KISIWA CHA MAUTI -6
Muktasari:
- Hapo kidogo niliona sura ya yule msichana ikichuja kama ambaye alihamaki au alipata fadhaa. Akalirudisha lile burungutu ndani ya mkoba wake kisha akainuka. “Ngoja nikamfahamishe mwenyewe” akaniambia na kuondoka.
KWA KIFUPI
“Siwezi kuona ni ndogo kwa sababu sijahitaji pesa. Mimi nimekuja hapa kwa ahadi yetu ya jana kwamba angenipa ufafanuzi wa madai niliyomuandikia”
Hapo kidogo niliona sura ya yule msichana ikichuja kama ambaye alihamaki au alipata fadhaa. Akalirudisha lile burungutu ndani ya mkoba wake kisha akainuka. “Ngoja nikamfahamishe mwenyewe” akaniambia na kuondoka.
Nikawa namtazama kwa nyuma. Kwa asilimia mia moja niliamini kuwa yale madai ya Sofia na Kabwe yalikuwa na ukweli ambao Makita hakutaka utoke kwenye vyombo vya habari..
SASA ENDELEA...
SASA alitaka kunizima kwa kutumia pesa. Bahati mbaya mimi nilikuwa na uchu wa habari, sikuwa na uchu wa pesa. Nilikuwa masikini. Mshahara wangu ulikuwa haufiki hata shilingi milioni moja kwa mwezi. Lakini suala la kutoa au kupokea rushwa lilinikera sana.
Wakati nawaza hivyo nikamuona yule mhudumu akija tena. Wakati ule nilikuwa namalizia ile bia yangu. Alikuja na chupa nyingine ya Kilimanjaro, akanifungulia.
“Nilikuwa sihitajji bia nyingine” nikamwambia.
“Sasa utakaa bure tu wakati hujui huyu mzee atatoka saa nagapi?”
“Basi kwa vile umeifungua nipatie tu”
“Mimi nimeagizwa niendelee kukuhudumia mpaka utakaposema basi” Msichana akaniambia.
“Ni nani aliyekuagiza?”
“Ni meneja wetu na yeye ameagizwa na bosi mwenyewe”
“Unahisi anaweza akanichelewesha sana?”
“Sina hakika. Ulikuwa na shida naye muhimu sana?’
“Tuna ahadi ya kuonana”
“Kama mna ahadi, sidhani kama atakuchelewesha sana”
“Nitajaribu kuendelea kumsubiri”
“Bia ya tatu kama huitaki nitaichukua mimi”
Mawazo ya msichana yalikuwa kwenye bia tu.
Aliponiambia hivyo sikumjibu kitu, nilibaki kumtazama. Akatabasamu na kuondoka.
Ile bia ya pili ambayo nayo niliinywa taratibu iliisha. Makita alikuwa hajatokea. Nikahisi huenda alikuwa amenisahau.
Yule msichana mhudumu akarudi tena. Alikuwa ameshika chano kilichokuwa na bia nyingine.
“Kama huitaki iache” akaniambia kabla sijamuuliza chochote. Akavuta kiti na kuketi.
“Utadhani nimekuja kulewa wakati nina kazi maalum”
“Kama huitaki nitakunywa mimi baadaye”
“Tatizo langu sio hilo. Tatizo langu mtu ninayemsubiri hatokei. Ninaishia kunywa bia”
“Sasa utafanyaje? Unataka kuondoka?”
“Kama Makita yupo siwezi kuondoka bila kuonana naye”
“Kunywa hii basi, mimi nitachukua nyingine kwa jina lako”
Ili kumridhisha yule msichana nikamkubalia. Nilikuwa nimeanza kuchangamka kidogo. Akanifungulia ile bia nyingine.
Baada ya kunifungulia aliondoka. Baadaye kidogo alirudi tena akiwa na bia nyingine. Akaketi na kuifungua. Aliipiga funda bila kutumia bilauli.
“Nimekuhisabia bia nne pamoja na hii” akaniambia baada ya kuiweka chupa juu ya meza.
Sikumjibu kitu. Akaondoka. Haukupita muda mrefu akatrudi tena na kupiga funda jingine.
“Unaitwa nani?” nikamuuliza baada ya bia kunichangamsha.
