Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 25
Muktasari:
- Makachero hao wakatoka. Walikwenda katika gesti ya Mosha wakashuka kwenye gari. Vile ambavyo walivaa kiraia na gari walilotumia lilikuwa na namba za kiraia, hakukuwa na mtu yeyote aliyewatambua kuwa ni makachero.
UTANGULIZI
Makachero hao wakatoka. Walikwenda katika gesti ya Mosha wakashuka kwenye gari. Vile ambavyo walivaa kiraia na gari walilotumia lilikuwa na namba za kiraia, hakukuwa na mtu yeyote aliyewatambua kuwa ni makachero.
SASA ENDELEA
WALIPOINGIA katika gesti hiyo walikutana na mhudumu wa gesti ambaye walimueleza kuwa awalikuwa wakimhitaji mwenye gesti ile.
Mhudumu kwa kudhani walikuwa maafisa wa serikali aliwambia.
“Mzee yuko uani”
“Anafanya nini uani” Eliasakamuuliza.
“Nendeni tu, mtamkuta amekaa”
Amour na Elias wakaenda uani. Kulikuwa kumewekwa meza moja na kiti. Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kiti hicho akinywa kilevi.
Juu ya meza kulikuwa na chupa kadhaa za bia. Aliyekuwa anakunywa alionekana tayari alikuwa ameshalewa.
Amour na Elias walipomuona walijua ndiye yeye Mosha. Wakamfuata.
“Habari yako mheshimiwa?” Elias akamsalimia.
Mtu huyo aliinua uso na kuwatazama.
“Nzuri. Karibuni”
“Hakuna viti tutakaribia wapi?” Elias alimwambia.
Mtu huyo alipaza sauti ya kilevi akamuita mhudumu.
“Hebu njoo hapa!”
Mhudumu akafika mara moja.
“Waletee viti hawa wageni” akamwambia bila kujua walikuwa kina nani.
Mhudumu alipoondoka mtu huyo aliwauliza.
“Mnatoka wapi?”
“Tunatoka Dar. Tulikuwa tunamhitaji bwana Mosha” Amour alimjibu.
“Mosha nani?”
“Mosha mwenye gesti hii”
“Mwenye gesti hii ni mimi. Mlikuwa mnahitaji vyumba au mwenye gesti?’
“Tunamhitaji mwenye gesti”
“Mwenye gesti mmempata, ndiye mimi”
Mhudumu alileta viti viwili. Akaviweka mbele ya meza.
“Karibuni” akawambia.
Amour na Elias wakakaa.
“Mlikuwa mna shida gani?” Mosha akawauliza huku akiwatazama kwa zamu.
Makachero hao walitazamana kabla ya kutoa vitambulishona kumuonesha mtu huyo.
“Sisi nimaafisa wa polisi kutoka Dae es Salaam. Tulikuwa tuna mazungumzo na wewe” Amour akamwambia.
Mosha aligutuka kidogo. Macho yake yakaonekana kuwa makali.
“Mna mazungumzo gani?”
“Tulisikiakwamba uliwahi kufanya biashara ya madini zamani. Ni kweli?” Amour akamuuliza.
“Nilifanya zamani sana”
“Unamfahamu mtummoja ambaye alikuwa akifanya biashara hiyo anaitwa Almasi”
“Yule tapeli! Anajifanya ni tajiri lakini utajiri wake ni wa wizi mtupu! Alinidhulumu pesazangu, yule sitamsahau hadi kufa!”
Amour akamtazama Elias. Kisha akayarudisha macho yake kwa Mosha.
“Alikudhulumu kiasi gani?”
“Pesa nyingi tu lakini niliamua kuachana naye. Nilikuja hapa Kibahanikaanzisha biashara nyingine”
“Ametuambia kwamba mna uhasama hadi leo?”
“Mpumbavu yule…!”
Mosha alimimina bia kwenye bilauli.
“Niwaagizie bia?” akawauliza.
“Hapana. Wewe endelea kunywa tu” Amour akamwambia.
