Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KISIWA CHA MAUTI - 16

KISIWA - 16 Pict

ILIPOISHIA

Mwili ulinisisimka nilipokiwaza kitanzi kikikaza kwenye shingo yangu. Nikawaza mengi. Nikamkumbuka hadi mfungwa mmoja  wa kisiasa wa nchi za nje aliyekatika kichwa wakati  ananyongwa. Jambo hilo halikuwa la kuwaza wakati kama ule wa usiku. Lazima akili itapata maruweruwe.

Hata hivyo nikapuuza mambo ya ndoto na kushikilia msimamo alionieleza mahabusu mwenzangu kuwa nijipe matumaini kuwa  nitashinda kesi ingawa upande mwingine wa akili yangu ulikuwa ukiamini kile nilichokiota.

SASA ENDELEA...


Asubuhi kulipokucha tuliletewa uji tukanywa. Majira ya saa nne hivi nikaja kutolewa mahabusi. Nikajua ama nilikuwa napelekwa mahakamani au ninakwenda kuhojiwa tena. Lakini sikupelekwa katika ile ofisi ya mrakibu, nilitolewa nje kabisa ya kaunta ya polisi, mahali ambapo hukaa wageni wanaohitaji msaada wa polisi au watu wanaokuja kudhamini mahabusu.

Nikaambiwa nisubiri kidogo kabla ya kupata maelezo. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa niliachwa huru bila ulinzi wowote, kinyume na ilivyokuwa siku mbili zilizopita.

Hakukuwa na polisi yeyote aliyekuwa akinifatiliza. Kila polisi alikuwa na shughuli zake. Nikajikuta nimechanganyika na raia wengine waliokuja hapo kituoni kwa shida mbalimbali.

Mwishoni nikaamua kukaa kwenye benchi lililokuwa pembeni huku nikiamini kuwa pengine nilikuwa nimeachiwa. Haukupita muda mrefu nikamuona Edda akiingia kwenye kituo hicho. Aliponiona alitabasamu na kunifuata.

“Nilijua uko Kibaha?” nikamwambia.

“Sikwenda Kibaha,” akaniambia huku akiketi kwenye lile benchi.

“Kwanini?” nikamuuliza.

“Wamenifukuza kazi jana.”

“Umefukuzwa kazi! Kwanini?”

“Kwa sababu yako wewe.”

“Mimi?”

“Wewe ndiyo. Nimeambiwa njama zetu ni moja mimi na wewe, eti kwa sababu ulikutwa nyumbani kwangu.”

“Kumbe yamekutokea hayo! Pole sana. Sasa mimi na wewe tuna njama gani jamani?”

“Wapuuzi. Lakini wamekomolewa. Janja yao imebainika.”

“Wamekomolewa kivipi?”

“Huoni kuwa umetolewa?”

“Nimeambiwa nisubiri hapa, lakini sijapata maelezo yoyote.”

“Jana nilikutana na mhariri wako nikazungumza naye.”

“Ulizungumza naye nini?”

“Kuna mambo makubwa yamegunduliwa….”

Edda akafungua mkoba wake na kunitolea gazeti. Lilikuwa gazeti letu la Kumekucha. Lilikuwa toleo la siku ile.

“Soma hiyo habari iliyoko ukurasa wa mbele,” Edda akaniambia.

Nikalikunjua lile gazeti kwa shauku na kutupa macho yangu kwenye ukurasa wa mbele.

Nikashituka nilipoona kichwa kilichosema:

SINEMA YA MAUAJI HOTELI YA NEW STAR. MENGI YAIBUKA.

Kulikuwa na mistari miwili ya vichwa vidogo ambayo ilisomeka:

“Msichana aliyedaiwa kuuawa alikufa katika ajali ya daladala iliyotokea Kimara.”

“Maiti yake iliibwa hospitalini ili kutengeneza kesi dhidi ya mwandishi wa habari.”

Mwandishi wa habari ile ambaye aliweka jina lake alikuwa mhariri wangu.

Huku mwili ukinisisimka, nilianza kuisoma ile habari.

Nikajikuta ninasoma mkasa wa kusisimua na kushangaza.