“Naitwa Edda” akanijibu.
“Edda unaishi wapi?”
“Kinondoni”
Nikagutuka kwa vile na mimi nilikuwa ninaishi huko huko.
“Kinondoni mtaa gani?”
Akanitajia mtaa kisha akapiga funda jingine kabla ya kuniuliza.
“Kwanini unaniuliza ninapoishi?”
Nikatabasamu kisha nikamwambia.
“Kuna siku naweza kukutembelea. Una mume”
“Wewe nitembelee tu, kama nina mume au sina utakuja kuona mwenyewe”
“Mmhh…mimi siwezi ngumi. Niambie mapema kama yupo nisije”
Msichana akacheka. Nikauona mwanya wake wa juu.
“Kumbe unaogopa ngumi!” akaniuliza.
“Si unauona uso wangu mzuri hauna ngeu”
“Usijali. Sina mume…”
“Basi nipe namba ya nyumba”
Msichana akanitajia namba ya nyumba anayoishi kisha akaniuliza.
“Nikupe na namba yangu ya simu?”
Bila shaka alikuwa amenipenda wakati mimi mwenzake nilikuwa namtania tu kupoteza muda.
“Nipatie ili tuwasiliane” nikamwambia.
Msichana akanitajia namba yake lakini hakuniuliza namba yangu.
Kwa vile alikuwa akinywa ile bia kwa kuibaiba aliinuka akaiacha chupa yake na kuondoka. Akaniacha nikiwa na hamu ya kuzungumza naye. Si unajua ulevi?
Msichana alipotokea tena, alikuwa na bia nyingine akaiweka bila kuifungua. Wakati ule nilikuwa nimebanwa na haja ndogo. Nilipomuona anaketi nikamwambia ninakwenda kujisaidia. Nikaondoka.
Niliporudi nilimkuta akimalizia bia yake na kufungua ile nyingine.
Tukaendelea kunywa. Kilevi kikanifanya nimsahau Makita. Akili yangu ikawa kwa yule msichana. Nakumbuka niliinuka tena nikaenda maliwatoni. Nilipotoka sikumuona yule msichana. Lakini chupa yake ya bia aliyokuwa ameinywa kidogo, ilikuwa juu ya meza.
Nikakaa na kumalizia bia yangu. Sikuweza kukumbuka tena baada ya hapo nini kilitokea. Nilikuwa kama nilipoteza fahamu. Sikuweza kujua kama niliendelea kunywa mpaka nikawa chakari au nini kilinitokea. Fahamu zangu zilizima kabisa.
Nilipokuja kuzinduka nilijikuta nipo kitandani ndani ya chumba ambacho hakikuwa chumba changu.
Nilikuwa sina nguo zaidi ya nguo ya ndani niliyokuwa nimevaa. Nikashituka na kujiuliza “Niko wapi?”
Wakati natembeza macho yangu ndani ya chumba hicho nikaona meza ndogo iliyokuwa na chupa tupu za bia. Nikakumbuka kwamba kabla ya kuzinduka na kujikuta nikiwa katika chumba hicho nilikuwa katika hoteli ya Makita nikinywa kilevi.
Sasa nikajiuliza, baada ya kulewa sana nilipangisha chumba katika hoteli hiyo na kuendelea kunywa humo chumbani?
Saa yangu ilikuwa mkononi. Nikaitazama na kuona ilikuwa saa moja asubuhi, tena tarehe ilionesha ilikuwa siku ya pili ya siku ile niliyokwenda kwa Makita.
Kama kweli nilikuwa katika chumba cha hoteli, maana yake nililala hapo hapo bila kujijua hadi asubuhi ile!
Nikashuka kitandani haraka. Ilikuwa kidogo niukanyage mwilli wa msichana uliokuwa umelala chini. Ulikuwa umevaa sare za wafanyakazi wa pale hoteli. Sikuwa na shaka yoyote ulikuwa mwili wa yule msichana niliyekuwa nikizungumza naye jana yake hapo hoteli.
Lakini uso wake ulikuwa umevimba na ulikuwa umekatwakatwa na kitu kama kisu au chupa.
