KISIWA CHA MAUTI - 9
ILIPOISHIA
Niliendelea kujiuliza, kama niliyemuua alikuwa msichana mwingine, mbona taarifa nilizoziona kwenye blogy zinaonesha kuwa aliyeuawa alikuwa Edda!
Hapo nilishindwa kupata jibu. Nikajiambia ni vizuri Edda atakaporudi niendelee kumdadisi. Huenda nikagundua yule msichanna alikuwa nani.
Lakini pia nilijiuliza, kwanini Edda hakuwa na habari ya tukio lilotokea hapo hoteli ambako anafanya kazi? Hata kama si yeye niliyemuua, kwanini asijue kilichotokea?
SASA ENDELEA...
Nikaendelea kujiuliza, alikuwa hajui kwa sababu siku ile hakwenda kazini? Kwa nini asipigiwe hata simu na mfanyakazi mwenzake na kujulishwa kilichotokea?
Maswali yangu mengi yalikosa majibu akilini mwangu. Nikaendelea kujiambia huenda Edda atakuwa na majibu ya baadhi ya maswali hayo.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, niliogopa kumdadisi Edda maswali mengi kwa sababu mwenyewe alionekana kutojua lolote. Niliona endapo nitamdadisi anaweza kupata hofu na kupiga simu kuulizia kilichotokea na hivyo kuniweka katika hatari ya kukamatwa.
Nilikuwa sitaki ijulikane kama nilikuwa nimejificha nyumbani kwa msichana huyo, na pia sikutaka msichana huyo ajue kuwa niliamua kubaki kwake ili kujihifadhi kabla ya kupata uamuzi mwingine.
Ilipita nusu saa tu, msichana akarudi. Alikuwa amenunua ndizi, samaki na viungo vingine.
Akaniambia atakuwa jikoni kwa muda.
Edda aliniacha chumbani mwake kwa karibu saa mbili. Mara moja moja alikuwa akija chumbani na kukaa kwa muda, kisha anarudi jikoni.
Mpaka ilipofika saa saba, ndizi na samaki wa kukaangwa vikawa tayari.
“Ungependa upate na chai ya kusukumia?” Edda akaniuliza wakati akipanga sahani kwenye meza yake ndogo.
Kwa vile sikuwa nimekunywa chai asubuhi, nikamwambia:
“Kama chai ipo, niwekee.”
“Ipo kwenye chupa, lakini ni ya rangi.”
“Ndiyo ninayoitaka.”
Edda akaongeza vikombe viwili juu ya meza. Akachukua chupa ya chai na kumimina chai kwenye vikombe.
“Sukari utaweka mwenyewe.”
“Sukari yangu huiwezi. Niseme kwamba mimi hula asali, si chai. Napenda sukari sana.”
“Inaweza kuja kukudhuru.”
“Nitafanyaje wakati naipenda, au niseme napenda vitu vitamu sana?”
Edda akacheka.
“Vitamu vinaua.”
“Hata nzi anasema akifa kidondani ni sawa. Panampa ladha kama mimi sukari inavyonipa ladha.”
“Karibu chakula. Mazungumzo baadaye,” Edda akaniambia.
Tukawa tunakula huku tunazungumza. Ingawa sikuenda hapo kwa Edda kwa ajili ya mapenzi, nilijisikia kumpenda sana. Tuliongea mengi mpaka tukakubaliana kwamba nilale pale kwake.
Akaniambia kwamba hataingia kazini asubuhi, bali ana zamu ya kuingia mchana, yaani siku iliyofuata.
Baada ya chakula tuliendelea na mazungumzo. Hapo ndipo nilipolirudisha lile suala la kule hotelini.
“Nilisikia kwamba kuna mfanyakazi mwenzenu aliyeuawa pale hotelini, ni kweli?” nikamuuliza.
“Ni nani?”
“Sikupata jina lake, lakini ni habari ya uhakika.”
“Aliuawa na nani?”
“Nilisikia kuna mteja wenu alikuja pale, akalewa sana kisha akakodi chumba. Inasemekana alitaka kumbaka yule msichana aliyekuwa akimhudumia mle chumbani. Mwisho akamuua na kutoroka.”
“Sijasikia habari hizo. Hilo tukio limetokea lini?”
“Nimeambiwa limetokea jana usiku.”
“Mimi sikuenda kazini leo. Lakini kama kungetokea tukio kama hilo, ningearifiwa na wenzangu.”
“Labda watakuarifu baadaye.”
“Labda.”
“Kwani jana uliondoka saa ngapi?”
“Niliondoka saa kumi na mbili jioni. Nikakuacha na mwenzangu aendelee kukuhudumia.”
“Nakumbuka kama nilikodi chumba pale pale.”
“Chumba cha nini?”
“Cha kujipumzisha.”
“Kama ulikodi chumba, ilikuwa ni baada ya mimi kuondoka. Nilikuacha ukiwa umelewa sana.”
“Nilikunywa chupa ngapi?”
“Ni kichwa chako tu chepesi. Ulikunywa bia chache sana. Sikumbuki ni ngapi, labda kama huyo mwenzangu alikuongezea zaidi.”
Hapo nikapata picha kwamba hadi Edda anaondoka pale hotelini saa kumi na mbili jioni, sikuwa nimekodi chumba na aliniacha nikiwa na mhudumu mwenzake aliyeendelea kunihudumia.
“Huyo mhudumu uliyemuacha anihudumie anaitwa nani?”
“Anaitwa Edda kama mimi. Pale tuko Edda wawili.”
Nikajua niliyemuua alikuwa Edda mwingine!
Nikayaacha hapo yale mazungumzo na kuanzisha mazungumzo mengine. Tukiwa katikati ya mazungumzo yetu, Edda akaniambia:
“Nakwenda kuosha vile vyombo tulivyokulia chakula.”
