Zuchu anavyotikisa mitandao Bongo
Muktasari:
- Safari hii, staa huyo ameongeza jambo jingine kwenye rekodi yake baada ya wimbo wake mpya, “Kucheza Unajua”, kuanza kufanya vizuri ndani na nje ya YouTube.
KAMA kuna jambo ambalo msanii Zuhura Othman ‘Zuchu’ amekuwa akifanya vizuri tangu alipoingia kwenye muziki, ni kutumia nguvu ya mashabiki wake mitandaoni kusukuma kazi zake.
Safari hii, staa huyo ameongeza jambo jingine kwenye rekodi yake baada ya wimbo wake mpya, “Kucheza Unajua”, kuanza kufanya vizuri ndani na nje ya YouTube.
Zuchu ni miongoni mwa wasanii wa kike wenye wafuasi wengi zaidi Tanzania kwenye mtandao wa Instagram, akiwa na zaidi ya wafuasi milioni 7.5. Idadi hiyo inampa nguvu kubwa kila anapotoa kazi mpya, kwani ujumbe wake unaweza kuwafikia mamilioni ya watu kwa muda mfupi. Sasa amekuja na “Kucheza Unajua”, wimbo aliomshirikisha DeSmile, ambao umeanza kufanya vizuri kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki mbalimbali wakishiriki katika dance challenge kupitia majukwaa kama TikTok.
Tofauti na baadhi ya kazi zake zilizotangulia, safari hii Zuchu ameonyesha upande mwingine wa muziki wake kwa kuingia kwenye mdundo wa Singeli, aina ya muziki inayokwenda sambamba na kasi, dansi na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii.
KUCHEZA UNAJUA
Ndani ya muda mfupi tangu kuanza kusambaa, “Kucheza Unajua” imeanza kuonyesha dalili za kuwa miongoni mwa nyimbo zinazozungumzwa zaidi mitandaoni.
Video ya dansi ya wimbo huo imekusanya zaidi ya views milioni 1.5 ndani ya siku nne, huku pia ikifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye orodha ya YouTube Trending Tanzania.
Hilo limekuwa jambo muhimu kwa Zuchu, kwa sababu katika zama hizi mafanikio ya wimbo hayapimwi kwa idadi ya usikilizaji pekee, bali pia namna unavyoweza kuingia katika maisha ya mashabiki kupitia video, mitandao ya kijamii na changamoto mbalimbali.
Kwa upande wa “Kucheza Unajua”, hilo limeanza kuonekana kupitia dance challenge iliyoibuka mitandaoni, huku mashabiki wakitengeneza video zao wakitumia wimbo huo.
NGUVU YA WAFUASI
Kwa Zuchu, matumizi ya mitandao ya kijamii si jambo jipya. Tangu aanze kujenga jina lake kwenye muziki, amekuwa akitumia majukwaa kama Instagram na YouTube kuwasiliana na mashabiki na kusukuma kazi zake.
Akiwa na zaidi ya wafuasi milioni 7.5 Instagram, kila hatua yake kwenye muziki ina uwezo wa kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi.
Hii ndiyo sababu kila anapotoa wimbo mpya, macho ya mashabiki na wadau wa muziki hugeukia namna kazi hiyo itakavyopokelewa kwenye majukwaa ya kidijitali.
Kwa “Kucheza Unajua”, Zuchu anaonekana kutumia nguvu hiyo kuunganisha muziki na dansi, jambo ambalo limeifanya kazi hiyo kupata nafasi ya kuzungumzwa zaidi mitandaoni.
SINGELI YAMPA SURA MPYA
Uamuzi wa Zuchu kuingia kwenye Singeli nao umeongeza mvuto wa wimbo huo. Mdundo huo una kasi na nafasi kubwa ya kuambatana na dansi, hivyo kuufanya uwe rahisi kutumiwa kwenye video fupi za mitandao ya kijamii.
Ushirikiano wake na DeSmile nao umeongeza ladha nyingine kwenye wimbo huo, huku Zuchu akionyesha kuwa bado anaweza kujaribu mitindo tofauti ya muziki bila kuachana na kile ambacho mashabiki wake wanakifahamu kwake.
NGUVU YA DIGITALI
Kwa miaka ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu katika mafanikio ya wasanii, hasa katika kizazi ambacho mashabiki hutumia YouTube, Instagram na TikTok kugundua na kusambaza muziki mpya
Zuchu ni miongoni mwa wasanii wa kike Tanzania ambao wamejenga msingi mkubwa kwenye majukwaa hayo.
Mafanikio ya “Kucheza Unajua” yanaonyesha tena namna jina lake lilivyo na nguvu kwenye soko la kidijitali, huku nafasi ya pili kwenye YouTube Trending Tanzania ikiwa ishara nyingine ya mwitikio wa mashabiki.