Na hapo chini palikuwa na chupa zilizovunjika. Nguo za msichana huyo zilikuwa zimechanwachanwa na damu ilikuwa imemtapakaa kila mahali. Jinsi alivyokuwa ametoa macho alionesha wazi kuwa alikuwa amekufa.
Nikajiambia bila shaka baada ya jana yake kujiona nimelewa, nilikodi chumba hapo hoteli. Yule msichana akawa anaendelea kuniletea bia.
Lakini baadaye nilimgeukia na kutaka kumbaka na ndipo ilipotokea vurugu.
Bila shaka katika vurugu hiyo ama nilimkatakata kwa vipande vya chupa au nilimkaba na kumuua.
Sasa hii imeshakuwa balaa!
Jinsi nilivyokuwa nimevua nguo na kubaki na chupi ilionesha wazi kuwa nilitaka kufanya kitendo hicho nikiwa sijielewi kwa kilevi.
Nikaziona nguo zangu zikiwa chini upande wa pili wa kitanda. Nikashuka kwenye kitanda huku nikikwepa kuukanyaga mwili wa yule msichana.
Nilikuwa nataka kuchukua nguo zangu lakini nikaona kitambulisho kilichoanguka karibu na mwili wa msichana huyo. Nikainama na kukiokota. Ndipo nilipogundua kuwa mkono wangu wa kulia ulikuwa umetapakaa damu iliyokuwa imeganda kiganjani.
Damu hiyo ilinidhihirishia kwamba mimi ndiye niliyeufanya unyama ule. Hata hivyo nilikiokota kile kitambulisho ili nijue kilikuwa cha nani. Nikaona kilikuwa cha Edda Ibrahim Msangi!
Yule msichana aliniambia kuwa anaitwa Edda!
Huku moyo ukinienda mbio kama saa mbovu, nilisema.
“Mama yangu wee…! Nimeshaua…!”
Nikakirudisha kile kitambulisho pale chini nikamtazama yule msichana. Picha yake wakati ananihudumia jana yake ilinijia akilini. Wakati ule alikuwa mrembo na mwenye sura ya kupendeza. Lakini wakati namtazama pale chini alikuwa na sura ya kutisha sana kama siye niliyekuwa nimezumgumza naye.
Nikachukua nguo zangu na kuzivaa haraka haraka.
Wakati ninavaa nilikuwa nikiwaza kwamba katika maisha yangu sijawai kubugia kilevi kiasi kile. Sikuweza kujua ni kwanini niliendelea kulewa hadi fahamu zikanipotea.
Simu yangu ikawa inaita mfukoni mwa suruali yangu. Sikutaka hata kujua ni nani aliyekuwa ananipigia lakini sikutaka kusikia ule mlio wa simu. Nikatia mkono mfukoni na kuitoa.
Aliyekuwa akinipigia alikuwa Sofia. Sikupokea. Nikaikata. Nilikuta simu ambazo ziliita bila kupokelewa zaidi ya tatu.
Pia sikutaka kujua ni kina nani waliokuwa wananipigia na walinipigia usiku au asubuhi ile.
Nilipomaliza kuvaa nilikwenda kwenye mlango. Nilitaka kuufungua ili nitoke.
Lakini mlango haukufunguka. Ulikuwa umefungwa na ufunguo haukuwepo kwenye kitasa!
Nikajiambia leo ndiyo siku ya kukamatwa na polisi nikiwa humu humu chumbani. Bora kama ningeweza kufungua huo mlango ningeweza kutoroka hapo hoteli.
Sasa nikawa natafuta funguo.
“Funguo iko wapi jamani?” nikajiuliza kimoyomoyo. Nisingeweza kuendelea kukaa mle chumbani na mtu aliyekufa.
Nikatembeza macho yangu kila mahali. Ufunguo sikuuona. Sijui nilikuwa natazama nini pale kwenye kitanda, nikaona kitu kinameremeta. Niliposogea karibu nikaona ulikuwa ufunguo!
Nikajiuliza ufunguo huo ulifikaje kwenye kitanda?
Nikahisi huenda niliuondoa mimi kwenye kitasa ili kumzuia yule msichana asitoke mle chumbani. Bila shaka kitendo hicho nilikifanya kabla ya kumuua.