Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHAMAUTI - 25

KISIWA 25 Pict

ILIPOISHIA

Ile shuka ya mwenzangu aliyokuwa akiiburuza ilitokeza nje ya mvungu wa kitanda. Harishi akaiona!

Tukaona mkono wake ukishika ncha ya shuka na kuivuta. Jamaa akaiachia. Shuka yote ikavutwa na kuchukuliwa na Harishi.

“Hizi ni shuka zangu ninazoziiba kwa Wahindi. Imewekwa na nani huku mvunguni?’ akajiuliza mwenyewe kisha akaitupa chini.

Tukaona miguu inageuka na kutoka. Alipotoka tulishukuru. Mimi nilitambaa hadi kwenye mlango, nikaufungua na kumchungulia.

SASA ENDELEA...


Nilimuona akiinama na kuushika mguu wa mwenzetu aliyemuua, akamburuza kuelekea kwenye mlango wa kutokea.

Mwenzangu alikuwa amebaki mvunguni akinitazama. Nikaufunga mlango taratibu, kisha nikarudi mle mvunguni.

“Mwenzetu ameuawa,” nikamwambia mwenzangu. “Harishi amemburuza na kutoka naye.”

“Alimuona wapi?”

“Mara ya kwanza aliingia ndani, wewe ulikuwa umelala. Akamsomba pale kwenye godoro na kutoka naye kwenda kumuua. Ndiyo pale ulipoamka.”

“Kumbe Yasmin alitaka tufe alipotuambia tulale?”

“Ni makosa yetu sisi. Yasmin alituambia tutoke alfajiri, sisi tumelala hadi sasa kumekucha.”

“Lakini ni kweli.”

Wakati tunazungumza kwenye mvungu, Yasmin akaingia.

Tulipoona miguu yake, tulitoka mvunguni.

“Jamani, niliwambia nini?” akatuuliza kwa kutaharuki.

Hakukuwa na aliyemjibu. Sote tulikuwa tumeshikwa na fadhaa.

“Si niliwambia mtoke alfajiri, mmelala hadi sasa wakati niliwambia kuwa Harishi atakuja leo?”

“Ni kweli ulituambia,” nikamkubalia.

“Sasa mbona hamkutoka alfajiri?”

“Tumepitiwa.”

“Mtanilaumu mimi bure, jamani!”

“Hatutakulaumu hata kidogo. Umetufanyia wema sana.”

“Harishi alikuja mapema sana, akaniambia anasikia harufu ya kimtuntu. Nikamwambia mtu ni mimi. Akaniambia, ‘Hebu ngoja.’ Akatoka kuja kuwatafuta.”

“Siku hizi atakuwa anakuja kila siku kwa sababu ameona anapata mlo anaoutaka. Ni lazima mjihadhari.”

“Mimi naona tuondoke tu humu ndani,” mwenzangu akasema kwa woga.

“Lakini amekwisha kwenda zake. Kwa leo hatarudi tena,” Yasmin akatuambia.

“Itabidi tuondoke tu,” mwenzangu alizidi kusisitiza.

“Kwani wenzenu wengine wako wapi?”

“Bado wamelala hadi sasa?” Yasmin akauliza kwa mshangao.

“Naona bado wamelala,” nikamjibu.

“Kumbe nyinyi hamuwezi kuamka alfajiri?”

“Tatizo ni kuwa usingizi wenyewe unakuja wakati wa alfajiri,” nikamwambia Yasmin.

“Basi ni balaa. Sasa itabidi usiku mwende mkalale sehemu nyingine, mjaribu bahati yenu.”

“Tutafanya hivyo.”

“Kuna nyumba nyingi hazina watu. Mnaweza kutafuta nyumba nzuri yenye vitanda, mfanye makazi yenu. Hapa mtakuwa mnakuja mchana tu, muda ambao nitawambia mimi.”

“Tumekuelewa, ngoja niwaamshe hawa mabwana.”

Tukatoka pamoja mle chumbani. Tulipotoka tukawaona wenzetu nao wametoka.

“Hivi ndivyo mnaamka, jamani?” Yasmin akawauliza.

