Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Singeli 'kichaka' kinachompa maisha D Voice

Muktasari:

  • Kabla ya D Voice kutambulishwa WCB Wasafi mwaka 2023, mwanamuziki huyo alikuwa akifanya Singeli kwa asilimia 100 ila kwa sasa imeshuka hadi asilimia 20 ila bado anajinasibisha na Singeli.

KILA mara D Voice anajitambulisha kama mwanamuziki wa Singeli lakini mtindo wake wa kufanya aina hiyo muziki tangu alipojiunga na lebo ya WCB Wasafi unaacha maswali na hata kumtenga na Ufalme wa Singeli ambao amejivika.

Kabla ya D Voice kutambulishwa WCB Wasafi mwaka 2023, mwanamuziki huyo alikuwa akifanya Singeli kwa asilimia 100 ila kwa sasa imeshuka hadi asilimia 20 ila bado anajinasibisha na Singeli.

D Voice kwa mara ya kwanza alivuma zaidi kupitia Singeli baada ya kuachia wimbo wake, Kuachana Shingapi (2021), ambao remix yake aliwashirikisha Barnaba, Lody Music na Platform.

Hivi karibuni WCB Wasafi ilitaja rekodi za D Voice ambazo ameweka katika muziki wa Singeli, rekodi ambazo tunaweza kusema ndicho kimekuwa kichaka cha kujifichia baada ya kuona namba hazimbebi katika Bongofleva.

Rekodi anazotajwa kuziweka ni hizi - msanii wa namba moja wa Singeli mwenye wafuatiliaji (subscribers) wengi YouTube, na msanii namba moja wa Singeli ambaye nyimbo zake zimesikilizwa au kutazamwa mara nyingi zaidi (most streamed) katika majukwaa yote ya kidijitali kama Boomplay na YouTube.

Lakini ukianza kuzifuatilia rekodi hizi, utabaini kuwa D Voice na WCB Wasafi wameamua tu kujipakulia minyama kwa sababu D Voice hana sifa za kutosha kwa sasa kujiweka katika kipengele cha mwanamuziki wa Singeli.

Kwa mfano, hadi sasa ndani ya mwaka huu wa 2026, D Voice ameachia nyimbo tano - Ningepata Nafasi, Baridi akimshirikisha Zuchu, Iyo akiwa na Diamond, Kumbe, na Banana akimshirikisha Jay Melody.

Kati ya nyimbo hizo tano, ni mmoja tu (Iyo) ndio wa Singeli, hizo nyingine nne ni za Bongofleva, kwa hiyo kimahesabu hadi sasa kwa mwaka huu D Voice ametoa muziki wa Singeli kwa asilimia 20 tu!.

Yaani tangu Januari hadi Septemba, D Voice ametoa wimbo mmoja tu Singeli na nyingine nne za Bongofleva, sasa kwanini ajitambulishe kama mwanamuziki wa Singeli na si Bongofleva?.

Yaani Dulla Makabila ambaye kwa mwaka huu tayari ameachia nyimbo nne za Singeli akae kundi moja na D Voice?. Si kwamba anaitumia historia yake ya huko nyuma kujivika ufalme ambao hastahili?.

D Voice na WCB Wasafi, anapojitaja kama msanii namba moja wa Singeli anayefanya vizuri mtandaoni hasa YouTube, ni kutaka tu kupora Ufalme wa kina Dulla Makabila kwa nguvu.

Nadhani D Voice hana nyimbo za Singeli za kumuweka juu ya Dulla Makabila, ila anachofanya ni kuchukua namba alizopata kwenye Bongofleva na kuleta kwenye Singeli.

Kwa mfano, albamu ya D Voice, Swahili Kid (2023) ambayo alitambulishwa nayo na WCB Wasafi, ina nyimbo 10, kati ya hizo za Singeli ni nne, sawa na asilimia 40, hizo asilimia 60 zilizosalia ni Bongofleva na Amapiano.

Na nyimbo zilizofanya vizuri zaidi katika albamu hiyo ni zile za Bongofleva hasa zile ambazo amemshirikisha Zuchu na Mbosso. Wimbo uliofanya vizuri zaidi katika albamu hiyo ni BamBam akimshirikisha Zuchu ambao video yake imetazamwa (views) YouTube mara milioni  25.

Hadi sasa, wimbo wa D Voice uliofanya vizuri zaidi YouTube ni Tunapendana (2024) akimshirikisha Mbosso, wimbo huu wa Bongofleva umetazamwa mara milioni 38. Na wimbo wa Singeli uliofanya vizuri YouTube ni Kuachana Shingapi (2021) uliotazamwa mara milioni 2.4.

Na kumbuka wimbo huo wa Singeli ulitoka kabla ya kujiunga na WCB Wasafi, hivyo licha ya kumshirikisha Diamond katika nyimbo mbili za Singeli lakini bado ameshindwa kupata wimbo mkubwa kama huo!.

Kwa ujumla, nyimbo za D Voice zilizotazamwa zaidi YouTube, kuanzia namba 1 hadi 11, zote ni za Bongofleva zikimpatia 'views' zaidi ya milioni 148.7. Wakati ukichukua nyimbo zake zote za Singeli, hazifikishi hata 'views' milioni 10.

Hadi hapo kwanini D Voice asiwe msanii wa Bongofleva?, kwanini anang'ang'ania Singeli ndio iwe utambulisho wake?. Jibu rahisi ni kwamba amechagua Singeli kuwa kichaka chake, kichaka cha kuchota Ufalme ambao anajua hawezi kuupata katika Bongofleva.