Mama wa mtoto mmoja atwaa taji la Miss Universe
Muktasari:
- Barreto, mwenye umri wa miaka 27, aliwashinda washiriki zaidi ya 110 kutoka mataifa mbalimbali na kutwaa taji hilo katika hafla iliyofanyika jana Jumanne usiku kwenye ukumbi wa Coliseo de Puerto Rico Jose Miguel Agrelot, jijini San Juan, Puerto Rico.
SAN JUAN, PUERTO RICO: MASHINDANO ya urembo duniani ya Miss Universe yameandika historia mpya baada ya kumtangaza Jennifer Barreto kuwa mshindi wa kwanza mwenye hadhi ya mama katika historia ya miaka 75 ya mashindano hayo.
Barreto, mwenye umri wa miaka 27, aliwashinda washiriki zaidi ya 110 kutoka mataifa mbalimbali na kutwaa taji hilo katika hafla iliyofanyika jana Jumanne usiku kwenye ukumbi wa Coliseo de Puerto Rico Jose Miguel Agrelot, jijini San Juan, Puerto Rico.
Mrembo huyo ambaye ni mwanamitindo, mwanasaikolojia na mfanyakazi wa masuala ya kijamii, ana mtoto wa kike anayeitwa Penelope, jambo lililomfanya kuingia katika historia ya mashindano hayo.
Ushindi huo pia umemfanya kuwa mwanamke wa sita kutoka Puerto Rico kutwaa taji la Miss Universe.
Barreto alikabidhiwa taji hilo na mshindi wa mwaka uliopita, Fatima Bosch kutoka Mexico, kabla ya kusherehekea ushindi wake kwa furaha jukwaani huku akiwa ameshikilia maua na kuonyesha taji lake lililopambwa kwa almasi.
Taji hilo linaloitwa The Radiance of an Eternal Legacy lina almasi 3,150 zilizowekwa kwenye dhahabu nyeupe ya karati 18.
Lilitengenezwa na mbunifu maarufu wa vito vya thamani, George Wittels, kwa kushirikiana na kampuni ya vito vya thamani ya Maison d'OR ya jijini Paris, Ufaransa.
Katika matokeo ya tano bora, Melissa Núñez wa Jamhuri ya Dominika alimaliza nafasi ya pili, akifuatiwa na Clara Vegas wa Venezuela aliyeshika nafasi ya tatu. Washiriki kutoka Ufilipino na New Zealand walikamilisha tano bora.
Ushindi wa Barreto umekuja baada ya Miss Universe kuondoa masharti yaliyokuwa yakiwazuia wanawake walioolewa na wenye watoto kushiriki mashindano hayo kwa muda mrefu.
Mabadiliko hayo yalitangazwa kuanza kutumika mwaka 2023, yakifungua milango kwa wanawake walioolewa na akina mama kushiriki kuwania taji hilo.
Kwa mujibu wa watangazaji wa mashindano hayo, Mario Lopez na mshindi wa zamani wa Miss Universe, R'Bonney Gabriel, mwaka huu kulikuwa na akina mama 10 waliokuwa wakishindania taji hilo.
Miongoni mwao alikuwa Justus Kelley wa Marekani, ambaye Agosti aliandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza aliyeolewa na mwenye mtoto kutwaa taji la Miss USA.
Mashindano ya mwaka huu pia yalishirikisha kwa mara ya kwanza warembo kutoka Saint Martin na Uganda.
Hata hivyo, toleo hilo la 75 halikukosa changamoto. Baadhi ya washiriki kutoka Afrika waliripotiwa kukabiliwa na vikwazo vya kupata visa vilivyotishia ushiriki wao.
Pia, video zilizosambaa zilionyesha warembo wakipata wakati mgumu kutembea kwenye njia iliyotengenezwa kwa muda ufukweni wakati wa maandalizi ya fainali.
Mrembo wa Ufaransa alionekana akitolewa hotelini kwa kiti cha magurudumu baada ya kupata jeraha wakati wa mazoezi ya mashindano hayo, kwa mujibu wa taarifa ya People.
Nayo Vietnam ilikosa mwakilishi baada ya mrembo wake, Nguyen Quynh Anh, kuvuliwa taji kufuatia sakata la kusambaa kwa ujumbe wake binafsi.
Changamoto hizo zimekuja mwaka mmoja baada ya mashindano hayo kukumbwa na matukio mbalimbali yaliyozua mijadala.
Katika mashindano ya mwaka uliopita, mkurugenzi wa Miss Universe Thailand, Nawat Itsaragrisil, alizua mjadala baada ya kumwita mshiriki kutoka Mexico, Fátima Bosch, 'mjinga' wakati wa mazungumzo yaliyokuwa yakirushwa mubashara.
Tukio hilo lilisababisha baadhi ya warembo kuondoka ukumbini kuonyesha mshikamano na Bosch. Baadaye Nawat aliondoa kauli yake na kuieleza kuwa haikubaliki.
Pia, mashindano ya mwaka jana yalishuhudia mrembo wa Jamaica, Gabrielle Henry, akipata jeraha kubwa la kichwa baada ya kuanguka kutoka jukwaani wakati wa hatua ya awali.
Henry alilazimika kujiondoa kwenye mashindano hayo na baadaye kufungua kesi dhidi ya waandaaji wa Miss Universe.
Puerto Rico imeratibiwa kuwa mwenyeji tena wa mashindano hayo ya kimataifa mwaka 2027.