Zuchu, Nandy kuna mahali wanapimana
Muktasari:
- Oktoba 2026, TanzaniaCharts ilitoa takwimu za wasanii waliofanya vizuri, zikionyesha Zuchu akiongoza kwa watazamaji milioni 37, huku Nandy akiwa na milioni saba.
KATIKA muziki wa Bongo Fleva kumekuwa na ushindani wa wasanii mbalimbali. Hili si jambo geni, kwani miaka ya nyuma tulishuhudia ushindani wa Inspector Haroun na Juma Nature, Zay B na Sister P, P Funk na Master J, baadaye Alikiba na Diamond Platnumz.
Ushindani huo umesaidia kuwakuza wasanii kimuziki, kuongeza mashabiki na kipato, huku wengine wakipanua soko lao nje ya nchi.
Sasa, katika gemu inayozidi kupanuka, ushindani mwingine umeibuka kati ya mastaa wa kike Nandy na Zuchu, ambao kazi zao zimekuwa zikigawa mashabiki.
Oktoba 2026, TanzaniaCharts ilitoa takwimu za wasanii waliofanya vizuri, zikionyesha Zuchu akiongoza kwa watazamaji milioni 37, huku Nandy akiwa na milioni saba.
Takwimu hizo zilipingwa na Nandy kupitia Instagram, akimtaka aliyechapisha taarifa hizo aache kutumia jina lake katika takwimu alizodai si sahihi.
Hapa Mwanaspoti linakuchambulia ushindani wa wawili hawa kupitia shoo, tuzo, chati za muziki na nini wadau wanasema kutokana na ushindani wa wasanii, kipi kinastahili kuonyesha ubora wao.
SHOO ZAO
Mwaka 2016, Nandy aliiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Tecno Own The Stage, Nigeria na kushika nafasi ya pili. Mwaka 2017 alishiriki Coke Studio Africa jijini Nairobi, Kenya, kabla ya kutumbuiza kwe nye kipi ndi cha 10 Over 10 cha Citizen TV akiwa na Willy Paul.
Mwaka 2019 alishiriki One Africa Music Fest, Dubai. Pia ameendelea kufanya shoo katika tamasha lake la Nandy Festival lililoanzishwa mwaka huohuo na kuzunguka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Zuchu, mwaka 2021 na 2022 alishiriki Africa Day Concert na AFRIMMA, Marekani. Mwaka 2022 alitumbuiza AFRIMA nchini Nigeria.
Mwaka 2023 alifanya shoo kubwa Comoro na kurejea tena mwaka 2024. Novemba mwaka huohuo alitumbuiza Festival de Mayotte, kabla ya Desemba kushiriki Furaha City Festival jijini Nairobi, Kenya.
Agosti 30, 2025 alishiriki sherehe za kufunga CHAN jijini Nairobi, pamoja na Mwananchi Day ya mwaka huohuo.
TUZO ZAO
Nandy amejizolea tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mwaka 2017 na 2020 alitwaa tuzo za Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki katika AFRIMA. Mwaka 2018 alishinda Maranatha Awards, Kenya, kupitia wimbo Nikumbushe Wema Wako.
Mwaka 2019 na 2020 alitwaa tuzo za African Entertainment Awards USA, huku mwaka 2022 akishinda AFRIMMA jijini Dallas, Marekani. Nyumbani, mwaka 2022 alibeba tuzo mbili za TMA, zikiwemo Msanii Bora wa Kike na People’s Choice. Mwaka 2025 alishinda Best Female Artist Tanzania katika Trace Awards.
Kwa upande wa Zuchu, mwaka 2020 alishinda Emerging Artist katika AFRIMMA, kabla ya kutwaa tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki mwaka 2022.
Katika TMA za 2023 alibeba vikombe vitano, vikiwemo Msanii Bora wa Kike Bongo Fleva na Video Bora kupitia wimbo Mwambieni. Mwaka 2025 alishinda Best Female Artiste of the Year katika Africa Golden Awards na Zanzibar Award za Trace Awards.
Pia alipata YouTube Silver Play Button mwaka 2020 na Gold Play Button mwaka 2021 baada ya kufikisha wafuasi milioni moja.
CHATI ZAO
Takwimu za majukwaa ya utiririshaji muziki zinaonyesha Zuchu akiongoza katika majukwaa kadhaa, huku Nandy akifuatia.
Kwenye Spotify, Zuchu anashika nafasi ya kwanza kwa wasanii wa kike Tanzania akiwa na wasikilizaji 357,400 kwa mwezi, huku Nandy akiwa nafasi ya pili na 217,200, kwa takwimu za Novemba 2026.
Audiomack, Zuchu anaongoza akiwa na wasikilizaji 396,000 kwa mwezi, huku Nandy akitajwa nafasi ya pili kwa streams.
Boomplay, Zuchu aliingia nafasi ya tano kwa wasanii wote waliokusanya streams nyingi Septemba 2026, akiwa na milioni 12, huku jumla ya streams zake za muda wote ikivuka milioni 465. Nandy anashika nafasi ya 371 kwa takwimu za muda wote.
Apple Music, Zuchu aliwahi kufikisha nafasi ya kwanza kupitia Mvua Ya Baraka, huku Nandy akiingia nafasi ya 16 hadi 19 kupitia Malaika.
Kwa upande wa Audiomack, takwimu za akaunti zao zinaonyesha Zuchu akiwa na plays milioni 109.4 na followers zaidi ya 727,000, huku Nandy akiwa na plays milioni 57 na followers zaidi ya 382,000.
Akizungumza na Mwanaspoti, mtayarishaji wa muziki Master J amesema ukubwa wa msanii haupaswi kupimwa kwa takwimu za mitandao pekee, bali pia mauzo ya kazi zake na idadi ya shoo anazopata. Kwa mtazamo wangu, ukubwa wa msanii unapimwa kwa mauzo yake na idadi ya shoo anazopata.
“Kuna wasanii wanatoa nyimbo nyingi, lakini hawana mauzo makubwa wala hawaongozi kwenye mitandao ya kijamii” amesema Master J.
Kwa upande wake, meneja wa Gogumama Music, Dollar Losa, amesema kuwa na namba nyingi YouTube hakutoshi kuthibitisha mafanikio ya msanii. “Msanii aliyefanikiwa hapimwi kwa namba za YouTube, huwezi kumpima kwa mtandao mmoja,” amesema.
Hata hivyo, amesema Zuchu anaonekana kuwa mbele ya Nandy katika maeneo mengi ya muziki, ikiwemo majukwaa ya kidijitali na mapokezi ya nyimbo zao.
Ameongeza wote wanapaswa kupongezwa kwa kufanya vizuri na ushindani wao uwe wa kibiashara, ukiwapa hamasa ya kufikia mafanikio makubwa badala ya kuwafanya maadui.