Wasanii watano maarufu waliowahi kulala sero
Muktasari:
- Baadhi ya matukio hayo yalizua mijadala mikubwa wakati yakitokea, huku majina ya wasanii hao yakitawala vichwa vya habari na mitandao ya kijamii. Miaka inapopita, si rahisi kwa kila shabiki kukumbuka mazingira na sababu zilizowafanya mastaa hao kujikuta nyuma ya nondo.
UMAARUFU wa mastaa huwafanya kuwa gumzo kutokana na kazi zao za muziki, filamu na maisha yao binafsi. Hata hivyo, nyuma ya majukwaa na mwanga wa kamera, baadhi yao wamewahi kukumbana na misukosuko ya kisheria iliyowafikisha mikononi mwa polisi na wengine kulala mahabusu.
Baadhi ya matukio hayo yalizua mijadala mikubwa wakati yakitokea, huku majina ya wasanii hao yakitawala vichwa vya habari na mitandao ya kijamii. Miaka inapopita, si rahisi kwa kila shabiki kukumbuka mazingira na sababu zilizowafanya mastaa hao kujikuta nyuma ya nondo.
Mwanaspoti inakukumbusha visa hivyo kwa kuwakutanisha wasanii watano maarufu waliowahi kushikiliwa polisi au kukaa rumande, sababu zilizowafikisha huko na yaliyofuata baada ya kukumbana na mkono wa sheria.
MATONYA
Msanii wa Bongo Fleva, Sefu Shabani Ramadhan, maarufu kama Matonya, ni miongoni mwa wasanii waliowahi kukaa rumande kwa zaidi ya siku 20 kutokana na kesi iliyomkabili nchini Kenya mwaka 2026.
Matonya alifikishwa katika Mahakama ya Shanzu, Mombasa, akikabiliwa na tuhuma za ubakaji ambazo alizikana. Baada ya kufikishwa mahakamani, alipelekwa Gereza la Shimo La Tewa ambako alikaa rumande akisubiri kutimiza masharti ya dhamana.
Aprili 28, 2026, aliachiliwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama. Tukio hilo lilivuta hisia za mashabiki wake, hasa kwa kuwa msanii huyo alikuwa nchini Kenya wakati akikabiliwa na kesi hiyo.
WEMA SEPETU
Mwigizaji na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, naye aliwahi kupelekwa mahabusu ya Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam mwaka 2019.
Juni 17, mwaka huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru akae mahabusu kwa siku saba, hadi Juni 24, baada ya kushindwa kufika mahakamani katika kesi iliyokuwa ikimkabili.
Wema alikuwa akikabiliwa na kesi ya kuchapisha na kusambaza video ya ngono kwenye mitandao ya kijamii. Amri ya kumweka mahabusu ilitolewa wakati mahakama ikisubiri uamuzi kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya dhamana yake.
OMMY DIMPOZ
Msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz, aliwahi kulala selo akiwa nchini Marekani mwaka 2016. Katika maelezo yake kwenye vyombo vya habari, amesema alikumbana na hali hiyo akiwa Minnesota baada ya kufanya onyesho ambalo masharti ya visa yake hayakumruhusu kulifanya.
Ameeleza kuwa visa yake kilimruhusu kutembelea eneo hilo, lakini hakumruhusu kufanya shughuli za kulipwa kupitia utumbuizaji.
Ommy amesema alikamatwa, akafungwa pingu na kupelekwa kituo cha polisi ambako alilazimika kuvaa mavazi ya mahabusu na kulala selo usiku mmoja.
Asubuhi iliyofuata aliendelea na taratibu za kushughulikia suala la visa yake. Amesema tukio hilo lilimshtua kwa sababu hakuwahi kufikiria kuwa angejikuta nyuma ya nondo akiwa nchini Marekani.
NAY WA MITEGO
Rapa Emmanuel Elibariki, maarufu kama Nay wa Mitego, naye aliwahi kulala selo mwaka 2017 kufuatia sakata la wimbo wake wa ‘Wapo’.
Nay alikamatwa Machi 26, 2017, eneo la Mvomero mkoani Morogoro, baada ya wimbo huo kutafsiriwa kuwa na maneno yaliyodaiwa kuikashifu Serikali iliyokuwa madarakani.
Baada ya kukamatwa, alishikiliwa na polisi Mvomero kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, maarufu kama Sentro. Taarifa zilizochapishwa wakati huo zilieleza kuwa alilala selo kwa siku mbili.
Baadaye aliachiwa huru kufuatia hatua ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kuingilia kati suala hilo. Nay alieleza kuwa hakufanya marekebisho ya wimbo huo kama ilivyokuwa imependekezwa.
MAUA SAMA
Msanii wa Bongo Fleva, Maua Sama, ni mwingine aliyewahi kukumbana na mkono wa sheria na kushikiliwa polisi mwaka 2018, baada ya kukamatwa pamoja na mtangazaji Soudy Brown.
Wawili hao walikamatwa Septemba 16, 2018, kufuatia kusambaa kwa video iliyowaonyesha watu wakirusha na kukanyaga fedha za Tanzania huku wakicheza wimbo wa Maua Sama uitwao ‘Iokote’.
Jeshi la Polisi liliwashikilia kwa tuhuma zilizohusishwa na tukio hilo. Awali walipelekwa Kituo cha Polisi Kinondoni kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa mitandaoni, hasa kutokana na kuhusishwa kwa jina la msanii huyo na video iliyokuwa ikisambaa kwa kasi.
Kwa namna tofauti, Matonya, Wema Sepetu, Ommy Dimpoz, Nay wa Mitego na Maua Sama ni baadhi ya mastaa ambao umaarufu wao haukuwazuia kukumbana na misukosuko ya kisheria, ikiwamo kushikiliwa polisi au kukaa rumande.