“Dada yetu, si unajua usingizi hautabiriki?” Mtu mmoja akamjibu.

“Hamkumbuki jana niliwambiaje? Si niliwambia muamke alfajiri muondoke?” Yasmin akawauliza.

“Ni kweli ulituambia, lakini ndiyo tumepitiwa.”

“Shakiri ameuliwa leo na Harishi!” nikawaambia.

“Unasema kweli?” wakaniuliza kwa pamoja kwa mshangao.

“Ni kwa sababu ya kuchelewa kuamka. Sisi tumeponea chupuchupu baada ya kuingia mvunguni mwa kitanda.”

“Basi tutakwisha!”

“Yasmin ametupa wazo. Badala ya kulala hapa, tutafute nyumba nyingine tuweke makazi yetu. Hapa tutakuwa tunakuja kula chakula mchana, katika muda atakaotuambia Yasmin.”

“Hivyo itakuwa vizuri,” mmoja wa wenzetu hao akasema.

“Sasa mjitayarishe, ninaenda kuwaandalia chai,” Yasmin akatuambia.

Wakati Yasmin anakwenda jikoni, wenzetu wawili waliokuwa wamelala chumba cha pili, walivyokuwa hadi mwenzetu akauliwa, tukawaeleza.

Kwa kweli walipata hofu.

“Sasa tukishakunywa chai tutoke tukatafute hiyo nyumba,” nikawambia wenzangu.

Ilipofika saa nne, tayari tulikuwa tumeoga na kunywa chai. Tukamwambia Yasmin tunataka kwenda kutafuta nyumba ya kukaa kwa maana tayari tulishakuwa wakazi wa kisiwa kile na hatukuwa na matumaini ya kuondoka.

“Kwani mpaka mwende nyote?” Yasmin akaniuliza.

“Unataka twende wangapi?” nikamuuliza.

“Mnaweza kwenda wawili, wawili wabaki.”

Mimi na wenzangu tukatazamana, lakini sote tulionekana kutoliafiki wazo la Yasmin.

“Acha tu twende sote,” nikamwambia Yasmin.

“Basi ngoja niwasindikize, msiniache peke yangu.”

“Tukizunguka na wewe itakuwa vizuri,” nikamwambia.

“Kwanini?”

“Kwa sababu wewe ndiye mwenyeji wetu, utaweza kutuongoza vizuri.”

“Haya basi, twendeni.”

Tukatoka na Yasmin. Yasmin alikuwa akikijua vyema kisiwa hicho. Alituzungusha mitaa mbalimbali tukiangalia nyumba. Mwisho alitupeleka katika nyumba moja ambayo alituambia ilikuwa ya mtu mmoja tajiri wa kisiwa kile ambaye naye aliuawa na Harishi.

Ilikuwa nyumba nzuri, lakini ilikuwa imechakaa kwa vile haikuwa ikiishi watu. Tulipoingia ndani tulikuta mavumbi yalikuwa yameenea nyumba nzima.

Tukaanza kazi ya kuisafisha nyumba. Yasmin alitusaidia kufanya usafi. Ilikuwa kazi iliyotuchukua saa kadhaa.

Tulipomaliza, tulichota maji kwenye kisima, tukaoga, kisha tukapumzika. Hapo ndipo tulipoanza kugawana vyumba.

Nyumba yenyewe ilikuwa na vyumba vinne na sisi wenyewe tulikuwa wanne. Kila mmoja alijichagulia chumba chake alichokipenda. Tulifungua makabati, tukatoa mashuka na kutandika vitanda tulivyovikuta humo ndani.

Wakati ninatandika kitanda, Yasmin aliniambia nimpe shuka atandike yeye. Nikampa.

“Natamani sana ningekuwa hapa pamoja na nyinyi,” Yasmin akaniambia wakati anatandika.

“Ukiwa hapa utatuponza sote.”

“Ninasema tu, lakini najua haitawezekana. Unajua katika nyinyi nyote nimekupenda wewe zaidi. Ninatamani ungekuwa mume wangu.”

“Hata mimi natamani ungekuwa mke wangu, lakini ndiyo tupo jela. Uhai wetu unahisabika.”

