Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 7

KISIWA 07 Pict

ILIPOISHIA

Sasa nikawa natafuta funguo.

“Funguo iko wapi jamani?” nikajiuliza kimoyomoyo. Nisingeweza kuendelea kukaa mle chumbani na mtu aliyekufa.

Nikatembeza macho yangu kila mahali. Ufunguo sikuuona. Sijui nilikuwa natazama nini pale kwenye kitanda, nikaona kitu kinameremeta. Niliposogea karibu nikaona ulikuwa ufunguo!

Nikajiuliza ufunguo huo ulifikaje kwenye kitanda?

Nikahisi huenda niliuondoa mimi kwenye kitasa ili kumzuia yule msichana asitoke mle chumbani. Bila shaka kitendo hicho nilikifanya kabla ya kumuua.

SASA ENDELEA...


Nikaenda na ule ufunguo kwenye mlango, nikautumbukiza kwenye kitasa. Wakati nafanya hivyo, nikasikia mlango unabishwa kwa nje.

Kitendo hicho kilinishitua. Nikahisi kama walikuwa polisi waliokuja kunikamata.

Nikatulia kimya. Mlango ukabishwa tena.

Nikaamua kuufungua. Mlango ukafunguka. Nikachungulia nje na kumuona mtumishi wa hoteli aliyekuwa akifanya usafi kwenye korido.

“Usafi,” akaniambia.

“Unataka kuingia humu chumbani?” nikamuuliza.

“Ndiyo. Ni muda wa kufanya usafi.”

“Sawa.”

Nikarudi ndani na kufunga mlango. Nikasimama nyuma ya mlango na kujiuliza, huyu mhudumu akiingia humu chumbani na kumuona mwenzake, itakuwaje?

Nikajijibu mwenyewe kwamba atakapomuona atapiga kelele kuwaita wafanyakazi wenzake au atatoka mbio.

Kama ni hivyo, nikajiambia, mimi sikutakiwa kuwepo pale muda huo.

Nikaufungua tena ule mlango na kumchungulia. Nikamuona ameupita mlango wangu akiendelea kufagia korido. Hapo hapo nikatoka. Sikugeuka tena kumtazama.

Nilitembea haraka hadi kwenye ngazi. Nikashuka. Chumba nilichokuwemo kilikuwa ghorofa ya kwanza. Nilipofika sakafu ya chini, sikusemeshana na mfanyakazi yeyote, nikatoka nje ya hoteli.

Pikipiki yangu ilikuwepo pale pale nilipoiegesha jana yake. Nikaifuata.

Wakati naiwasha, nikasikia sauti kutoka juu ya ghorofa.

“Wewe kaka, usiondoke, hebu subiri...!”

Nilipotazama juu, nikamuona yule mhudumu wa usafi akichungulia dirishani. Bila shaka dirisha lile lilikuwa la chumba nilicholala.

Alikuwa ameingia kufanya usafi akakutana na maiti iliyokuwa imetapakaa damu!

“Usiondoke... usiondoke...” aliendelea kusisitiza.

Hapa ni lazima niondoke. Kama ni kukamatwa, ni baadaye, nikajiambia huku nikiwasha pikipiki na kuipanda. Nilitia gia huku macho yangu yakitazama juu.

Yule msichana alipoona nimepanda pikipiki, aliondoka dirishani. Bila shaka alikuwa anashuka ngazi ili atoe taarifa kwa wenzake kabla sijakimbia.

Lakini hawakunipata. Niliikimbiza pikipiki kwa kasi sana. Baada ya sekunde chache tu sikuwepo tena katika eneo hilo.

Baada ya kulitoka eneo la Masaki, niliona gari la polisi linakuja mbele yangu likiwa limewasha king’ora cha hatari. Nikajua polisi hao walikuwa wanakwenda katika Hoteli ya Makita baada ya kupigiwa simu.

Nilipishana na gari hilo la polisi lililokuwa linakwenda kwa mwendo wa kasi.

Hawakunitambua. Nikashukuru kimoyomoyo.

