Wanapiga pesa wakiwa kaburini
Muktasari:
Katikati wikiendi, jarida maarufu la Forbes, liliachia orodha ya mastaa wa burudani waliofariki dunia lakini bado wameingiza pesa mwaka huu kutokana na kazi zao za nyuma, hebu waangalie.
KUNA baadhi ya mambo ni vigumu kuyaeleza lakini hutokea. Kwa mfano unawezaje kuelezea ni vipi mfu anaweza kupiga pesa za uhakika wakati nafasi yake ikiwa imetangulia mbele za haki. Lakini kumbe inawezekana!
Katikati wikiendi, jarida maarufu la Forbes, liliachia orodha ya mastaa wa burudani waliofariki dunia lakini bado wameingiza pesa mwaka huu kutokana na kazi zao za nyuma, hebu waangalie.
1. Michael Jackson (Pauni 75 mil)
Mfalme huyo wa muziki wa pop alifariki dunia 2009 lakini mpaka sasa rekodi alizoachia bado zinazidi kumwingizia pesa.
Kwa miaka mitatu mfululizo, ameorodheshwa katika nafasi ya kwanza miongoni mwa mastaa wafu wanaoingiza hela nyingi kila mwaka. Tangu kifo chake hadi kufikia sasa, tayari katengeneza zaidi ya Dola 1 bilioni kiasi ambacho kama angelikuwa hai, kingemtosha kufuta deni lake la mamilioni ya pesa alilokuwa nalo kabla ya kufikwa na mauti. Michael alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 50, lakini kazi zake zimeendelea kuuza na kuingizia familia yake kipato kizuri. Aidha kipato chake kingine kinatokana na majengo yake ya kibiashara aliyowekeza enzi za uhai wake. Kipato cha Pauni 75 milioni mwaka huu kimepungua sana kikilinganishwa na Pauni 90 milioni aliyotengeneza 2014. Cha kushangaza ni kuwa amefanikiwa kuingiza fedha upesi mno wakati akiwa mfu, ikilinganishwa na enzi za uhai wake alikoweza kuingiza kiasi sawa na hiyo Dola 1 bilioni tangu alipoanza muziki miaka ya 1970.
2. Elvis Presley (Pauni 36 mil)
Elvis ndiye mfalme wa mtindo wa Rock ambaye angali anavuna pesa za uhakika akiwa kaburini zaidi ya mastaa wengine wakubwa wa sasa. Agosti mwaka huu shoo ya kumbukumbu ya ‘Elvis Presley Forever’ iliyoandaliwa na idara ya posta ya Marekani, ilingiza mamilioni ya pesa kutokana na mauzo ya tiketi.
Vile vile, pesa zaidi zilitokana na watalii waliozuru nyumbani kwake Graceland Home iliyogeuzwa kuwa makazi yake baada ya kifo chake. Aidha kando na vitega uchumi hivyo, kazi zake bado zinazidi kununuliwa sana sokoni.
Elvis ambaye pia alikuwa mwigizaji wa Hollywood alifariki dunia 1977, akiwa na umri wa miaka 42 kutokana na athari ya matumizi ya dawa za kulevya alizoanza kutumia 1973 na hata kuzidisha baada ya kutalikiana na mkewe 1976, Linda Thompson. Elvis alikumbana na mauti bafuni akiwa kazidiwa na unga.
3. Bob Marley (Pauni 13.7 mil)
Kwenye listi hiyo inayowajumulisha mastaa wengine wafu walio wanamuziki na waigizaji, Bob anakamata nafasi ya tatu kwa wanaburudani na ya nne kwa jumla kutokana na kipato chake hicho.
Bob ndiye mfalme wa muziki wa rege ambao hadi wa leo unazidi kuivunia familia yake pesa za maana licha ya yeye kufariki zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Sehemu kubwa ya kipato hicho inatokana na mauzo ya albamu zake za muziki pamoja na kampuni iliyoanzishwa na familia yake kwa jina lake Marley Beverage.
Mkali huyu wa rege mwenye zaidi ya albamu tano alifariki dunia Mei 1981, akiwa na miaka 36.
Akiwa hospitalini kabla hajakata roho, alimwita mwanawe wa kiume Ziggy Marley na kumpa maneno yake ya mwisho; “Pesa haiwezi kununua uhai.”
4. John Lennon (Pauni 7.8 bil)
Alikuwa ni mwandishi na mwanamuziki kutoka Uingereza aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na bendi yake ya The Beatles. Lennon alizaliwa Liverpool, Uingereza lakini akahamia Manhattan miaka ya 1970 alikofanya kazi zake za muziki.
Mafanikio yake ya muziki ni makubwa akiorodheshwa miongoni mwa wanamuziki 100 bora wa Uingereza wa nyakati zote. Kazi zake zimeuza zaidi ya nakala 14 milioni kufikia 2012.
Lennon alifariki dunia Desemba 1980 baada ya kupigwa risasi mara tano na mmoja wa mashabiki wake sugu Mark David Chapman wakati akiingia kwenye chumba chake cha hoteli moja jijini New York. Chapman aliamua kumuua Lennon baada ya kuokoka na kuchukizwa na moja ya kauli za Lennon kwamba “Kundi lake la Beatle lilikuwa maarufu zaidi ya Yesu.”
5. Paul Walker (Pauni 6.8 bil)
Walker alifariki dunia miaka miwili iliyopita baada ya gari la kifahari aina ya Ferrari alilokuwa akiliendesha kugonga nguzo moja ya umeme na kulipuka. Walker ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na uhodari wake wa uigizaji kwenye msururu wa filamu za Fast & Furious, alikuwa likizoni akijiandaa kustaafu uigizaji ili aweze kuwa karibu na binti yake lakini alikumbana na mauti.
Imeandaliwa na Thomas Matiko