Linex: Sitaki muziki uniendeshe akili yangu
Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya mahojiano na Linex Sunday Mjeda, kuhusiana na mwaliko alioupata wa miaka 30 ya Bongo Fleva pamoja na mambo mbalimbali yanayohusiana na kazi yake ya muziki.
MSANII wa Bongo Fleva, Sunday Mangu ‘Linex Sunday Mjeda’ ni kati ya wanamuziki wanaoendelea kupiga kazi kimyakimya, akiwa na bendi yake wakati mwingine anafanya chaka tu chaka na mashabiki wanaendelea kufurahia kazi zake.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Linex Sunday Mjeda, kuhusiana na mwaliko alioupata wa miaka 30 ya Bongo Fleva pamoja na mambo mbalimbali yanayohusiana na kazi yake ya muziki.
SHOO ANAZOPIGA
Anaendelea kupiga kazi kimyakimya akiwa na bendi yake, hivyo anapokuwa anahitajika kufanya shoo inakuwa ya makubaliano ya kuimba laivu au kuimba kwa kufuatisha muziki (playback).
“Nilipokuwa naletewa kazi, huwa nawauliza wanataka niende mwenyewe au nibebe vijana, kama wanataka niimbe laivu au playback, naendelea na kazi zangu za muziki kama kawaida, lakini chaka tu chaka kwangu mfano nikienda kuimba kwenye baa zipo zile ambazo hazikubaliani nao pesa, kutokana na namna nilivyoishi, lakini bado napata pesa nzuri,” anasema Linex Sunday Mjeda na kuongeza;
“Kuna wakati kaka yangu Banana Zorro, anakuwa ananipa kazi hasa shoo za kuimba laivu kwa wiki anaweza akaniachia siku tatu, ningekuwa sijaishi nao kwa heshima sidhani kama angeweza kufanya hilo.”
NYIMBO ZINAZOISHI
Anazungumzia kinachombeba katika muziki wake, anachokiona ni zawadi kutoka kwa Mungu na kinaendelea kumwingizia kipato cha kuishi vizuri na kutunza familia yake.
Linex anasema kitu kikubwa ana nyimbo zaidi ya tano zinazoishi, ambazo zikipigwa zinakuwa kama zimetoka kipindi hiki na zinakuwa na mwitikio mkubwa mbele ya mashabiki wake, akiwa anafanya shoo.
“Nyimbo zangu zikiwa zinapigwa zinakuwa na vibe na mashabiki wanakuwa wanaitikia, hilo kwangu ni zawadi kubwa ambayo Mungu alinipendelea, mfano nyimbo zangu kama Mama Halima, Moyo wa Subira,Wema kwa Ubaya, Salima na nyinginezo,” anasema staa huyo na kuongeza:
“Ukiachana na nyimbo zangu, kuna wazee wa zamani ambao nyimbo zao zikipigwa hadi leo, watu wanaamka wanacheza na kuimba mfano wimbo wa Kitambaa cheupe wa marehemu King Kiki, ujumbe uliopo ndani yake unaishi.”
MIAKA 30 YA BONGO FLEVA
Hivi karibuni ilionekana video akifanya shoo, iliyojaza nyomi ya watu analizungumzia hilo kwamba ni ya miaka 13 iliyopita, imewekwa mitandaoni kipindi hiki kwa ajili ya tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva linalotarajia kufanyika Kahama, Novemba 27, 2026.
“Hiyo video ya shoo uliyoiona niliifanya Kahama miaka 13 iliyopita, narudi tena kwa mara nyingine kupitia miaka 30 ya Bongo Fleva, nawashukuru waandaji kwa kunipa heshima hiyo, naamini wenyeji wa mkoa huo watajaa kwa wingi,” anasema na kuongeza;
“Ingawa kwa umri wangu sikustahili kuwepo katika tamasha hilo, kitendo cha kaka zangu kunipa nafasi hiyo kwangu nachukulia kama upendo na heshima.”
HAENDEKEZI MUZIKI
Anasema siyo mtu wa kuendekeza trendi katika mitandao ya kijamii, badala yake anaamini nguvu ya kazi iwe kubwa mbele ya jamii:” Ukiendekeza muziki na kutaka kuzungumziwa kila kona, unaweza ukachanganyikiwa mimi siyo mtu wa kutaka hayo, ninachozingatia ni kufanya kazi kwa ustadi.
“Mbali na video ya miaka 13 iliyopita kutrendi mitandaoni sana, siyo kitu kinachonipa presha ya kutaka kufanya zaidi, naamini katika muziki mzuri lakini siyo uniendeshe akili zangu, mimi natakiwa kuuendesha muziki.”
WEMA UNAVYOISHI
Anasema kuna nyakati msanii jina lake linaweza likawa juu, asipokuwa makini anaweza akawa anawaona watu wengine kama hawana kitu cha maana, kitu anachoshukuru wakati anatajwa kila kona bado aliendelea kuishi kwa nidhamu na heshima.
“Nidhamu na heshima ni wema unaoishi, kuna maeneo nakwenda kupiga shoo kwa sapoti kubwa, kutokana na kuishi nao vizuri, ustaa una mambo mengi ikikosekana hekima, unaweza ukawa unawaona wengine kama hakuna kitu kabisa, lakini wengi wao walioishi kawaida wanaishi na watu vizuri hadi sasa,” anasema.
ANAKUJA NA SAPRAIZI
Anasema katika kumbukumbu yake ya kuzaliwa inayokuwa Februari 14, anakuja na sapraizi kubwa:”Endapo Mungu akijalia atafanya kitu kikubwa, ambacho kitakuwa na mtazamo wa tofauti kwenye kazi zake.”
CHIPUKIZI
Anasema wasanii chipukizi wanapaswa kutambua uwekezaji hauwezi kumaliza kila kitu na kipaji hakiwezi kujitosheleza, inahitajika nidhamu, bidii, muda wa kutosha, kuheshimu watu na pesa.
“Ndiyo maana kuna wasanii wamekuwa wakubwa baada ya kuonekana mitandaoni na hawana kitu, kuna wengine watu wamewekeza mamilioni ya pesa, ila hawajui kuimba, nasisitiza kipaji kizingatie vitu nilivyovitaja,”anasema na kuongeza;
“Muziki ni mpana ukiachana wasanii, kuna mameneja, wapiga picha, watayarishaji (producer), waongozaji (director), warembo wanaotumika katika video (video queen, video king ), wanenguaji kuna watu wengi, ambao wanajipatia kipato cha kuzisaidia familia zao, hivyo lazima uheshimike kama kazi.”
Anasema habagui msanii wa kumsikiliza isipokuwa anavutiwa na uandishi wenye tija ambao atajifunza kitu cha tofauti:” Nawasikiliza wasanii wa sasa na zamani, studio tunakutana na wasanii wa kike wengi bado jamii haijawasikia, ila wana vipaji vikubwa, sauti zao za vibwagizo zinasikika katika nyimbo nyingi za wasanii wakubwa.”
FAMILIA WAIMBAJI
“Familia nzima ni waimbaji wadogo zangu wapo wachungaji, mama zangu wote wanaimba, mdogo wangu anaitwa David anaimba nyimbo za dini, nikiwa mdogo nikiumwa mama alikuwa ananiombea napona, hivyo na watoto wangu wote wanaimba,”anasema Linex anayeutaja wimbo wa Kesho Yangu kuhusu maisha yake halisi, alipitia kipindi ambacho alikuwa na watu ila hawakuweza kutatua changamoto zake, alijihisi kama yupo msituni peke yake.