KISIWA CHA MAUTI - 11
ILIPOISHIA
Nikaona alikuwa ameshika gazeti la Kumekucha akilisoma.
Ni kama alilipitishia macho tu akaliacha na kushika lile gazeti jingine.
Nalo baada ya kusoma kichwa cha habari alilirudisha kwenye kochi.
“Kuna tukio kama hilo limetokea?” Edda akamuuliza alipomuona meneja anachukua muda kumjibu.
Edda alionekana dhahiri kuwa alikuwa na kiherehere cha kupata ukweli.
SASA ENDELEA...
“Ndio tukio limetokea, labda wewe hujapata habari. Kuna msichana ameuawa pale hoteli juzi usiku,” meneja huyo alimwambia kwa utulivu.
“Msichana gani?” Edda akamuuliza kwa pupa.
“Ni mfanyakazi wetu. Hilo tukio mimi pia nilijulishwa nikiwa nyumbani. Lilitokea usiku na lilijulikana asubuhi.”
“Aliyefanya hayo mauaji ni nani?”
“Ni yule mwandishi uliyekuwa unamhudumia jana. Kumbe alikuja na yake. Si alichukua chumba wakati wewe upo?”
“Hapana. Mimi nilikuwa nimeshaondoka.”
“Basi alichukua chumba. Kumbe alikuwa na nia ya kumbaka yule mhudumu uliyemuachia. Sasa wakapurukushana humo chumbani. Akamuua mwenzake kisha akatoroka.”
“Kuna mhudumu aliyeuawa hapo hotelini?”
“Ndiyo. Walikosea wakaandika jina lako, lakini yeye pia anaitwa Edda.”
“Ndiyo, nilipoondoka nilimuacha Edda akimhudumia yule kaka.”
“Basi ndiye huyo aliyeuawa.”
“Lakini Edda nilimpigia simu hivi asubuhi akaniambia hajui kama kuna tukio kama hilo.”
“Kumbe ulimpigia simu? Unajua mimi sikuwepo wakati tukio hilo linatokea, na wakati nafika ofisini huyo mhudumu alikuwa ameshaondolewa. Inawezekana ni msichana mwingine. Pale si mko wengi.”
“Hujamfahamu?”
“Nikirudi ndiyo nitauliza vizuri.”
“Nilivyompigia Edda ameniambia hajui kama kuna tukio kama hilo!”
“Atajuaje wakati hajafika kazini? Yeye pia anaingia mchana.”
“Nashukuru kwa kunifahamisha kwamba si mimi niliyetajwa. Nilipata wasiwasi sana.”
“Ndiyo maana ulinunua magazeti mawili.”
“Nilinunua magazeti mawili ili kupata ukweli, lakini sikuupata mpaka wewe ulivyokuja kunieleza. Unajua ndugu zangu huko bara wakisikia watapata wasiwasi. Nimeshapigiwa simu nyingi kutoka kwa ndugu na marafiki.”
“Wakikupigia waambie si wewe. Majina tu yamefanana. Kwanza hakukuwekwa picha yako, na mimi nilitaka picha isitoke.”
“Sawa, nashukuru sana. Basi nitajiandaa kwa safari ya huko Kibaha.”
“Sawa. Gari litakufuata kesho saa tatu asubuhi. Dereva akija akukute umeshajiandaa.”
“Sawa.”
“Haya, mimi naenda.”
“Ngoja nikutoe.”
Edda na meneja wake wakatoka. Sikutoka mvunguni mpaka niliposikia mlango wa gari ukifunguliwa na kufungwa. Nilipotoka mvunguni nilikuwa nimejaa vumbi. Nikaanza kujikung’uta.
Edda aliporudi chumbani alinikuta nikiendelea kujifuta vumbi.
“Eh, umechafuka sana. Inaelekea huko mvunguni kuna vumbi jingi,” akaniambia.
