KISIWA CHA MAUTI - 10
ILIPOISHIA
Sikumjibu kitu. Nililishika gazeti hilo la pili ambalo ni la kampuni niliyokuwa ninafanya kazi.
Habari kama ile niliyoisoma ndiyo iliyokuwa katika ukurasa wa mbele. Mwandishi alikuwa ni mhariri wangu.
Habari hiyo ilikuwa na kichwa kilichosema.
NI MAUAJI YA UTATA
Mhariri wangu aliandika habari ile kwa mtazamo tofauti akiwataka polisi kufanya uchunguzi wa kina. Mhariri wangu alisema mwandishi wao alikwenda kikazi hotelini hapo.
SASA ENDELEA...
“Kwanini waandike wewe umeuawa wakati mimi niliyeuawa sina habari?” Edda akaniuliza.
“Kama lilivyoandika hili gazeti letu, haya mauaji yana utata, lakini ni kweli mauaji yametokea.”
“Wewe ndiye umeua?”
“Ngoja nikueleze kilichotokea.”
Nikamueleza Edda ukweli wote bila kumficha.
“Mbona unanitisha, Masha! Basi kama umeua, umemuua Edda mwingine, si mimi. Ngoja nijaribu kumpigia simu. Namba yake ninayo.”
Edda akampigia msichana huyo. Simu ikaita. Sote tukashangaa.
“Imepokelewa,” Edda akaninong’oneza, kisha akasema kwenye simu:
“Edda, habari yako?”
Sauti ya msichana wa upande wa pili niliisikia.
“Nzuri. Uko wapi?”
“Niko nyumbani. Leo naingia mchana. Eti, kumetokea nini hapo hotelini?”
“Kwani umesikia kumetokea nini?”
“Nimesikia kuna mauaji yametokea. Na cha kushangaza, magazeti yameandika wewe ndiye umeuawa!”
“Nimeuawa?”
“Kwani hujaona kwenye magazeti?”
“Sijasoma gazeti lolote. Labda wamekosea. Mimi si niko hai tunazungumza.”
“Ndiyo, nashangaa.”
“Achana na habari hizo, tutaonana mchana.”
“Poa.”
Edda akakata simu.
“Hata huyo Edda mwingine niliyemfikiria ni mzima. Hii habari itakuwa imeandikwa kwa makosa,” Edda akaniambia.
“Labda,” nikamwambia, lakini ndani ya moyo wangu nilijua kuwa tukio hilo lilitokea kweli. Maiti niliishuhudia kwa macho yangu. Na niliamini kuwa polisi walikuwa wananitafuta kweli.
Kwamba niliyemuua si Edda isingetosha nijipeleke polisi. Huenda nimeua mtu mwingine. Na kilichokosewa ni jina tu.
Ghafla simu ya Edda ikaita.
Edda alipotazama skrini ya simu yake akaniambia:
“Meneja ananipigia.”
Kisha akaipokea simu.
“Hello, bosi!”
“Habari ya asubuhi?” sauti ikasikika kutoka upande wa pili wa simu.
“Nzuri, bosi.”
“Nakuja nyumbani kwako, nina mazungumzo kidogo. Si uko nyumbani?”
“Ndiyo, niko nyumbani.”
“Nisubiri, ninakuja.”
“Bosi, mbona unanishitua? Kuna mazungumzo gani?”
“Nitakuja kukuambia. Hivi niko njiani. Nakaribia kufika kwako.”
Simu ya upande wa pili ikakatwa.
“Meneja ameniambia anakuja kwangu. Hivi yuko njiani. Sijui ana habari gani!” Edda akaniambia akidhani sikuisikia sauti ya meneja huyo.
“Labda ni habari hii hii ya mauaji.”
“Kwamba anakuja kuniambia wamekosea kuandika jina langu?”
“Labda.”
“Si angeniambia tu kwenye simu kwamba nisishituke...”
“Sasa sijui kama ana habari nyingine.”
“Sasa mimi sitaki meneja wako anikute hapa kwako.”
Wakati namwambia hivyo, tukaona gari linafunga breki barazani. Tuliliona kupitia dirishani.
“Tena meneja mwenyewe huyo amefika,” Edda akasema.
“Ataingia humu ndani?”
“Kama ana mazungumzo, ataingia.”
“Mimi sitaki anikute humu chumbani mwako.”
“Sasa tutafanyaje na ameshafika?”
“Si unajua wananitafuta wanikamate!”
Mara tukasikia mlango wa gari ukifunguliwa na kufungwa. Nilikuwa nimemtolea macho Edda, ambaye alionekana hakuwa na ufumbuzi.
“Inabidi niende nikamkaribishe,” Edda akaniambia.
“Sasa nitajificha wapi?”
“Basi ingia mvunguni mwa kitanda kama utaweza.”
Nikakitazama kitanda. Kilikuwa na uwazi wa kutosha chini ya mvungu.
Wakati ule nakubaliana na maelekezo ya Edda, mlango wa mbele ukabishwa. Nikakurupuka na kujilaza chini kando ya kitanda, kisha nikajiburuza kuelekea mvunguni mwa kitanda.
Edda alisimama na kunitazama, kisha akatoka kwenda kumfungulia mlango meneja wake.
Nilifanikiwa kuingia mvunguni kabisa mwa kitanda, ambako kulikuwa na giza na pasipofaa kukaa binadamu hata kwa dakika moja. Kulikuwa na vumbi ambalo nilikuwa nikilipumua na kunikereketa kooni.
