KISIWA CHAMAUTI - 31
ILIPOISHIA
Shazume alikuwa kimya akitusikiliza. Bila shaka alikuwa anaona tunajidanganya kujifariji. Kwa mawazo yake, sisi tulikuwa ni wa kufa tu.
“Si unajua mzazi aliyekwishamkatia tamaa mwanawe, halafu anaambiwa amepatikana, atafurahije?” Yasmin akaniuliza..
SASA ENDELEA...
“ATAFURAHI sana”
Iliwezekana tulikuwa tulikuwa tunajidanganya kweli kama alivyowaza Shazume lakini tulifarijika. Saa zikapita.
Tulipomaliza kula Yasmin alileta stori tofauti tofauti kutuondoa katika mawazo mabaya. Tukawa tunazungumza.
Aliondoka jioni sana. Tukamsindikiza kwa pamoja hadi nusu ya njia, tukarudi. Tukakaa kwenye kile kisehemu chetu kusubiri usiku. Hatukujua nini kitatokea kati yetu usiku huo.
Usiku ule tulikesha macho kwa sababu ya hofu. Tulikuwa tumejilaza chini kila mmoja upande wake lakini hakukuwa na aliyelala usingizi. Mara kwa mara nilimuona Shazume akijigeuza kila upande.
Ilikuwa kati kati ya usiku Shazume aliposhika mguu wangu. Sikujua kama alikuwa anataka kuniamsha au alitaka kujua nilikuwa macho lakini aliponishika nilishituka nikarusha mguu wangu.
“Nini?” nikamuuliza nikiizuia sauti yangu isisikike sana.
“Nimebanwa na haja ndogo” akaniambia.
“Sasa?” nikamuuliza.
“Tunaweza kutoka nikajisaidie”
“Haya tutoke” nikamwambia.
Shazume akainuka na mimi nikainuka. Akatangulia kutoka kwenye mlango. Kulikuwa giza sana. Hatukuweza kuona kwa mbali.
“Twende nje au uani?” Shazume akaniuliza.
“Naona tutoke uani” nikamjibu.
Shazume akaelekea upande wa uani. Mimi nilikuwa nikimfuata nyuma. Alifungua mlango akachungulia uani. Mwezi ulikuwa unaangaza, ua ulikuwa mweupe. Baada ya kuchungulia kwa tahadhari Shazume alivuka kizingiti cha mlango akatoka uani na mimi nikatoka.
Yeye alikwenda upande wake na mimi nilikwenda upande wangu tukachutama na kujisaidia. Mimi sikuwa na haja ndogo lakini baada ya mwenzangu kuniambiana mimi nikaisikia.
Tulipomaliza haja zetu tulirudi ndani tukajilaza tena. Safari hii tulipojilaza tu usingizi ulitupitia tukalala.
Wakati nipo usingizini niliota Harishi anatufukuza baada ya kutufuma tukiwa na Yasmin kwenye lile jumba lake. Tukaingia katika chumba kimoja kujificha chini ya mvungu wa kitanda. Muda si muda Harishi akafungua mlango na kuingia mle chumbani kututafuta.
Akaona mguu wa Shazume umetokeza chini ya mvungu. Akaushika na kuuvuta. Shazume akawa anapiga kelele kuniita.
Kelele hizo ndizo zilizoniamsha. Nikaamka na kuangaza macho. Nikasikia Shazume akiendelea kupiga kelele kuniita lakini sauti yake ilitokea kwa juu, sio pale chini tulipolala. Nikashituka sana kwa kujua kuwa haikuwa ndoto.
Nikatazama juu. Kwanza niliona kanzu nyeupe halafu nikaona upanga uking’aa. Nilipoona hivyo nilijisogeza zaidi ndani ya makorokoro na kuendelea kuchungulia.
Nilimuona Shazume ameinuliwa juu juu na Harishi. Nikajiambia kumbe ile ndoto ilikuwa ni kweli. Shazume alitolewa mle chumbani. Sikuweza kujua Harishi aliwasili muda gani na kumkamata Shazume.