Alichukua kitambaa na kuanza kunifuta. Alinifuta shati langu pamoja na suruali.
“Kwanini hufagii huko mvunguni?” nikamuuliza.
“Huo muda ninao, baby wangu?”
“Hebu jaribu kufagia leo kwani nilikuwa karibu nitoke kwa kikohozi cha vumbi.”
“Nitafagia.”
“Halafu kaninunulie pakiti ya maziwa. Koo langu limeharibika kabisa.”
“Ngoja nikakununulie, halafu tuje tuzungumze.”
Edda akakiweka kitambaa alichokuwa akinifutia vumbi kisha akatoka.
Nikakaa kwenye sofa nikilielekea pangaboi.
Sasa nikaanza kuyatafakari maneno ya yule meneja ambayo niliyaona wazi kuwa yalikuwa na utata. Sikuweza kujua Edda aliyachukuliaje, lakini kwa upande wangu niliona kulikuwa kuna kitu kinafichwa. Ilikuwa ni kama alivyoandika mhariri wangu, “Ni mauaji yenye utata!”
Nilijiuliza, kama habari zile zilizoandikwa zilimkariri meneja pamoja na Jeshi la Polisi, kwanini meneja mwenyewe aseme hajui aliyeuawa mpaka aende akaulize?
Na ni kwanini aseme aliyeuawa ni Edda mwingine, lakini alipoambiwa kwamba Edda huyo alipigiwa simu na kueleza kuwa alikuwa hajui kilichotokea, akabadili maneno?
Ni kitu gani kinachofichwa hapa? Nikajiuliza bila kupata jibu.
Nilikuwa na hakika kwamba meneja huyo aliyeongea na Edda alikuwa anaficha kitu. Alibabaika sana kuyajibu maswali ya Edda. Nilijua kuwa Edda alishindwa kumbana kwa sababu alikuwa bosi wake.
Mara Edda akaingia akiwa na pakiti ya maziwa.
“Nimekuchukulia maziwa baridi,” akaniambia huku akinipa pakiti ya maziwa aliyokuwa ameishika.
“Yanafaa,” nikamjibu huku nikiipokea ile pakiti.
“Sasa hebu kaa unieleze alichokwambia meneja wako.”
“Kwani hukumsikia?” Edda akaniuliza huku akiketi kando yangu.
“Nimemsikia, lakini nilitaka unipe tathmini yako kuhusu maneno yake.”
Niliing’ata ncha moja ya pakiti hiyo ya maziwa na kuanza kuyagugumia kinywani.
“Unajua kuwa sikumuelewa. Aliponiambia wamekosea kuandika jina langu, halafu ananiambia ni Edda mwingine, wakati Edda mwingine nimeongea naye na hajui kumetokea nini!” Edda aliniambia.
“Sasa umeyachukuliaje maneno yake?” nikamuuliza kabla ya kuimaliza ile pakiti ya maziwa.
“Hakuna chochote kilichotokea.”
“Kipo. Ni kweli nililala kwenye chumba cha hoteli na maiti ya huyo msichana niliyemdhani ni wewe ilikuwemo chumbani.”
“Una uhakika?”
“Nina uhakika.”
“Una maana kuwa uliua?”
“Sina kumbukumbu za kuua, na kama niliua ni lazima niliyemuua afahamike.”
“Ni kweli. Sasa utafanyaje?”
“Nitaendelea kujificha mpaka yule niliyemuua atakapotajwa.”
“Sasa mimi napelekwa Kibaha, itakuwaje?”
“Itabidi nitafute mahali pengine pa kujificha. Nyumbani kwangu siwezi kurudi, nitakamatwa.”
“Masha, naomba uwe muwazi, nini kilitokea hapo hotelini?”
“Nakuapia vile, sijui nini kilitokea. Kila kitu nakiona kama sinema!”
“Umeua?”
“Kama nimefanya hivyo sikuwa nikijielewa.”
