Warembo walioandikiwa nyimbo na Barnaba
Muktasari:
- Leo, tunakuletea orodha ya waimbaji wa kike kutokea kwenye Bongofleva ambao wameandikiwa nyimbo na Barnaba, Bosi wa High Tablet Sound studio. Fahamu zaidi.
MBALI na uimbaji wake wa kuvutia, sifa nyingine kubwa ya Barnaba ni kujua kuandika nyimbo vizuri na amewaandikia wanamuziki wenzake wengi.
Leo, tunakuletea orodha ya waimbaji wa kike kutokea kwenye Bongofleva ambao wameandikiwa nyimbo na Barnaba, Bosi wa High Tablet Sound studio. Fahamu zaidi.
1. Vanessa Mdee: Barnaba amehusika kuandika nyimbo tatu za Vanessa Mdee, kuna Hawajui (2014) na nyingine mbili walizoshirikiana ambazo ni Siri (2015) na Chausiku (2018) na zote hizi zilifanya vizuri.
2. Recho: Wimbo uliomtoa mwimbaji huyo wa Tanzania House of Talent (THT), Kizunguzungu (2011) uliandikwa na Barnaba ambaye kwa wakati huo walikuwa na uhusiano. Wimbo huo ulifanya vizuri na ndiyo sababu hadi sasa mwanamuziki huyo anaitwa Recho Kizunguzungu.
3. Shaa: Msanii huyu wa zamani wa kundi la Wakilisha, aliandikiwa na Barnaba wimbo wake uitwao Promise (2012) ambao ulitayarishwa na Manecky chini AM Records.
4. Linah: Moja ya nyimbo za mwanzoni kumpatia mafanikio ya kimuziki Linah ni pamoja na Lonely (2011), huu uliandikwa na Barnaba ambaye wameshirikiana pia katika nyimbo kadhaa ikiwemo Wrong Number.
5. Lulu Diva: Wimbo wa kwanza rasmi wa Lulu Diva, Milele (2016), umeandikwa na Barnaba ambaye pia ameshirikishwa ndani yake. Wimbo huo ulikuja baada ya Lulu Diva kukutanishwa na Barnaba kupitia rafiki yake na mwanamuziki mwenzake, Belle 9.
6. Ruby: Wimbo ulimtoa Ruby kimuziki, Na Yule (2015) umeandikwa na Barnaba, lakini wakati anapewa wimbo huo alitaka kuukata kutokana na kile alichosema unasikika kama wa Injili ila ulipotoka ukafanya vizuri.
7. Shilole: Barnaba ameandika nyimbo tatu za Shilole, Malele (2014), Chuna Bunzi (2017) na Say my Name (2016) ambao wameshirikiana, huku video yake ikifanyika Afrika Kusini.
8. Mwasiti: Wimbo wa Mwasiti, Sio Kisa Pombe (2011) akimshirikisha rapa Quick Rocka, uliandikwa na Barnaba ambaye alipewa nafasi ya kuwa alipo sasa na Mwasiti. Ikumbukwe awali, Barnaba alikuwa akienda THT na nguo za shule ili kutafuta njia ya kuonyesha uwezo wake na kutoka kimuziki, wakati huo Mwasiti ndiye aliyekuwa Jaji wa THT na alimpa nafasi na mengine sasa ni historia.