Muda ule ule nilioingia humo mvunguni nililazimika kupiga chafya mara mbili. Nikajiambia kama nitaendelea kupiga chafya wakati huyu meneja akiwa humu chumbani, atashituka na kugundua kuwa kuna mtu aliyejificha mvunguni, na bila shaka atamuuliza Edda kuna nani mvunguni.
Wakati nawaza hivyo, nikamuona Edda na meneja wake wakiingia. Niliona miguu yao. Kwanza ilitangulia kuingia miguu ya Edda, kisha ya huyo meneja.
“Karibu ukae,” nikamsikia Edda akimwambia meneja huyo.
Meneja akakaa kwenye sofa na Edda naye akakaa kitandani.
Ikanijia chafya nyingine. Nikajaribu kuibana. Nilivuta pumzi, kisha nikazuia na kuishusha taratibu ili isisikike.
“Chumba chako kidogo sana,” nikaisikia sauti ya meneja akimwambia Edda.
“Nyumba za Dar zote zina vyumba vidogo. Hata ukiwa na vyombo vyako huwezi kuviweka labda upangishe vyumba viwili,” Edda akamjibu.
“Si vibaya kuwa na vyumba viwili. Kimoja unakitumia kama sebule, kingine cha kulala.”
“Ni gharama. Mimi napenda sana niwe na chumba kingine cha sebule, lakini ni gharama. Mshahara ninaopata hautoshi kulipia vyumba viwili, kisha nipate pesa ya kula na kukidhi mambo mengine.”
“Una maana huna mwenzako humu ndani?”
Moyo wangu ukashituka.
“Sina. Niko mwenyewe tu,” Edda akamjibu bila hofu.
“Unataka uniambie hakuna shemeji anayeingia chumbani mwako?”
Chafya nyingine ikanijia. Nikajaribu kuibana na kuishusha taratibu. Hata hivyo, ilisikika. Nina imani Edda aliyekuwa amekaa kwenye kitanda aliisikia.
Kutokana na kuvuta hewa yenye vumbi, nilipata hali mbaya sana humo mvunguni.
Nikajiambia kama huyu mtu atakaa kwa muda mrefu humu chumbani, itabidi nitoke nitake nisitake.
“Chumbani mwangu haingii mtu. Hao mashemeji tunamalizana huko huko. Kama mtu anataka kuja hapa, ahudumie chumba. Kama hawezi, asiingie.”
Edda alisema na kucheka. Meneja naye akacheka.
Walipomaliza kucheka, pakapita ukimya wa sekunde kadhaa, kisha nikamsikia meneja akimwambia Edda:
“Nimekuja kukufahamisha kuhusu mabadiliko ya kazi. Bosi amekuhamishia katika hoteli yetu nyingine.”
“Hoteli gani tena?” Edda akauliza kwa mshangao.
“Hoteli yetu ya Kibaha. Yaani kwa leo hutakuja kazini. Leo si utaingia mchana?”
“Ndiyo.”
“Sasa leo usije kazini. Jiandae kwa safari ya Kibaha.”
“Huko Kibaha natakiwa niripoti lini?”
“Kesho mchana. Utaondoka hapa asubuhi. Itakuja gari kukuchukua.”
“Mbona imekuwa haraka haraka hivyo? Sikujulishwa mapema?”
“Kuna mfanyakazi wetu mmoja wa hoteli ya Kibaha aliacha kazi ghafla jana. Sasa wewe unatakiwa ukazibe pengo lake.”
“Hadi lini, au ndiyo moja kwa moja?”
“Hadi atakapoajiriwa mfanyakazi mwingine.”
“Nitarudishwa huku huku?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo chumba changu sitakitoa.”
“Usikitoe. Huendi kukaa moja kwa moja.”
“Sasa huko nitafikia wapi? Sina ndugu wala rafiki.”
“Utalala pale pale hotelini.”
“Kama hivyo ni sawa.”
Pakapita kimya kingine kifupi kabla ya Edda kuuliza:
“Kuna jingine?”
“Hapana, ni hilo tu.”
Nikamuona meneja akinyanyuka.
“Kuna kitu nilitaka kusahau,” akamwambia Edda, kisha akaongeza:
“Umesoma magazeti ya leo?”
“Nimesoma. Nimeona habari ya kushangaza inayosema nimeuawa na mwandishi wa habari niliyekuwa nikimhudumia jana.”
Hapo ndipo nilipopata tatizo. Pengine ni kile kiherehere changu; lile vumbi nililokuwa nikivuta sasa lilinisababishia kutaka kukohoa. Nilihisi koo linawasha kabisa.
Nikajaribu kumeza mate. Haikusaidia. Kikohozi kiliendelea kunijia kwa nguvu. Kama ningekohoa, yule mwanamke angenisikia bila shaka yoyote.
Nikakibana kifua, kisha nikajikohoza kimyakimya kama mtu aliyekabwa. Nilifanya hivyo mara mbili. Kifua kikatulia kidogo, lakini nilijua kikohozi kingerudi tena muda si mrefu.
Edda hakumweleza kwa mdomo tu, bali alimuonesha na yale magazeti niliyokuwa nimeyaacha juu ya sofa.
Nilitoa kichwa kidogo na kumchungulia meneja huyo.
Nikaona alikuwa ameshika gazeti la Kumekucha akilisoma.
Ni kama alilipitishia macho tu, akaliacha na kushika lile gazeti jingine. Nalo, baada ya kusoma kichwa cha habari, alilirudisha kwenye kochi.
“Kuna tukio kama hilo limetokea?” Edda akamuuliza alipomuona meneja anachukua muda kumjibu.
Edda alionekana dhahiri kuwa alikuwa na kiherehere cha kupata ukweli.