Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 8

KISIWA 08 Pict

ILIPOISHIA

Nikaipokea.

“Shikamoo mkuu” nikamwamkia.

“Marahaba. Mbona hujaonekana tangu jana”

Nikamueleza kile kilichotokea.

“Kwani wewe uko wapi?”

“Sipendi niseme niko wapi lakini nipo hapa Dar”

“Hizo taarifa tumeshazipata, sasa nataka uje hapa ofisini”

“Sitaweza kuja. Bado nafikiria nifanye nini”

SASA ENDELEA...



“Sikiliza Masha. Njoo hapa ofisini tushauriane. Bado utakuwa na hiyari ya kwenda polisi au kutokwenda”

“Mkuu naomba uniache tu…”

“Utakuwa kama umekusudia kufanya hilo tukio. Sisi tuna maswali ambayo tunajiuliza ambayo yanaweza kukusaidia wewe. Najua umetaharuki lakini ni vizuri uje hapa ofisini”

“Sawa. Nitakuja”

Mhariri akakata simu. Sikuwa na nia kwenda tena ofisini. Nilimjibu kuwa nitakwenda ili kukatisha yale mazungumzo tu. Nilipokata simu niliamua nivae nguo niende nyumbani, nichukue vitu vyangu muhimu kisha nijue pa kwenda. Nilihisi huenda polisi  walikuwa hawajafika nyumbani.

Nilitoa pikipiki nikaanza safari ya kuelekea mtaa ninaoishi. Wakati naendesha, picha ya yule msichana ilinijia mbele ya macho yangu. Nilikuwa kama ninayemuona akinimiminia  bia kwenye bilauli na kuniambia ‘karibu’ huku uso wake ukiwa na tabasamu.

Picha iliendelea kunijia  wakati akinitajia jina lake. Mara nyingi msichana wa kimjini unapoanza kujuana naye hupenda kuficha jina lake na  kutaja jina la uongo. Lakini yeye alinitajia jina lake la kweli aliponiambia anaitwa Edda. Alikuwa msichana mpole sana  na mwenye kuthamini mahusiano.

Wakati ile picha ikiendelea kunijia, nilijihisi nilikuwa mwenye hatia kuitoa roho ya msichana yule kwa sababu ya ulevi. Niliamini ni kwa sababu ya ulevi kwakuwa alishanirusu nifike kwake kwa maongezi zaidi.

Baada ya dakika chache tu nikaingia katika mtaa niliokuwa ninaishi. Tangu nikiwa mbali niliona gari limesimama mbele ya nyumba niliyokuwa nimepanga chumba. Nilipolikazia  macho gari hilo nikagundua kuwa lilikuwa gari la polisi.

Nikasimamisha pikipiki haraka. Niliona polisi wakiingia na  kutoka mle ndani. Nikageuza pikipiki na kurudi. Nilijua  kuwa wale polisi walikuwa wamenifuata mimi wakijua nitakuwa  nyumbani kwangu.

Kama ningerudi nyumbani mapema polisi hao wangenikuta na kunikamata.

Nikiwa  nimeikoleza pikipiki nikirudi, nikaona simu yangu inaita. Kwanza nilitaka nihakikishe kuwa niko mbali na ule mtaa ninaoishi,  ndipo  nisimamishe pikipiki na kuona ni nani aliyekuwa ananipigia.

Niliporidhika kuwa mahali nilipofika nilikuwa salama nikasimamisha pikipiki na kutoa simu.

Simu ilikuwa imeacha kuita lakini niliona namba ya Edda, yule msichana niliyemuua kule hoteli!

Nikashituka na kujiuliza, huyu msichana ni yule yule au ni mwingine?

Kwa kutaka kujua nikaipiga ile namba. Ikapokelewa. Sikusema kitu. Nikasikia  sauti ya mwanamke ikisema.

“Vipi Masha, habari ya tangu jana?”

