KISIWA CHAMAUTI - 35
Muktasari:
- Tukasubiri. Harishi sasa alikuwa amenyamaza. Sauti yake haikusikika tena. Lakini ule moshi uliendelea kuonekana ndani ya ile chupa. Ulikuwa unabadilika rangi kila mara.
ILIPOISHIA
Tulitoka katika lile jumba. Wakati tunatoka Yasmin aligeuka juma akalitazama jumba hilo kwa mara ya mwisho. Sikujua alikuwa akiwaza nini. Baada ya kulitazama kwa sekunde chache aligeuka mbele na kuendelea na safari. “Lete begi nikusaidie” nikamwambia.
Nilimpokea begi. Lilikuwa zito kiasi. “Umetia nini?” nikamuuliza.
“Mna vitu vyangu” “Umeamua kuondoka navyo” “Nataka wazazi wangu wakavione” “Naamini watafurahi kukuona” “Na mimi nitafurahi kuwaona” “Tulifika mahali ilipoachwa helikopta. Rubani akatufundisha jinsi ya kujipakia kwenye helikopta. “Mnapotaka kupanda helikopta mnainama namna hii ili kukwepa mapangaboi na hata wakati wa kushuka mnainama” akatuambia huku akituonyesha jinsi ya kuinama. Yasmin ndiye aliyetakiwa ajipakie kwanza. Baada ya Yasmin kujipakia tulifuatia sisi..
SASA ENDELEA...
SOTE tulipokuwa ndani ya helikopta, helikopta ikapaa juu na kuanza safari. Nilimuona Yasmin akitazama chini kupitia kwenye vioo. Bila shaka macho yake yalikuwa yanaagana na kisiwa hicho alichokikaa kwa zaidi ya mwaka mmoja akiwa peke yake na asiye na matumaini ya kunusurika.
Kwa upande wangu nilikuwa siamini kuwa tunaondoka. Niliona kama niko kwenye ndoto.
Nasaha za Yasmin zilikuwa zimetimia siku ile. Nilikumbuka kuwa aliwahi kuniambia kuwa aliota ninamuua Harishi na kumuokoa yeye. Wakati huo niliona kama maneno ya mzaha lakini kweli yametimia. Bila kutegemea nimemzamisha Harishi chini ya bahari na hatukutegemea kama angeweza kutoka tena.
Pia nilikumbuka jinsi Yasmin alivyokuwa akinipa moyo kuwa tutaokoka. Na siku ile tukaokoka kweli.
Wakati helikopta ikizidi kuyoyoma na Yasminakiendelea kukiangalia kisiwa hicho, pengine akikumbuka enzi zake na Harishi, nilikumbuka jambo moja tena jambo muhimu.
Niliikumbuka ahadi yetu ya kumuoa Yasmin pindi tutakaponusurika na kurudi makwetu.
Sikudhani kuwa Yasmin alikuwa angali akiikumbuka ahadi ile japokuwa alinipa siku chache tu zilizopita
Niliamini kuwa kwa vile tulikuwa tumeshaokolewa mawazo ya Yasmin yanaweza kuwa yamebadilika. Kule aliniona kama mwenza wake kwa vile tulikuwa kwenye kifungo. Sote tulikuwa sawa. Lakini tukifika huko tunakokwenda yeye atakuwa binti wa rais mwenye hadhi na heshima, na mimi nitakuwa mvuvi nisiye na thamani yoyote. Sikudhni kama nitakuwa na maana tena kwake.
Helikopta sasa ilikuwa ikipita juu ya Bahari ya Hindi. Yasmin aliacha kutazama chini, sasa akawa anatazama mbele. Kwa vile viti vyetu vilikuwa vinapakana aligeuza uso akanitazama mimi. Nilidhani alitaka kuniambia kitu. Na mimi nikamtazama. Lakini hakuniambia kitu. Nikauona uso wake ukichanua tabasamu. Na mimi nikatabasamu. Baada ya hapo aliugeuza uso wake mbele.
Sikuweza kujua alikuwa akiwaza nini au aliwazia nini aliponitazama na kutabasamu lakini vyovyote ambavyo aliwaza alikuwa ameniwazia vizuri.