Katika mkasa huo kulikuwa na maelezo yaliyohusu daladala iliyopata ajali maeneo ya Kimara siku nne zilizopita. Kulikuwa na wasichana sita waliokufa hapo hapo na walikuwapo majeruhi kumi na wawili.

Miili ya wasichana hao ilipelekwa hospitali ya Mwananyamala. Jioni ya siku ile ile, meneja wa hoteli ya Makita alifika hospitalini hapo na kuikagua miili ya watu waliokufa. Akadai kwamba mwili wa msichana mmoja ulikuwa wa mdogo wake na akaomba kuuchukua.

Baada ya kukabidhiwa mwili huo, akiwa na vijana wake wawili waliupakia kwenye gari na kuondoka. Asubuhi ya siku iliyofuata, mama mmoja miongoni mwa watu waliokwenda hospitalini hapo kukagua miili ya jamaa zao akadai kwamba hakuona mwili wa binti yake ambaye alikuwemo katika ile daladala iliyopata ajali.

Siku ya tatu yake tena mama huyo akaenda hospitali ya Muhimbili ambako aliukuta mwili wa binti yake huyo. Lakini alipotaka kuuchukua kwa ajili ya mazishi akaambiwa huo mwili ni wa msichana aliyeuawa katika hoteli ya New Star.

Mama huyo hakukubali. Akaendelea kusisitiza kuwa huo ulikuwa mwili wa mwanawe aliyekufa katika ajali ya daladala na uliondolewa katika hospitali ya Mwananyamala katika mazingira ambayo hayakueleweka.

Lakini uchunguzi wa mwandishi wa ile habari ukabainisha kuwa mwili huo ulipochukuliwa na meneja wa hoteli ya Makita ulikwenda kupodoolewa na kuvishwa sare za hoteli ya Makita na kisha kulazwa katika chumba alicholala Masha ili ionekane ni mfanyakazi wa hotelini hapo.

Uchunguzi huo uliendelea kubainisha kuwa ili kuonesha kuwa msichana huyo ni mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, kando yake waliweka kitambulisho cha mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo anayeitwa Edda.

Uchunguzi wa mhariri wa gazeti hilo haukuishia hapo tu, bali ulikwenda mbali zaidi na kuonesha kuwa kabla ya mchezo huo kufanyika, mwandishi aliyekwenda hotelini hapo kutaka kuonana na Makita alikataa rushwa ya shilingi milioni kumi alizotakiwa kupewa ili asiandike habari ya mali za Makita.

Baada ya mbinu ya kumpa rushwa kushindikana ndipo alipowekewa dawa za kulevya katika kilevi. Baada ya Masha kupoteza fahamu, alipelekwa katika chumba kimoja miongoni mwa vyumba vya hapo hotelini akalazwa.

Na ili ionekane kuwa alikuwa akiagiza bia akiwa chumbani, meneja wa hoteli hiyo aliweka chupa tupu kadhaa kwenye chumba hicho na nyingine alizivunja kuonesha kuwa kulitokea purukushani humo chumbani.

Saa sita usiku ndipo mwili ulioibwa kutoka hospitali ya Mwananyamala ulipoingizwa chumbani humo na kulazwa chini ukiwa bado una damu. Kwa vile mwili huo ulipodoolewa na kuvalishwa sare za wafanyakazi wa hapo hotelini, ulionekana kama wa mfanyakazi wa hotelini hapo huku kando yake pakiwa na kitambulisho cha Edda.

Habari zikaendelea kueleza kuwa Masha alipopata fahamu asubuhi ilibidi akimbie kwa kuhisi kuwa alikuwa ameua, kumbe alikuwa amebambikiwa maiti ili atengenezewe kesi ya mauaji kwa lengo la kumkomoa kwa vile alitaka kuandika habari zilizohusu mali za Makita.

Bila shaka mhariri wangu aligundua jinsi nilivyochanganyikiwa baada ya kukimbia hapo hotelini, kwani alieleza kuwa badala ya kwenda kuripoti polisi, niliamua kukimbia pamoja na pikipiki ya kampuni na kwenda kujificha mahali pasipojulikana.