“Lakini pia upande huu wetu nao siuelewi. Wanatoa taarifa polisi ya kuuawa mtu hotelini, lakini mtu mwenyewe aliyeuawa hawamjui. Wanataja mtu mwingine!”
“Kauli ile ya meneja wako inanitia mashaka sana.”
“Umesema hutarudi nyumbani kwako?”
“Sitarudi. Ninajua nikienda nyumbani ninakamatwa.”
“Waambie hao polisi, mbona huyo mtu ninayetuhumiwa kumuua yuko hai? Waelekeze ninapoishi. Watakuja kunikuta.”
“Ingekuwa sikuuona maiti mle chumbani ningefanya hivyo, lakini niliiona maiti ya msichana mfanyakazi wa pale hotelini. Huyo meneja wenu si amekwambia anakwenda kuulizia yule msichana ni nani?”
“Unajua ninakufikiria wewe?”
“Unanifikiria nini?”
“Utafanyaje wakati mimi ninaondoka kesho na wewe upo hapa kwangu?”
“Unaweza kwenda tu. Mimi nitatafuta sehemu nyingine au pia naweza kusafiri kwenda kwetu Pemba.”
“Lakini ni lazima kwanza ujue ni nani uliyemuua.”
“Ndiyo. Sitaondoka hapa Dar mpaka niliyemuua atajwe.”
Kilichonipa moyo ni kuwa Edda hakubadilika hata baada ya kulengwa na shutuma hizo za mauaji. Kilichomsikitisha yeye ni kule kutajwa kuwa ameuawa wakati si kweli.
Ilipofika jioni nikakumbuka kwamba sikuwa na nguo za kubadili. Nguo nilizokuwa nimevaa zilikuwa zimeshachafuka na nilikuwa nikizivaa hizo hizo.
Nikamwambia Edda.
“Nataka nikutume nyumbani kwangu.”
“Unitume nini?”
“Ukanichukulie nguo zangu.”
“Mmh…!”
“Unaweza kwenda kunichukulia tu. Nitakupa funguo.”
“Huko nyumbani kwako nitakujua kweli?”
“Utapelekwa na bodaboda. Nitamwelekeza nyumba ninayoishi.”
“Si nitaulizwa mimi ni nani ninayefungua chumba cha watu?”
“Hakuna atakayekuuliza. Pale tuko wapangaji watupu. Na kila mpangaji ana sehemu yake ya vyumba viwili, choo chake na jiko lake. Tunachangia mlango tu wa kuingilia na ua ni mmoja.”
“Kwa hiyo nikionekana ninafungua mlango wako, sitaulizwa na mtu yeyote?”
“Hata kama mtu atakuuliza utamwambia nimekutuma. Sasa kama kuna ujumbe wowote watakwambia.”
“Nikishaingia humo chumbani nifungue kabati?”
“Fungua kabati unichukulie suruali mbili na mashati mawili. Utakuta begi dogo nimelitundika, utalichukua unitilie hizo nguo kisha uniletee.”
“Sawa, nitakwenda.”
“Nenda sasa hivi. Muite mwenye bodaboda nimpe maelekezo.”
Edda, msichana mpole na mcheshi, akanitazama. Mara nyingi anaponitazama ninaona kama anatabasamu, lakini hatabasamu. Hivyo ndivyo anavyoonekana. Usipomgundua, na wewe unaweza kutabasamu ukidhani mnatabasamu nyote.
Nilipomwona anatabasamu nilijua ilikuwa ni kawaida ya uso wake. Akainuka na kutoka.
Baadaye kidogo nikasikia pikipiki ya bodaboda ikisimama barazani. Nikatoka mle chumbani na kwenda barazani. Nikamkuta Edda yuko mlangoni huku pikipiki ikiwa pembeni mwa baraza la nyumba.
“Nimeshakuja naye, mwelekeze niende naye mara moja,” Edda akaniambia.