Wakati helikopta ikiendelea kupasua bahari niligeuka nyuma kuangalia kwenye vioo vilivyokuwa vimeizunguka helikopta nzima. Nilikuwa naangalia kile kisiwa tulichokuwa tumekiacha kwa mbali. Tuliendelea kukiacha kadiri helikopta ilivyozidi kusonga mbele.
Hatimaye tulikuwa katikati ya bahari. Hatukuona nchi tena. Baadaye tuliona mitumbwi ya wavuvi wakivua samaki. Baada ya muda ambao sikuweza kuukadiria tuliona nchi kwa mbali. Ilianza kutokea mbele yetu kama chuguu ya rangi ya kijani iliyochukua eneo kubwa. Kadiri tulivyozidi kwenda chuguu hiyo ilizidi kuonekana kubwa.
Sasa tuliweza kuona miti kwa mbali. Kijani tulichokuwa tunakiona ilikuwa miti iliyokuwa imeenea katika ardhi. Majumba ya ghorofa na barabara sasa vilionekana waziwazi. Nikajiambia kwamba tulikuwa tumekitokea kisiwa cha Unguja.
Muda si muda tukawa tumeivuka bahari. Sasa tulikuwa tunapita juu ya kisiwa cha kwetu baada ya kukitoka kile kisiwa cha kifo. Nilishukuru sana.
Tuliona vespa, bajaji na magari yanayokokotwa na punda yakipita chini yetu. Nikawa natabasamu peke yangu.
“Yasmin unakuona kwetu?” nikamwambia Yasmin.
“Ahaa ndio hapa!” Yasmin akaniuliza.
“Hapa ni Zanzibar. Kisiwa hiki kinaitwa Unguja”
“Uliniambia wewe unatoka Pemba”
“Pemba ni kwetu na Unguja pia kwetu. Yote ni Zanzibar moja”
Yasmin akatabasamu.
“Nimefurahi kufika kwenu. Nitawaona wazazi wako na ndugu zako” Wakati nazungumza na Yasmin helikopta ilikuwa inatua kwenye kiwanja cha ndege.
Tukaacha mazungumzo na kuchungulia kwenye madirisha. Tuliona jengo la kiwanja cha ndege kwa mbele. Pia tuliona ndege kadhaa zikiwa zimeegeshwa huku wafanyakazi wakienda huku na huko.
Helikopta ilipotua tulishuka
Kwa vile rubani alikuwa akifanya mawasiliano tangu tukiwa juu. Tulikuta maofisa wanne wa polisi wakitusubiri. Polisi tuliyekuwa naye aliwapa maelezo ya zoezi lililofanyika. Akawaeleza pia tulivyopatikana katika kile kisiwa.
Polisi hao walituchukua katika chumba kimoja wakaanza kuwahoji wale wazungu pamoja na mwendesha boti waliyekuwa naye. Baada ya wao kutoa maelezo lilikuja gari likawachukua. Tukaanza kuhojiwa mimi na Yasmin. Maelezo yetu ndio yaliyowaacha hoi maofisa hao.
“Unasema wewe ni bini wa rais wa Comoro na ulikumbwa na jinni aliyekupeleka katika hicho kisiwa mwaka mmoja uliopita?” Afisa mmoja akamuuliza Yasmin.
“Ndiyo”
Niliposema “Ndiyo” maofisa hao walitazamana kwa mshangao.
“Hebu tueleze ulivyofikishwa katika kisiwa hicho kutoka Comoro?” Afisa huyo akaendelea kumuuliza.
“Sijui. Ninachokumbuka ni kwamba nilikuwa kwenye sherehe ya harusi yangu nikaanguka na kupoteza fahamu. Nilipozinduka nikajikuta niko katika kile kisiwa ndani ya lile jumba nililokuwa ninaishi” Yasmin aliendelea kueleza.
“Ulijuaje kuwa ulikumbwa na jinni?’
“Wakati nazinduka nilimuona jinni mwenyewe. Aliniambia anaitwa Harishi na kwamba yeye ndiye aliyenikumba na kunileta pale”
“Alikuwa anataka nini kwako?”
“Alikuwa anataka niishi naye kama mke wake”
“Na ukawa unaishi naye?”