Bila shaka kilichokuwa kimeninusuru mimi, ni kuwa nililala nyuma ya mlango. Harishi alipoingia alimuona Shazume na kumkamata yeye. Ile ndoto niliyoota ilikuwa ya kweli. Harishi alikuwa ametuingilia!
Jitihada zetu za kujaribu kumkwepa zilikuwa za bure kwani Harishi alikuwa akitugundua kila tulipokwenda kujificha na sababu ni kuwa alikuwa akifuata harufu zetu kama vile m’bwa.
Harishi alipomtoa Shazume ukumbini, nilimsikia Shazume akipiga ukulele mmoja tu “Nakufa!.” Halafu sikusikia kitu tena.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio na nilikuwa nikihema kwa nguvu kama niliyekuwa nafukuzwa. Tukio hilo lilikuwa la ghafla sana kiasi kwamba nililazimika kujiuliza, kama bado nilikuwa kwenye ile ndoto au kilichokuwa kinatokea kilikuwa kweli.
Hofu yangu sasa ilikuwa kwangu. Nilijiua Harishi akimaliza kumuua Shazume ataniingilia na mimi kwani alipoingia humo chumbani alituona tukiwa wawili.
Wazo hilo likanifanya nizidi kujisogeza kwenye makorokoro ili Harishi akiingia tena asinione. Lakini muda ulipita. Sikumuona tena Harishi.
Nikaendelea kukaa hapo hapo hadi nikaona kunakucha. Nikahisi kwa muda ule Harishi atakuwa ameshaondoka. Nikajiburuza kujitoa kwenye yale makorokoro nilikojiingiza.
Nilinyata hadi kwenye mlango nikaufungua na kuchungulia ukumbini. Nilichungulia upande wa mbele na upande wa uani. Niliiona maiti ya Shazume imelala chini kando ya mlango wa chumba tulichokuwemo. Harishi mwenyewe hakuwepo.
Nikatoka nje na kuangalia kila upande. Sikuona kitu. Kando ya ile nyumba palikuwa na mti. Nikapata wazo kuwa nipande juu ya ule mti kujificha. Nikaenda kwenye mti huo nikaupanda na kukaa kwenye tawi mahali ambapo nisingeweza kuonekana. Wakati nipo juu ya ule mti nilimuona Yasmin kwa mbali akija. Nikajiambia tuliobaki katika kisiwa kile tulikuwa watu wawili tu, mimi na Yasmin.
Sikupenda kujisifu kuwa nilikuwa nina bahati kwa sababu nimenusurika. Nilijua kuwa wakati wangu ulikuwa haujafika. Pengine niliandikiwa niwe wa mwisho kufa.
Historia ya kisiwa hicho tangu tulipofika kila siku alikufa mtu. Leo nimeishuhudia maiti ya Shazume, huenda kesho Yasmin ataishuhudia maiti yangu.
Yasmin alipofika pale nilimuacha aingie mle ndani. Mara moja nikamuona ametoka akiwa amechanganyikiwa. Bila shaka alikuwa ameshitushwa na maiti ya Shazume. Kile kitendo cha kutoniona mimi inawezekana kilimpa hisia kuwa na mimi nilikuwa nimeuawa kama Shazume. Tatizo ni kuwa mwili wangu hakuuona. Bila shaka alitoka nje kuutafuta mwili wangu.
Alisimama mbele ya ile nyumba akaangalia kila upande kisha akarudi tena mle ndani. Mimi nikashuka kwenye ule mti.
Yasmin alipotoka tena akanikuta nimesimama mbele ya mlango. Akashituka na kuniuliza. “Ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nimepanda juu ya huu mti” nikamjibu.
Akaja kunikumbatia kifuani kwangu. Kumbe alikuwa analia. Nilipoona analia na mimi nikaanza kulia. Kama Yasmin alikuwa anaona uchungu jinsi tulivyokuwa tunauliwa na Harishi, mimi niliona uchungu nilipowaza nitakavyouliwa na Harishi hapo kesho.
“Buriani Yasmin, ndio tunaagana. Kesho hatutakuwa pamoja tena. Shazume ametutangulia leo” nikamwambia Yasmin.
Yasmin akajifuta machozi yake na kunitazama.