Akaendelea kuandika kuwa nilifanya juhudi ya kumtafuta msichana niliyedaiwa kumuua na kufanikiwa kukutana naye, ambapo nilishangaa kumuona msichana huyo akiwa hai.

Mhariri alimkariri Edda ambaye alikutana naye kabla ya gazeti kwenda mitamboni, ambapo alimueleza kwamba hakuwa amekufa na kwamba habari za yeye kuuawa alikuwa hazijui.

Mhariri aliendelea kueleza kuwa Edda alidai kuwa alikuwa anahamishiwa katika hoteli ya Makita iliyoko Kibaha kwa kile ambacho mhariri huyo alikieleza kuwa ni mbinu ya kumficha Edda asije akaonekana wakati walishasingizia kuwa ameuawa.

Akaendelea kueleza kwa vile ilivyobainika kuwa Edda hakuuawa, uhamisho ukafa na Edda akafukuzwa kazi baada ya Masha kukamatwa akiwa nyumbani kwake.

Ili kupata habari kamili, mhariri alieleza kuwa alifanya mahojiano na baadhi ya maafisa wa polisi, akiwamo kamanda wa polisi, kabla ya gazeti kwenda mitamboni na kugundua jinsi polisi walivyotatizika na kadhia hii.

Mhariri akamalizia kwa kuandika kuwa hadi wakati wanakwenda mitamboni, Masha alikuwa bado ameshikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji hewa.

Kwa kweli baada ya kusoma habari zile nilimshukuru Mungu na ndipo nilipogundua kilichokuwa nyuma ya pazia.

Kumbe ile maiti ya msichana iliibwa hospitalini na kuja kuwekwa katika chumba nilichokuwa nimelala ili ionekane nimemuua mimi.

Kwanza nilimshukuru sana mhariri wangu kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kufuatilia na kuifanyia uchunguzi wa kina kadhia ile.

Hapo ndipo nilipoamini nguvu ya vyombo vya habari ni kubwa katika kufichua na pia kubadili mitazamo ya watu, kama vile ilivyobadili ghafla mtazamo wa polisi na kuamua kuniachia kimya kimya.

Niliamini kuwa polisi waliniachia baada ya kusoma zile habari na kugundua kuwa zilikuwa na ukweli.

Pia niligundua kuwa polisi hao waliniachia kimya kimya kwa sababu walikuwa wanaona aibu kwa jinsi gazeti lilivyoweza kufanya uchunguzi na kufichua ukweli. Vinginevyo ilikuwa nifikishwe mahakamani na kushitakiwa kwa mauaji.

Kwa upande mwingine niliamini kuwa Makita alikuwa mtu hatari na mjinga, japokuwa amesoma. Kitendo alichofanya ili kunizima nisiandike habari zake ni cha hatari na cha kijinga.

Hapo hapo nikampa mkono Edda.

“Asante Edda,” nikamwambia.

“Unanipa asante ya nini?” Edda akaniuliza.

“Nakupa asante kwa sababu umeonesha ujasiri na umetoa mchango mkubwa katika kuachiwa kwangu. Ninaamini kuwa mhariri wangu alipata ujasiri wa kutoa hii habari baada ya kuonana na wewe na kupata maelezo yako.”

“Na mimi pia nimefurahi. Hata kama wamenifukuza kazi, lakini nimetimiza wajibu wangu.”

“Mhariri wangu pia anastahili sifa. Amefanya kazi nzuri. Naamini baada ya polisi kusoma hii habari ndipo walipoamua kuniachia.”

Wakati nazungumza na Edda akaja yule mrakibu wa polisi na kuniita ofisini kwake.

Tulipoingia ofisini kwake akanikaribisha kwenye kiti. Muda ule sauti yake ilikuwa ni ya kawaida. Haikuwa kali kama ile aliyokuwa nayo juzi na jana yake. Bila shaka ni baada ya kuona sikuwa na kosa.

Akajidai kuniuliza.

“Wamekuachia saa ngapi?”

“Mimi sijui kama wameniachia,” nikamwambia.