“Sikuwa na la kufanya zaidi ya kukubali”
“Ulikuwa unapata wapi chakula na mahitaji mengine?”
“Alikuwa ananiletea yeye chakula na nguo”
“Anavipata wapi?”
“Aliniambia kuwa anaiba kwenye maduka”
“Wapi?”
“Alikuwa anazunguka sehemu nyingi za Afrika Mashariki pamoja na Comoro”
Tumeambiwa kwamba kisiwa ulichokuwa unaishi wewe hakina watu isipokuwa nyumba tupu, ni kwanini?”
“Harishi alinieleza kuwa watu waliokuwa wakiishi katika kisiwa kile aliwaua yeye kwa kuwafyonza damu na kula bongo zao. chakula chake kilikuwa damu na ubongo”
Maafisa hao wakatazamana tena kwa mshangao.
“Chakula chake kilikuwa damu na ubongo wa binaadamu?” Afisa huyo akamuuliza tena Yasmin.
“Ndiyo” Yasmin alimjibu.
“Kwanini wewe hakukula?”
“Mimi alinichukulia kama mke wake”
“Na tuliambiwa kwamba kuna watu saba ambao chombo chao kiliharibika baharini na walifikakatika kile kisiwa, ni kina nani?”
“Mmojawapo ni huyu hapa” Yasmin alinionesha mimi na kuongeza.
“Walifikapale wakiwa watu saba wakauawa na Harishi akabaki yeye peke yake”
“Kwanini yeye hakuuawa?”
“Kuna kisa kirefu kimepita”
“Tunataka tukisikie”
Yasmin akawaeleza yaliyotokea hadi tukaweza kumzamisha Harishi chini ya bahari akiwa ndani ya chupa.
Baada ya Yasmin kuhojiwa nilihojiwa mimi. Nilijieleza kuwa nilikuwa Mzanzibari na kazi yangu ilikuwa uvuvi. Nikaeleza jinsi nilivyofika katika kisiwa kile na kumkuta Yasmin ndani ya lile jumba.
Nilipomaliza maelezo yangu simu zilipigwa sehemu mbalimbali. Haukupita muda mrefu maofisa usalama wa ikulu pamoja na waziri wa nchi ofisi ya raisi walifika kiwanja cha ndege.
Baada ya kupata maelezo yetu, waziri wan chi alimuuliza Yasmin kama kweli alikuwa binti wa rais wa Comoro.
Yasmin akasisitiza kuwa alikuwa binti wa rais huyo na akaomba aunganishwe naye kwenye simu.
Taarifa za Yasmin zilipofika ikulu, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi iliwasiliana na Wizara ya mambo ya nje ya Comoro.
Mpaka inafika saa kumi na moja jioni ndege ya serikali iliyotoka Comoro ikiwa imempakia kaka wa Yasmin ambaye alikuwa kanali wa jeshi pamoja na maofisa usalama wa ikulu ya Comoro ilitua kiwanja cha ndege cha Unguja.
Watu hao walipokewa na mkurugenzi wa usalama na kupelekwa kukutanishwa na Yasmin ambaye mpaka wakati huo nilikuwa pamoja naye.
Kaka wa Yasmin Kanali Umar Sharif Abdilatif alipomuona Yasmin alishituka.
Na Yasmin naye alishituka. Walitazamana kwa sekunde kadhaa kabla ya kukimbiliana na kukumbatiana kwa furaha na majonzi.
Maofisa usalama waliotoka ikulu ya Comoro ambao walikuwa wakimfahamu Yasmin nao walishangaa walipomuona kwani taarifa zilizokuwa nchini mwao zilionesha kuwa Yasmin alipotea katika mazingira ya kutatanisha wakati wa harusi yake zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Baada ya maofisa hao kumsalimia Yasmin walithibitisha kwamba alikuwa binti wa Rais Sharif Abdulatif aliyepotea nchini mwao katika mazingira ya kutatanisha.
Wakati huo Yasmin alikuwa akitiririkwa na machozi kwa kumuona kaka yake.
Yasmin aliwaeleza masahibu yaliyokuwa yamemtokea, maelezo ambayo yalimshitua kaka yake pamoja na maofisa hao.