi ya mchungaji huyo iliyokuwa ndani ya kanisa lao.

Aliliegesha gari katika eneo la kuegeshea, akaingia ndani ya kanisa hilo. Punde tu alitokea kwenye mlango wa ofisi ya mchungaji. Alibisha mlango, alipojibiwa aliufungua na kuingia.

“Oh, Bwana Almasi, karibu sana,” mchungaji aliyekuwa amevaa suti nyeupe alimkaribisha.

“Asante. Bwana na asifiwe.”

“Ameen. Karibu kiti.”

Almasi akakaa kwenye kiti kilichokuwa mbele ya meza ya mchungaji.

“Kuna tatizo lolote au umenitembelea tu?”

“Matatizo yangu ni yale yale. Kuna jambo limetokea leo.”

“Jambo gani?”

“Mke wangu amepelekwa kwa mganga na mdogo wake hata bila ruhusa yangu.”

Mchungaji akatikisa kichwa kusikitika.

“Kwanini? Alifuata nini kwa mganga? Na ameambiwa nini huko?”

“Ameambiwa eti kuna nadhiri iliyokuwa inawaua watoto wangu.”

“Nadhiri gani?”

Almasi akabetua mabega yake.

“Siijui. Tena mganga amekwenda mbali zaidi. Amemwambia kuwa mauaji yataendelea iwapo mimi sitakwenda kwake.”

“Mara nyingi katika kutubu makosa ni lazima uungame makosa yako. Almasi, hebu niambie uliwahi kufanya kosa gani huko nyuma?”

“Sikuwahi kufanya kosa lolote.”

“Hukuwahi kuwa mshirikina?”

“Sikuwahi hata siku moja.”

“Kwanini mganga alikwambia uliwahi kuweka nadhiri?”

“Ni muongo.”

“Umesema kweli. Kazi za uganga zimetawaliwa na uongo na maono ya kishetani. Usiende huko na umkataze mke wako aache kwenda kwa waganga. Yesu ndiyo jibu la kila kitu. Umenielewa?”

“Nitamkataza mke wangu na mimi sitathubutu kuingia katika majaribu mengine.”

Wakati Almasi anarudi nyumbani, aliyatafakari maneno ya mchungaji wake na kuona yalikuwa sahihi.

Tangu mtoto wake wa mwisho alipouawa, alikuwa amemrudia Mungu wake na kuwa muumini mzuri wa kanisa.

Lakini bado mambo yalikuwa yakimchanganya kichwani mwake kiasi kwamba aliona akili yake ilikuwa haifanyi kazi kabisa.

Akaona si vibaya aende akapate angalau bia moja kuchangamsha akili.

Akasimamisha gari mbele ya hoteli moja na kuingia hotelini humo. Aliagiza chupa moja ya bia. Baada ya kunywa bia moja, aliona aongeze ya pili. Akili yake ilipoanza kuchangamka, akaongeza bia ya tatu.

“Baada ya hii siongezi tena,” akajisemea moyoni.

Lakini baada ya kunywa bia ile, alijikuta akiongeza bia ya nne.

“Ewe shetani niachie, hii iwe bia ya mwisho,” akajiambia.

Alipomaliza tu kupiga funda la mwisho la bia, akainuka haraka kwenye kiti. Kwa vile alikuwa ameshalipia bia hizo, aliondoka haraka. Alitoka nje ya hoteli, akajipakia kwenye gari lake na kurudi nyumbani.

Alipofika nyumbani kwake, alimuita mke wake na kumfokea kutokana na kitendo chake cha kwenda kwa mganga. Maria alikuwa ameshaondoka.

Alimwambia alikuwa amekwenda kumshitakia kwa mchungaji wao na akampa ujumbe uliotoka kwa mchungaji huyo kwamba aache kabisa kwenda kwa waganga.

Baada ya mke wake kumuomba msamaha, Almasi alikwenda kuketi kwenye kochi. Usingizi ukampitia hapo hapo, akalala fofofo.

Ilikuwa kama saa nne usiku alipozinduka. Aliona taa za nyumba nzima zilikuwa zimezimwa. Akatazama saa yake na kuona ilikuwa saa nne usiku.

Akajiuliza ni nani aliyekuwa amezima taa. Kabla ya kupata jibu, akasikia sauti ya mwanaume ikiuliza kutoka chumbani mwake.

“Wewe ni mke wa Almasi?”

Akatega masikio yake kusikiliza.

“Ndiyo, mimi ni mke wa Almasi,” sauti ya mke wake ikajibu.

“Mume wako alikuweka kama dhamana, lakini umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana,” sauti hiyo ya kiume iliendelea kumwambia.

Maneno hayo yakamshitua Almasi. Kutokana na ule ulevi, akataka ainuke ili akimbie, lakini lile giza likamzuia.

“Aliniweka dhamana wapi?” akaisikia sauti ya mke wake ikiuliza kutoka chumbani.

“Muda wako ndio umeishia hapa. Huwezi kupata jibu.”

Hapo hapo akasikia sauti ya mtu anayekoroma. Ghafla akaona taa zinawaka.

Ni nani aliyeziwasha?

Akainuka kwenye kochi na kupiga hatua za haraka kuelekea chumbani kwake. Aliusukuma mlango akapiga hatua kuingia ndani.

Kama angepiga hatua ya pili, angeukanyaga mchirizi wa damu ulioelekea kwenye mlango.

Mke wake alikuwa amelala chini hatua chache mbele yake. Kichwa chake kilikuwa kimetenganishwa kabisa na kiwiliwili!

“Yesu wangu!” akaguta. Kisha akajisemea:

“Mke wangu naye ameshauawa!”

Aliogopa kuingia ndani zaidi, akatoka nje ya chumba na kufunga mlango.

“Hawa watu wamekuja kumuua mke wangu humu humu ndani!” akaendelea kujisemea huku akipiga hatua za haraka kutoka nje.