“Wewe hutaniacha, kama ni kufa tutakufa sote. Mwili wangu utalala juu ya mwili wako” Yasmin akaniambia kwa sauti nzito lakini ya kijasiri.
Akaongeza. “Ili uamini kuwa wewe utakufa na mimi turudi kule kule kwenye lile jumba,hatuna sababu yoyote ya kujificha. Akija Harishi nitamwambia atuue sote, Anitangulize mimi kisha wewe”
“Twende!” nikamwambia Yasmin bila kusita.
Yasmin akanishika mkono tukatembea kuelekea katika lile jumba. Hatukuzungumza kitu tena mpaka tulipofika katika jumba hilo Yasmin aliniuliza.
“Utakunywa uji?”
“Sitakunywa” nikamjibu kwa mkato
“Kwanini?”
“Roho yangu imefadhaika sana”
“Hata roho yangu imefadhaika lakini kama wanipenda tunywe kidogo” Ili kumridhisha Yasmin nilimkubalia. Yasmin aliniacha ukumbini akaenda jikoni. Baaada ya muda kidogo alikuja na vikombe viwili vilivyojaa uji wa ngano uliotiwa asali.
Alinipa kikombe kimoja kisha aliketi nami.
“Yasmin kweli tumeshindwa kuondoka kwenye kisiwa hiki cha mauti” nikamuuliza Yasmin
“Tutaondokaje wakati tumezungukwa na bahari na hatuna chombo!”
“Nashangaa kwamba hakuna wavuvi wanaokuja katika kisiwa hiki!”
“Hiki kisiwa kiko mbali na pia kinajulikana. Hakuna wavuvi wanaoweza kufika hapa”
“Chombo chetu kilipotuharibikia tulipokiona kisiwa hiki tulidhani tumeokoka kumbe tumekuja kuangamia”
“Hata kama msingekiona hiki kisiwa pia mngeangamia. Mngekula nini? Mngekufa kwa njaa”
“Mimi naona bora kufa kwa njaa kwa sababu njaa itakuwa imekulevya, hutajijua. Kuliko kusubiri….” sikumalizia sentensi yangu. Niliona nilikuwa najikumbusha kifo kibaya cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo1.
Siku zote tulizokaa hapa kisiwani niliweza kujikaza na kuondoa hofu licha ya wenzangu kuendelea kuuawa lakini kwa siku ile ambayo nilibakimimi na Yasmin peke yetu, sikuweza kuzuia hofu yangu.
Mawazo ya kifo cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo yalikuwa yametawala akili yangu.
“Harishi ni kiumbe na sisi ni viumbe. Huwezi kujua Mungu amepanga nini” Yasmin akaniambia.
“Namuamini Mungu na simkatii tamaa”
“Hapo umezungumza kitu cha maana sana. Haifai kukata tama. Nimeshakwambia kama ni kufa leo tutakufa sote. Na mimi ndio nitakufa kwanza”
“Unataka tuendelee kukaa humu hadi usiku”
“Ndiyo. Unafikiri utakwenda wapi?”
“Sioni pa kwenda”
“Basi tukae tu humu”
“Harishi akija atukute pamoja?”
“Ndiyo”
“Aniue mbele yako!”
“Hapana. Ataniua mimi kwanza”
“Mimi sipendi nikusababishie kifo, niache nife mwenyewe”
“Na mimi sitapenda nikusababishie kifo”
“Wewe hutanisababishia kifo, ni Harishi”
“Sikiliza kaka yangu. Sisi tukae hapa hadi usiku. Litakalotokea lolote na litokee lakini kama ni kufa nitatangulia mimi”
Nilimuangalia tu Yasmin, sikumjibu kitu tena. Nikaendelea kunywa uji huku nikiwaza kama ni kweli alikuwa amejitolea nafsi yake kwa ajili yangu.
Maneno yake yalionesha alichokuwa akisema kilikuwa na udhati.
Hata hivyo niliwaza kuwa msimamo wa Yasmin haukuwa na msaada wowote kwangu zaidi ya kuonesha upendo. Ulikuwa msimamo wa kukata tamaa na haukuwa na maana.