Sikuwa na shaka yoyote kuwa ilikuwa sauti ya Edda. Nikajiuliza nilikuwa naota au niko katika maisha halisi?

Nikajiambia kama naota au niko katika  maisha halisi nitajua.

“Nzuri. Habari yako?” nikamsalimia.

“Nzuri. Leo sijafika kazini. Nina mapumziko”

“Nazungumza na Edda  au…?”

“Ndiyo, mimi Edda”

“Wewe ni Edda?”

“Ndiyo. Si nilikupa namba yangu jana kule hoteli”

“Ndiyo ulinipa. Lakini sikumbuki tulivyoachana”

“Mimi nilimaliza zamu yangu nikaondoka, nikakuacha unaendelea kunywa”

“Nilikuwa nikihudumiwa na nani?”

“Na mhudumu mwingine msichana mwenzangu”

Nikajiuliza kimoyo moyo huyo mwenzake ndiye niliyemuua kule  chumbani?

“Hakuna taarifa zozote ulizopata kutoka  huko Hoteli?”

“Kuhusu nini?”

“Kuhusu mimi”

“Sijapata taarifa yoyote, kwani hukuonana  na Bosi?”

“Sikuonana naye”

“Yule mzee atakusumbua, yuko bize sana”

“Wewe uko wapi muda huu?”

“Nilikuwa nimekwenda saluni. Hivi sasa ninarudi, niko kwenye kibajaj”

“Unarudi wapi?”

“Nyumbani”

“Mimi nakuja huko huko”

“Njoo, utanikuta”

“Sawa”

Nikakata simu. Nilikuwa nimezima pikipiki, nikaiwasha haraka na kuondoka. Nilitaka kwenda nyumbani kwa msichana huyo ili nithibitishe kwamba ndiye  yeye Edda kweli.

Hapo sikufikiria tena habari ya polisi. Nikaelekea katika mtaa huo. Nilipokata kona tu kuingia katika  mtaa huo, nyumba aliyonielekeza Edda niliiona. Ilikuwa ya pili mkono wa kushoto.

Vile natokea tu nikaona bajaj inasimama mbele ya nyumba hiyo. Nikamuona  msichana anashuka kwenye bajaj hiyo na kuagana na dereva wa bajaj.

Nilishituka na kushangaa nilipogundua alikuwa Edda! Nikataka nimuwahi kabla hajaingia ndani. Nilipoifikia nyumba hiyo Edda  alikuwa amefunguliwa mlango.

Nikafunga breki barazani na kumuita.

“Edda…!”

Edda akageuka na kunitazama.

“Ah… Masha!” akasema huku akitabasamu kisha akaongeza.

“Inaonekana ulikuwa karibu”

“Wakati nazungumza na wewe nilikuwa nyumbani kwangu. Mimi pia naishi hapa Kinondoni”

Wakati namwambia hivyo nilikuwa najiuliza, huyu msichana si nimemuua, mbona yuko hai?

“Ulivyoniambia ninakuja sikuamini. Nilijua unanitania tu”  Msichana akaniambia.

Sasa niligundua kuwa niliyemuua alikuwa msichana mwingine.

“Kwanini nikutanie wakati tumekubaliana?”

“Basi karibu ndani”

Nikaiegesha vyema pikipiki kisha nikaizima”

Msichana alitangulia kuingia ndani. Nikamfuata.

Chumba chake kilikuwa cha kwanza cha mkono wa kulia.

Alitoa funguo akafungua mlango wa  chumba hicho kisha akaingia ndani. Nilibaki mbele ya mlango wa chumba hicho mpaka alipotoa kichwa na kuniambia.

“Karibu ndani”

Nikaingia.

Kilikuwa chumba kidogo kama vilivyo vyumba vya nyumba nyingi za Dar es Salaam zilizojengwa kibiashara. Kilienea kitanda cha futi sita kwa sita. Kabati dogo la nguo lililokuwa na kioo cha kujitazamia na sofa moja kubwa.