Sasa nikajiuliza niende wapi. Niende nyumbani kwangu au niende kazini kwangu?

Nyumbani nisingeweza kwenda. Huenda nikifika nitakutana na polisi wakinisubiri. Kadhalika, nikienda ofisini vilevile ninaweza kukamatwa.

Kwa vile nilijitambulisha pale hotelini kwamba nilikuwa mwandishi wa Gazeti la Kumekucha, polisi wanaweza kufika ofisini kwetu.

Sasa niende wapi? Nikaendelea kujiuliza.

Nilikuwa nimechafuka na sikuwa nimeoga. Mkono wangu ulikuwa na mabaki ya damu ya Edda iliyokuwa imeganda kwenye kiganja changu. Niliona nitafute mahali ambapo ningeweza kuoga na kujiweka vizuri kabla ya kufikiria la kufanya.

Nikapata wazo la kwenda kukodi chumba katika gesti ambako ningeoga na kupanga nifanye nini.

Nikaenda kukodi chumba katika gesti moja iliyokuwa pale Kinondoni lakini katika mtaa tofauti na ule niliokuwa ninaishi. Niliingiza pikipiki ndani.

Nikaoga na kusukutua maji. Nikajilaza kitandani na kuanza kuwaza kuhusu lile tukio lililotokea. Kusema kweli, sikujua tukio hilo lilitokeaje, lakini nilifahamu fika kwamba chanzo chake kilikuwa ni kulewa kupita kiasi.

Nilijiambia kosa langu lilikuwa kusahau majukumu yangu na kukubali kukirimiwa pombe ambayo hatimaye imesababisha nitende kosa la mauaji.

Nilikataa rushwa ya pesa, lakini nikakubali rushwa ya ulevi, ambayo adhabu yake nimeshaiona.

Nikarudia tena kujiambia kwamba iliwezekana baada ya kulewa nilimtamani yule msichana aliyekuwa akinihudumia, nikachukua chumba pale hotelini kwa ajili yake, ambapo aliendelea kunihudumia nikiwa chumbani.

Huenda alikataa kufanya mapenzi na mimi pale hotelini, lakini kwa akili zangu za kilevi nikaamua kumshika kwa nguvu na hatimaye yakatokea yaliyotokea.

Sikushangaa kuona nilitenda mambo yote hayo bila kujijua. Kama nilikunywa kupita kiasi wakati sikuwa na uzoefu wa kunywa pombe nyingi, iliwezekana nilipoteza akili. Nilishawahi kuona watu wenye hadhi kubwa wakifanya mambo ya aibu hadharani baada ya kuzidiwa na kilevi.

Wapo waliojaribu kubaka. Wapo pia waliotokwa na haja ndogo hadharani. Na wapo waliofikia hata kutaka kuvua nguo mbele za watu.

Labda kitu kilichonishangaza na ambacho nimekuwa nikijiuliza akilini mwangu bila kupata majibu ni kwa nini nililewa kupita kiasi. Katika maisha yangu sikuwahi kunywa pombe kiasi kile na hatimaye kufanya mambo ya ajabu.

Lakini pamoja na mawazo yote niliyokuwa nayo, jambo moja tu ndilo lililokuwa wazi mbele yangu kwamba sasa ninakabiliwa na kesi ya mauaji. Licha ya kukimbia kwangu pale hotelini, nilijua kwamba lazima nitakamatwa.

Kwa vile hakuna mtu anayewasubiri polisi wamkamate akiwa anajua ameua, ndiyo sababu nilikimbia.

Nikajiambia kama taarifa zitakuwa zimeshamfikia mhariri wangu, nisingeweza kufika tena ofisini hata kama polisi wasingekuwepo. Kwa vyovyote vile, tukio lile litakuwa limeitia aibu kampuni yetu na uongozi hautaweza kunivumilia.

Nikajikuta ninatikisa kichwa kwa masikitiko.

Nilikuwa bado mchanga na nilikuwa nina mengi ya kufanya ili kuandaa maisha yangu ya sasa na ya baadaye. Sasa yote hayo yatabaki kuwa ndoto ambayo haikutimia. Kesi ya mauaji ya kukusudia hukumu yake ni kifo. Tukio hili ndilo litakalozikatisha ndoto zangu za maisha.