Mosha akapiga funda la bia kisha akairudisha bilauli juu ya meza.
“Lakini atalaanika tu, utajiri wote utamtoka!” akajisemea kabla ya kuulizwa chochote.
“Bado mnafuatana fuatana hadi sasa?” Amour akamuuliza.
“Mimi sina shughuli naye yeyote dhalimu yule lakini ninajua iko siku atanifuata mwenyewe anipigie magoti”
“Utamfanya nini?”
“Ninajua mwenyewe” Mosha alisema kisha kama aliyejigutuka akauliza.
“Mliniambie nyie ni maafisa wa nini…?”
“Tulikwammbia kwamba sisi ni maafisa wa polisi kutoka Dar” Amour akamwambia.
“Mlikuwa mnahitajii nini?”
“Kujua uhusiano wako na Almasi”
“Kwani kumetokea nini?”
“Inasemekana kwamba mauaji ya watoto wake yanatokana na wizi aliowafanyia wenzake katika biasharaya madini”
“Watoto wake wanauawa? Bado hata yeye atauawa!”
Amour akamtazama Elias kisha akayarudisha tena macho yake kwa Mosha.
“Una uhakika kwamba hata yeye atauawa?”
“Nina uhakika”
“Atauawa na nani?”
Mosha aliinua bilauli iliyokuwa juu ya meza akapiga funda la kilevi kilichokuwemo kisha akairudisha na kumkazia macho Inspekta Amour.
“Atauawa na walimwengu. Wewe ukiwa mtu wa kudhulumu dhulumu tu ujue mwisho wako utakuwa mikononi mwa wenzako”
“Inaelekea unaujua vizuri mpango wa kuuawa kwa watoto wake” Amour alimwambia kisha akainuka.
“Nitaujuaje wakati yuko Dar, mimi niko Kibaha” Mosha alimwambia huku akibetua mabega yake.
Alitoa sigara akaipachika midomoni na kuiwasha.
“Unakwenda wapi?” akamuuliza Amour aliyekuwa akipiga hatua pembeni.
“Maelezo yako yana utata. Umesema Almasi pia atauawa kama walivyouawa watoto wake kwa sababu ya kudhulumu watu?” Elias akamuuliza.
Amour alikuwa ametoa simu akiongea kwa pembeni.
“Ndio ninavyoona mimi. Sasa unadhani hao watoto wake wanauawa na nani?”
“Inaelekea wewe unajua mengi, ndio tunataka utueleze” Elias alimwambia.
“Kama nyinyi ni polisi mwende mkamuulize wenyewe”
Amour alirudi na kuketi.
“Mosha una biashara gani zaidi ya hii gesti?” Amour akamuuliza Mosha.
“Sina biashara nyingine. Nilikuwa nafuga kuku wa mayai lakini binaadamu waliwatia zongo, unawalisha kuku lakini hawatoi mayai. Nikaamua kuachana nayo. Nikabaki na hii gesti tu. Nashukuru napata riziki yangu”
“Una mke na watoto?”
“Sasa umri huu nitakuwa sina mke wala mtoto, itawezekana kweli?”
“Una watoto wangapi?”
“Nina watoto watano. Nasi watoto, ni vijana wakubwa. Wawili wana kazi zao. Wengine bado wanasoma”
“Hao watoto wako unao hapa Kibaha?”
“Hao wakubwa wako Arusha. Wadogo zao ndio ninao hapa”
Zilipita dakika chache wakaingia polisiwaliofuatana na mkuu wa polisi wa wilaya ya Kibaha.
Walikwenda kule uani. Amour alipowaona aliinuka na kuwambia.
“Mosha huyu hapa mkamateni”
Mosha mwenyewe akashituka aliposikia agizo lile la kukamatwa.
“Nikamatwe kwa kosa gani?” akauliza kwa kutaharuki.
“Tunaamini utatusaidia mambo mengi” Amour akamwambia.
