Prime
WCB Wasafi walivyonogewa na Amapiano!
Kwa miaka minne sasa muziki wa Amapiano unazidi kuchukua nafasi kubwa katika Bongofleva, huku wasanii WCB Wasafi wakiamua kwenda sambamba na upepo huo mithili ya samaki na maji, inaonekana ni biashara nzuri kwao wakati huu.
Tangu mwaka huu umeanza tayari wasanii watatu wa WCB Wasafi wametoa nyimbo nne za Amapiano na kufikisha jumla ya nyimbo 11 za Amapiano tangu mwaka 2021, huku Focalistic, Costa Titch na wasanii wengine wa Afrika Kusini wakishirikishwa zaidi.
Amapiano ni aina mpya ya muziki iliyoibuka kutoka nchini Afrika Kusini mapema miaka ya 2010 ukiwa na vionjo vya aina nyingine za muziki kama Deep House, Jazz, Kwaito, Afrobeat n.k.
Inaelezwa kuwa muziki wa Amapiano ulianza Gauteng ila kumekuwepo na mvutano ni wapi hasa asili ya muziki huo nchini humo, wapo wengine wanaodai ulianzia katika vitongoji vya Johannesburg.
Staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa rekodi lebo ya WCB Wasafi, ni miongoni wa wasanii wanaohusudi sana aina hiyo ya muziki hasa kwa upande wa biashara kutokana unazidi kuwa na mashabiki wengi kila siku.
Utakumbuka wimbo wa kwanza wa Diamond wenye mahadhi ya Amapiano 'IYO ulitoka Julai 2021 huku wakiwashirikisha wakali wa muziki huo kutokea Afrika Kusini, Focalistic, Mapara A Jazz na Ntosh Gazi.
Hiyo ni baada ya Marioo kufanya vizuri na wimbo wake wa Amapiano, Mama Amina (2020) ambao aliwashirikisha Shomadjozi na Bontle Smith wa Afrika Kusini, hadi sasa 'Mama Amina' inatajwa kama 'Swahili Amapiano' bora kuwahi kutokea.
Kufanya vizuri kwa wimbo huo ndipo hasa kuliwaamsha wasanii wengine wa Bongofleva kufanya Amapiano, miongoni mwao ni Diamond, Harmonize, Rayvanny, Zuchu, Ommy Dimpoz, Mbosso, Nandy, Jux n.k.
Baada ya Diamond kufanya vizuri na 'IYO' alikuja kutoa wimbo mwingine wa Amapiano, Fresh (2022) akiwapa shavu Focalistic, Costa Titch na Pabi Cooper, wote kutoka Afrika Kusini, huu ulitoka katika EP yake ya kwanza, First of All (FOA).
Akitangaza ujio wake mpoya mwishoni wa Juni, Diamond alidai mpango wake ni kutawala soko la muziki Tanzania na Afrika hadi Januari 2024, safari yake hii ikaanza kwa kuachia ngoma ya Amapiano, SHU akiwa na Chley Nkosi wa Afrika Kusini tena.
Hivyo utabaini kuwa kila mwaka Diamond ni lazima atoa wimbo mmoja wa Amapiano, ameweza kufanya hivyo tangu mwaka 2021 hadi 2023 ambapo ameachia IYO, Fresh na SHU.
Wasanii wake wa WCB Wasafi nao hawapo nyuma katika kuachia ngoma za Amapiano, kuanzia Mbosso, Zuchu, Lava Lava na Rayvanny ambaye aliachana na lebo hiyo tangu Julai 2022.
Rayvanny ndiye alikuwa msanii wa kwanza WCB Wasafi kuimba Amapiano alipoachia wimbo, Woza (2021) akimshirkisha Diamond, hata baada ya kuondoka WCB alifanya ngoma nyingine ya Amapiano na Diamond, Nitongoze ambayo ilishinda Tuzo za Muziki Tanznaia (TMA) 2022 kama Wimbo Bora wa kushirikiana.
Akiwa na mwaka mmoja WCB Wasafi, Desemba 2021 Zuchu naye akatoa ngoma yake ya Amapiano, 'Kitu' huku akiwashirikisha Bontle Smith na Tyler ICU wa Afrika Kusini, na hadi sasa Zuchu hajatoa wimbo mwingine wa Amapiano.
Ndipo kijiti cha Amapiano kikahamia kwa Mbosso ambaye tunaweza kumuita Mfalme wa Amapiano pale WCB Wasafi, alianza na ngoma, Moyo (2022) akiwa na Costa Titch na Phantom Steeze wa Afrika Kusini.
Alipoachia EP yake ya kwanza, Khan (2022) yenye nyimbo sita, mbili kati ya hizo zilikuwa za Amapiano ambazo ni 'Yataniua' akimshirkisha Diamond na 'Shetani' akiwashirikisha Costa Titch na Alfa Kat wa Afrika Kusini kwa mara ngingine tena!.
Na sasa Mbosso anafanya vizuri na wimbo mpya wa Amapiano, 'Sitaki' ambao umetoka hivi karibuni, hiyo ni sawa na Lava Lava ambaye naye ametoa ngoma mbili za Amapiano kwa kufuatata. Alianza na 'Tajiri' na baada ya wiki mbili tu, amekuja na 'Tuna Kikao' akiwa na Diamond, huu ndio unafanya vizuri kwa sasa.
Nyimbo hizi 11 za Amapiano zilizotolewa na WCB Wasafi zinatosha kabisa albamu kama wangeamua kufanya hivyo, ndiyo, albamu ya nyimbo 11 tu, mbona albamu ya pili ya Diamond, Lala Salama (2012) ilikuwa nyimbo 10!.
Hata hivyo, bado hawajafanikiwa kuwa na ushawishi mkubwa kupitia Amapiano nje ya Tanzania, sio WCB Wasafi tu, hata wasanii wote wa Bongofleva wanaofanya aina hiyo ya muziki.
Mathalani hakuna aliyepata nafasi katika tuzo za Amapiano 2023 nchini Afrika Kusini ambapo vipengele zaidi ya 25 viliwaniwa!, kipengele ambacho wasanii wa Bongofleva na nchi ningine walitazamiwa kuwepo ni cha 'Friends of Amapiano', ila ni wasanii wa Nigeria tu ndio waliopenya ambao ni Asake, Davido na Wizkid tu!.