Akaniacha peke yangu. Kumbe na mimi nikapitiwa na usingizi hapo hapo. Nikalala fofofo.
Nilipokuja kuzinduka, nikamuona Edda naye alikuwa amelala kitandani. Sikumuamsha. Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa kumi jioni.
Nikataka niwashe simu yangu ili niingie katika blogu yoyote nione kama nitakuta habari nyingine inayonihusu, lakini niliogopa kuwasha simu.
Nilihisi nikiwasha simu, polisi au mhariri wangu wanaweza kunipigia au nikakuta meseji zao, jambo ambalo sikutaka litokee.
Edda aliamka saa kumi na moja, akaenda msalani kisha akarudi.
“Nilikukuta umepitiwa na usingizi na mimi nikalala,” akaniambia.
“Nilijishitukia tu nimepitiwa na usingizi. Si unajua, shibe mwana malevya, njaa mwana malegeza.”
Edda akacheka. Nikaendelea kumwambia:
“Ukilala kwa sababu umeshiba ni kwamba umelewa, lakini ukilala kwa sababu una njaa ni kwamba umelegea.”
“Kwa hiyo wewe umelala kwa sababu ulishiba?”
“Nilishiba sana na nakushukuru sana.”
“Asante.”
Nilikuwa najaribu kujichangamsha kwa maneno ya kusisimua ili Edda asigundue kuwa nilikuwa nina jambo zito moyoni mwangu. Na mpaka muda ule, licha ya kumuuliza maswali mengi, alikuwa hajajua kilichotokea.
Tukaendelea kuzungumza hadi saa mbili usiku, ambapo alikwenda kuoga kisha akaniambia niende nikaoge. Alinipeleka hadi bafuni akanipa taulo.
Niliporudi kuoga, nilivaa nguo zangu zile zile. Nikamwambia tutoke tutafute hoteli yenye chakula kizuri iliyo karibu, tule halafu turudi.
Hata hivyo, sikutaka tutoke na pikipiki. Edda akanifungulia mlango wa nyuma, nikaiingiza ile pikipiki na kuiegesha karibu na ukuta.
Tulikwenda kula chakula katika hoteli moja iliyokuwa mtaa wa tatu kutoka mtaa ule aliokuwa akiishi Edda.
Baada ya kula chakula, nilimnunulia Edda bia mbili. Mimi sikutaka kunywa hata bia moja.
Tuliporudi nyumbani tukalala.
Asubuhi kulipokucha, mimi ndiye niliyemuamsha Edda. Akaniambia nitangulie kwenda kuoga. Nikaenda. Niliporudi, akaenda yeye.
Wakati anataka kwenda kununua mikate ili aje achemshe chai, nikampa pesa aninunulie magazeti mawili ya kila siku, likiwemo gazeti la Kumekucha.
Baada ya muda kidogo, Edda akarudi akiwa ametaharuki.
“Mbona katika haya magazeti wameandika nimeuawa? Mimi ndiye Edda Ibrahim!” akaniambia kwa mshutuko.
“Wameandika hivyo?” nikajidai kumuuliza wakati nilishajua fika kwamba lazima habari hiyo ingeandikwa.
Edda akanipa gazeti moja. Jingine akabaki nalo. Gazeti alilonipa lilikuwa la kila siku, lakini halikuwa gazeti letu la Kumekucha.
Stori iliyoandikwa kwenye ukurasa wa mbele ilikuwa na kichwa kilichosema:
MWANDISHI ADAIWA KUUA!
Stori hiyo iliwekewa vichwa vidogo viwili. Kimoja kilisema:
“Mauaji yamefanyika katika chumba cha hoteli Masaki.”
Kichwa kidogo kingine kilisomeka:
“Aliyeuawa ni mfanyakazi wa hoteli hiyo aliyetambulika kwa jina la Edda Ibrahim.”
Nikaanza kuisoma ile habari ambayo maelezo yake yalimkariri Kamanda wa Polisi pamoja na Meneja wa hoteli hiyo.
Habari iliandikwa kwamba nilifika pale hotelini na kumuulizia bosi wa hoteli ile. Nilipoambiwa bosi hakuwepo, nilianza kuagiza bia. Habari iliendelea kueleza kuwa nilipojiona nimelewa, nilikodi chumba hapo hapo hotelini ambapo nilimuagiza msichana aliyekuwa akinihudumia aniletee bia chumbani.
Habari zikaendelea kueleza kuwa tukiwa humo chumbani nilimtaka kimapenzi msichana huyo, lakini alipokataa nilianza kumpiga hadi kumuua, kisha nikatoroka wakati wa asubuhi.
Habari zilimalizia kueleza kuwa polisi walikuwa katika msako mkali wa kunitafuta.
“Hebu lete na gazeti hilo,” nikamwambia Edda baada ya kumaliza kuisoma ile habari.
“Umeona walivyoniandika? Edda Ibrahim ni mimi,” Edda akaniambia.
Wakati ananipa lile gazeti aliniambia:
“Ni habari ya uongo.”
Sikumjibu kitu. Nililishika gazeti hilo la pili ambalo ni la kampuni niliyokuwa ninafanya kazi.
Habari kama ile niliyoisoma ndiyo iliyokuwa katika ukurasa wa mbele. Mwandishi alikuwa ni mhariri wangu.
Habari hiyo ilikuwa na kichwa kilichosema:
NI MAUAJI YA UTATA
Mhariri wangu aliandika habari ile kwa mtazamo tofauti, akiwataka polisi kufanya uchunguzi wa kina. Mhariri wangu alisema mwandishi wao alikwenda kikazi hotelini hapo.