“Ni kweli. Tusikumbushie hayo. Tuswali tuombe nusura itufikie.”

“Wewe unaswali?” nikamuuliza Yasmin.

“Ninaswali, lakini kwa siri sana. Harishi hataki niswali. Swala ndiyo inayonipa matumaini ya kuishi.”

“Umenikumbusha jambo zuri sana na sisi tutaanza kuswali.”

“Kila mara ninaota kuna mtu atakuja kumwangamiza Harishi na mtu huyo atakuwa mume wangu.”

“Mtu huyo atatokea wapi?”

“Sijui.”

“Mtu huyo atastahili kuwa mume wako kwa sababu atakuwa jabari sana atakayeweza kupambana na jini na kumwangamiza.”

“Usisahau kwamba majini yameumbwa kama sisi!”

“Ni kweli, Yasmin, sema tu yamepewa uwezo wa kutudhuru.”

Yasmin alikuwa amemaliza kutandika, akakaa kitandani na kuniita.

“Njoo tukae kidogo.”

Nikaenda kuketi naye.

“Kwa kweli, wewe ni mzuri na unapendeza sana. Sina la kusema,” nilimwambia Yasmin ambaye alitabasamu. Alipotabasamu, mashavu yake yaliunda vidimbwi.

Mara moja akainuka pale kwenye kitanda.

“Sasa ninaenda kupika. Tunaweza kwenda sote?”

“Twende na wenzetu?” nikamuuliza.

“Hapana. Wao waache hapa hapa. Twende mimi na wewe.”

“Una hakika kuwa nitakuwa salama?”

“Harishi hatakuja leo. Ameshakuja asubuhi, ni mpaka kesho.”

“Ngoja niwaage wenzangu.”

Tukatoka ukumbini. Wenzangu walikuwa wameketi wakizungumza. Nikawambia kuwa namsindikiza Yasmin.

“Ninakwenda kupika, nitampa chakula awaletee,” Yasmin akawambia.

“Yaani utasubiri chakula huko huko?” Mmoja akaniuliza, lakini uso wake haukuonesha furaha.

“Ndiyo, atakisubiri,” Yasmin akamjibu.

Masudi akawatazama wenzake kabla ya kuniambia.

“Sawa. Sisi tutasubiri.”

Jina lake lilikuwa Masudi. Katika sisi watu wanne tuliobaki, yeye alikuwa ndiye mkubwa kwetu kiumri.

Wakati mimi na Yasmin tunatoka kwenye ile nyumba tukirudi nyumbani kwa Yasmin, Yasmin aliniambia, “Yule kaka uliyezungumza naye anaitwa nani?”

“Anaitwa Masudi.”

“Naona kama hakufurahi ulivyomwambia tunatoka mimi na wewe.”

“Inawezekana, ni binadamu. Labda ameona tumewabagua.”

“Mbona wengine hawakusema kitu?”

“Kila mtu ana mawazo yake. Yule amezoea kutuamrisha kwa sababu kwenye kundi letu yeye ndiye mkubwa kiumri na amekuwa kama kiongozi wetu.”

“Kwa hiyo alitaka anisindikize yeye?”

Yasmin aliposema hivyo nilicheka, na yeye akacheka.

“Unafikiri nakutania?” aliponiuliza hivyo, alitaja jina langu.

“Hunitanii, unaniambia ukweli. Najua Masudi hakufurahi,” nikamwambia.

Pakapita kimya kifupi kabla ya Yasmin kuniambia.

“Kisiwa chote hiki kilikuwa kina watu.”

“Wewe uliwakuta hao watu?” nikamuuliza.

“Wakati Harishi ananileta hapa, alikuwa ameshamaliza watu wote. Wengine walihama wenyewe kukimbia kifo.”

“Na kama leo anakuja na kutukuta hivi, itakuwaje?”

“Atakukamata wewe. Atakufyonza damu na ndiyo ataniuliza wewe ni nani na ulifuata nini hapa.”

“Ina maana wewe hatakuadhibu?”

“Ananitisha tu pale ninapomuudhi, lakini kama atanikuta na mwanaume, nadhani ataniadhibu.”