“Nyinyi watu msiniletee utani. Mmekuja hapa kuchunguza maisha yangu!” Mosha alisema alipoona anavamiwa na polisi.
Alijaribu kuleta ubishi. Nguvu ikatumika kumtoa nje ya gesti na kumpakia kwenye gari.
“Tunakwenda naye Dar moja kwa moja. Nitachukua polisi wako wawili. Tukishamfikisha watarudi” Amour alimwambia mkuu wa polisi wa Kibaha wakiwa nje ya gari.
“Mmegundua kuwa anahusika” Mkuu huyo akamuuliza Amour.
“Ametuambia kuwa hata Almasi mwenyewe atauawa kama walivyouawa watoto wake na ndipo nilipokupigia simu. Inaonekana ana mengi anayoyajua”
“Kama amesema hivyo ni lazima adhibitiwe ili aeleze ukweli”
“Kwa hiyo sisi tunarudi Dar. Tutawasilina”
“Sawa. Hakuna tatizo”
Walipeana mkono wa kuagana kisha Amour akafungua mlango wa gari na kujipakia. Mkuu wa polisi wa Kibaha aliingia kwenye gari jingine walilokuja nalo wakaondoka baada ya gari la Amour kutangulia kuondoka.
Walipofika makao ya polisi jijini Dar, polisi waliomsindikiza Mosha waliruhusiwa warudi Kibaha. Mosha alipelekwa katika chumba cha mahojiano.
“Sisi tuko katika uchunguzi wa mauaji ya watoto wa Almasi, umetutia wasiwasi sana ulipotuambia hata baba mtu mwenyewe atauawa” Amour alimwambia Mosha aliyekuwa amekaa kwenye kiti. Amour na Elias walikuwa wima.
“Mimi nilisema tu, kwani nikisema ndio atauawa kweli”
“Sisi tunajua kuuawa ni kuuawa tu, hatujui kuuawa kweli au kuuawa uongo. Hatutengezi sinema hapa” Amour aliwambia.
“Tulichogundua ni kuwa kuna mengi unayoyajua kuhusu kuuawa kwa watoto wa Almasi. Sasa tueleze”
“Hizo taarifa za kuuawa kwa watoto wake ninazisikia kwa watu tu. Mimi niko Kibaha naendelea na shughuli zangu. Yeye yuko Dar. Kinachoendelea huku siwezi kukijua”
“Ulijuaje kuwa Almasi atauawa?” Amour alimuuliza kwa hasira.
“Nilisema tu kwa sababu ya hasira. Yule mtu ni dhalimu. Utajiri wake wote ni wa kudhulumu”
“Sisi tumegundua wewe ndiye uliyekuwa ukiandaa mipango ya kuwaua watoto wa Almasi na kama ulivyoropoka mwenyewe hivi sasa una mpango wa kumuua Almasi mwenyewe”
Mosha licha ya kutaharuki alithubutu kutoa kicheko cha uongo.
“Yesu wangu, sijawahi na sijawahikuwaza mpango huo hata siku moja”
“Kama hujakuwa na mpango huo ni vipi umetuambia kuwa hata Almasi mwenyewe atauawa na umesisitiza kuwa kifo chake kitatokea mikononi mwa watu”
“Hayo maneno nilisema tu lakini si kweli”
“Usitudanganye. Hayo ndiyo yaliyomo katika mipango yako, ndio sababu uliyasema. Kama leo Almasi anauawa tutamkamata nani?”
Mosha akanywea.
“Basi mnisamehe, nilikosea kusema”
“Unajua kuna kuua kwa mdomo. Unaweza kumwambia mtu nitakuua na kesho akakutwa ameuawa kweli, basi muuaji utakuwa wewe”
“Mimi nilikuwa sijui. Nilisema kwa mzaha tu”
“Elias kamuweke ndani mpaka pale atakapokuwa tayari kutueleza anachokijua”
“Yesu wangu! Mnataka kuniweka ndani, kwani Almasi ameuawa?”
“Watoto wake wameuawa na umesema na yeye atauawa...”