“Karibu ukae” akaniambia.

Nikakaa kwenye lile sofa

Alifunua pazia la dirisha lililokuwa upande wa nje. Mwanga ukaingia ndani. Baada ya hapo alikwenda kuketi kwenye kitanda.

“Nakuona umependeza!” nikamwambia huku nikimtazama  kichwani. Nywele zake zilikuwa zimewekewa dawa na kuwekwa katika mtindo maalum.

Msichana akaminya midomo yake kutabasamu. Alipofanya hivyo mashavu yake yaliunda vishimo na kuufanya uso wake uonekane wa kupendeza zaidi.

“Asante” akaniambia na  kuongeza.

“Si unajua  leo nina mapumziko. Naweza kutoka”

“Unaweza kutoka uende wapi? Halafu mgeni wako umuachie  nani?” nikamuuliza. Nusu ulikuwa mzaha, nusu ilikuwa kweli.

“Kwani utashinda hapa kwangu?”

“Naweza, kwani kuna tatizo?”

“Hakuna  tatizo, ni wewe tu”

“Nitakuwa nimekuvunjia  safari zako?”

“Hapana. Kama utakuwa hapa sitatoka”

Ili kumpa moyo na aone kuwa nitakuwa naye kama nilivyomwambia nilitia mkono mfukoni mwangu nikatoa pochi  yangu. Niliifungua na kutoa noti  mbili nyekundu. Nina  maana noti za elfu kumi kumi.  Nikampa.

“Mgeni njoo mwenyeji apone. Nenda sokoni ufanye maandalizi ya msosi wa mchana” nikamwambia.

Edda alizipokea zile pesa huku akicheka.

“Unasemaje, mgeni njoo mwenyeji apone? Sasa maana yake nini?”

“Maana yangu ni kuwa leo hutatumia  pesa yako”

“Kweli?”

“Nimekuja kikamilifu baada ya yale mazungumzo yetu ya jana”

“Tena kama umegundua, leo nina mapumziko”

“Ndio hapo sasa, ukae  tuzungumze”

“Sasa subiri basi niende  sokoni nifanye  maandalizi ya chakula”

“Sawa. Wewe nenda. Mimi nipo”

“Sijui  ungependa chakula gani mgeni wangu?”

“Chochote tu unachopenda wewe”

“Mimi napenda ndizi”

“Sawa”

“Ninunue ndizi na nini,  nyama au samaki?”

“Samaki”

“Subiri niende mara moja”

Edda alipotoka nikaanza kuwaza. Nilijiuliza ni msichana gani niliyemuua? Msichana ambaye nilimuona pale chini amekufa  alikuwa ni Edda na  ndiye aliyekuwa akinihuduumia pale hoteli.

Isitoshe nilikiona kitambulisho chake kilichokuwa kimeanguka. Alikuwa ni Edda  na  hakuwa msichanna  mwingine.

Sasa kama Edda yuko hai, ule  mwili niliouona pale chini, ulikuwa wa nani?

Nikakumbuka  kwamba Edda aliniambia aliniacha nikihudumiwa  na msichana mwingine. Nikajiuliza huyo  msichana mwingine  ndiye  niliyemuua?

Niliendelea kujiuliza, kama niliyemuua alikuwa msichana mwingine,  mbona taarifa nilizoziona  kwenye blogy zinaonesha  kuwa aliyeuawa alikuwa Edda!

Hapo nilishindwa kupata jibu. Nikajiambia  ni vizuri Edda atakaporudi niendelee kumdadisi. Huenda  nikagundua yule msichanna alikuwa nani.

Lakini  pia  nilijiuliza, kwanini Edda  hakuwa na habari ya tukio lilotokea hapo hoteli ambako anafanya kazi?  Hata kama si yeye  niliyemuua, kwanini asijue kilichotokea?