Wakati nawaza hayo, nilikuwa nikiichezea simu yangu. Nikaona simu ambazo zilipigwa lakini sikuzipokea. Nikazifungua ili nione ni nani aliyenipigia.

Simu ya kwanza ilipigwa jana yake. Ilitoka kwa mhariri wangu.

Simu ya pili ilipigwa jana yake pia, na ilitoka kwa Sofia. Simu ya tatu ilipigwa asubuhi ile, nayo ilitoka kwa mpangaji mwenzangu ambaye nilikuwa ninaishi naye pale nyumbani. Sikuweza kujua alikuwa ananipigia ili anieleze nini.

Hapo hapo nikapata wazo la kuingia kwenye blogu yoyote ili nione kama walikuwa wameshapata ile habari. Kulikuwa na blogu moja ambayo nilikuwa naiiamini kwa habari za papo kwa papo. Nikaingia kwenye blogu hiyo nikiwa sina matumaini kwamba habari ile itakuwa imewafikia.

Macho yangu yakakutana na Breaking News. Ilikuwa ni habari iliyowekwa dakika ileile ikiwa na kichwa MWANDISHI MAARUFU AKUMBWA NA KASHFA YA MAUAJI.

Sikutaka hata kuisoma, lakini nikajilazimisha ili nijue wameeleza nini.

Habari ilieleza kwamba mwandishi maarufu, wakataja jina langu, alifika katika hoteli moja iliyopo Masaki, wakaitaja kwa jina, na kueleza kuwa nilifanya mauaji.

Waliendelea kueleza kuwa tangu jana yake nilifika katika hoteli hiyo nikimtafuta bosi wa hoteli, lakini nikaanza kuagiza pombe na hatimaye nikakodi chumba na kuendelea kunywea humo.

Habari ikaendelea kueleza kuwa nikiwa humo chumbani nilimtaka kimapenzi msichana aliyekuwa akinihudumia ambaye walimtaja kwa jina la Edda. Habari ikafafanua kuwa msichana huyo aliponikataa, nilimshika kwa nguvu na kumuua kwa kumkaba na kumkata kwa vipande vya chupa.

Kamanda wa Polisi, ambaye alithibitisha tukio hilo kwa njia ya simu, alisema mhudumu wa usafi wa hoteli hiyo ndiye aliyegundua kuuawa kwa msichana huyo baada ya kuingia chumbani humo, ambapo mtuhumiwa alitoroka kwa pikipiki.

Taarifa ikamalizia kueleza kuwa polisi wanamsaka mwandishi huyo ili afikishwe mahakamani kwa kosa la mauaji.

Habari ile ilikuwa kama imeniongezea maumivu ya moyo. Niseme ukweli, wazo la kufikishwa mahakamani kwa kosa ambalo nilijua hukumu yake ni kunyongwa lilinifanya nitamani nife kabisa kuliko kusubiri kunyongwa.

Nikashuka kitandani nikiwa na wazo la kwenda nyumbani kuchukua baadhi ya nguo zangu na vitu vyangu muhimu, kisha nikimbie Jiji la Dar es Salaam kabla ya kukamatwa.

Lakini hapo hapo simu yangu ikaita. Nilipoangalia skrini nikaona namba ya mhariri wangu. Nikajiuliza niipokee au nisiipokee. Nikaona niipokee ili nimweleze ukweli. Sikuona kama kulikuwa na kitu cha kuficha.

Nikaipokea.

“Shikamoo mkuu,” nikamwamkia.

“Marahaba. Mbona hujaonekana tangu jana?”

Nikamweleza kile kilichotokea.

“Kwani wewe uko wapi?”

“Sipendi kusema nilipo, lakini nipo hapa Dar.”

“Hizo taarifa tumeshazipata. Sasa nataka uje hapa ofisini.”

“Sitaweza kuja. Bado nafikiria nifanye nini.”