Waziri Riziki Pembe amtaja Diamond akitoa wazo jipya kwa TaSuBa
Muktasari:
- Dk Pembe ametoa wazo hilo leo Novemba 16, 2026 kwenye ukumbi wa chuo cha TaSuBa Bagamoyo, ambapo amesema mfumo huo unaweza kuwasaidia wasanii wenye majukumu mengi ambao wangependa kupata sifa na ujuzi wa kitaaluma, lakini wanashindwa kuhudhuria mafunzo ya darasani kutokana na shughuli zao.
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Riziki Pembe Juma, ameitaka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kufikiria kuanzisha mafunzo ya sanaa kwa njia ya mtandao ili kutoa fursa kwa wasanii wakubwa kupata elimu na ujuzi bila kulazimika kufika chuoni ana kwa ana.
Dk Pembe ametoa wazo hilo leo Novemba 16, 2026 kwenye ukumbi wa chuo cha TaSuBa Bagamoyo, ambapo amesema mfumo huo unaweza kuwasaidia wasanii wenye majukumu mengi ambao wangependa kupata sifa na ujuzi wa kitaaluma, lakini wanashindwa kuhudhuria mafunzo ya darasani kutokana na shughuli zao.
Akifafanua hoja yake, waziri huyo amemtaja mwanamuziki maarufu nchini, Diamond Platnumz, kama mfano wa msanii ambaye angeweza kutamani kujiunga na mafunzo hayo, lakini uwepo wake chuoni ungeweza kugeuza umakini wa wanafunzi kutoka kwenye masomo na kuelekezwa kwake.
“Kwa mfano tuchukulie hapa anakuja Diamond kujifunza. Watu watasoma kweli? Hatutasoma. Watakuja kila wakati wanataka kwenda kumwangalia Diamond,” amesema Dk Pembe.
Ameongeza kuwa, hali hiyo inaweza kuwafanya wanafunzi wengi kuwa na shauku ya kumuona msanii huyo badala ya kuzingatia kile kinachofundishwa darasani.
Kutokana na hali hiyo, ameshauri TaSUBa kuangalia uwezekano wa kutumia teknolojia ya mtandao kurahisisha upatikanaji wa mafunzo, hasa kwa wasanii ambao hawawezi kuhudhuria masomo kwa njia ya ana kwa ana.
Katika maelezo yake, Dk Pembe pia amegusia umuhimu wa teknolojia mpya ikiwemo Akili Unde (AI), akieleza inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa watumiaji wenye ujuzi wa kuitumia, lakini pia inaweza kuwapotosha wale wasioielewa vizuri.