Wanamuziki wasubiri tuzo za Grammy wakiwazia 'kofi la Smith'

Muktasari:
- Achana na sakata la kibao cha Will Smith kwa Chris Rock Jumapili iliyopita, wasanii wa Marekani na duniani watakuwa katika tamasha jingine kubwa la kutuza wanamuziki, maarufu kwa jina la Grammy.
Las Vegas, Marekani (AFP). Achana na sakata la kibao cha Will Smith kwa Chris Rock Jumapili iliyopita, wasanii wa Marekani na duniani watakuwa katika tamasha jingine kubwa la kutuza wanamuziki, maarufu kwa jina la Grammy.
Majina makubwa kama Taylor Swift, Justin Bieber, Billie Eilish na Olivia Rodrigo watakuwa wakiwania Tuzo za Grammy, lakini katikati yao yuko Jon Batiste, mwanamuziki wa jazz aliyeongoza kwa kutajwa kuwania tuzo nyingi mwaka huu.
Jumapili iliyopita, Smith, ambaye alichomoza kwa umaarufu duniani kutokana na kuigiza filamu ya Fresh Prince of Bel Air na nyota wa kibao cha Summer Time alichorap pamoja na DJ Jazz Jeffy, alipanda jukwaani na kumzaba kibao mchekeshaji Rock aliyeingiza utani katika ugonjwa wa kunyonyoka nywele wa Jada Pinckett, ambaye ni mke wa muigizaji filamu huyo.
Tukio hilo lilifunika tamasha hilo kubwa ulimwenguni la kutuza wasanii wa filamu, lakini jana (Ijumaa), Smith ametangaza kujizulu uanachama wa taasisi ya Academy of Motion Picture Arts and Sciences inayoandaa tuzo za Oscar na kusema yuko tayari kwa hatua zozote.
Haitarajiwi tukio kama hilo kutokea kwa mchekeshaji Trevor Noah atakayesherehesha usiku wa Jumapili wakati wanamuziki duniani watakapokuwa Las Vegas kusherehekea mafanikio ya kazi zao baada ya tarehe ya awali ya Januari 31 kusogezwa mbele.
Na katika kujaribu kuzuia hali kama hiyo, habari zinasema Kanye West, ambaye ametajwa kuwania tuzo tano, ameondolewa katika orodha ya watumbuizaji kutokana na tabia zake tata, lakini baadhi wanasema anaweza kupanda jukwaani dakika za mwisho.
Kwa wiki nne, West amekuwa akifanya mashambulizi ya maneno makali kwa mchekeshaji Pete Davidson, ambaye ana mahusiano na mke wake wa zamani, Kim Kardashian.
Rapa huyo mwenye miaka 44 pia alizuiwa Instagram kwa saa 24 baada ya kumtukana Trevor Noah, ambaye atakuwa MC wa tamasha la kesho usiku, baada ya kusema West amekuwa "mkorofi zaidi na zaidi kwa jinsi anavyojaribu kumrudisha Kim".
Na hali hiyo ikidhibitiwa, uwanja uko wazi kwa msanii yeyote kutwaa tuzo baada ya taasisi ya Recording Academy kupanua tuzo nne kubwa kwa kuongeza idadi ya wanaoziwania kufikia kumi, ikiwa ni jitihada za kuboresha ujumuishaji wa makundi yote katika jamii.
Anayepewa nafasi kubwa ya kutamba ni Batiste, mwenye miaka 35 ambaye ametajwa kuwania tuzo 11 licha ya jina lake kutokuwa maarufu katika duru za muziki.
Batiste amerekodi pamoja na wanamuziki magwiji kuanzia kwa Stevie Wonder baadaye kwa Prince hadi Willie Nelson, na pengine ni maarufu zaidi Marekani kutokana na kuwa kiongozi wa bendi na muongozaji muziki wa kipindi maarufu cha komedi cha "The Late Night Show With Stephen Colbert".
Atakuwa akiwania tuzo ya kwanza ya Grammy, akivaana na majina makubwa kama Bieber na Rodrigo katika tuzo kubwa za Albamu na Rekodi ya Mwaka.
Pia atakuwa katika kinyang'anyiro cha tuzo za R&B na jazz katika usiku huo utakaoshereheshwa na mchekeshaji Trevor Noah.
Mwingine anayewania tuzo nyingi ni Justin Bieber aliyetajwa katika tuzo nane, kama ilivyo kwa nyota wa miondoko ya R&B, H.E.R. na mwimbaji na rapa, Doja Cat.
Kipenzi cha Grammy, Billie Eilish anawania tuzo saba, kama ilivyo kwa Olivia Rodrigo, muigizaji wa zamani wa chaneli ya Disney ambaye mwaka jana alichomoza na kibao chake cha "Drivers License."
Lady Gaga na Tony Bennett wana nafasi kubwa ya kujaza zaidi kabati lao la tuzo za Grammy baada ya albamu yao ya "Love For Sale" kutajwa katika tuzo sita.
Kanye West ametajwa katika tuzo kadhaa kutokana na kazi yake ya albamu ya "Donda" na atapambana na Taylor Swift ("Evenmore") katika tuzo ya Albamu ya Mwaka.
Eneo la rap linamjumuisha West sambamba na Nas, J. Cole na Tyler, lakini Drake alijiondoa mwezi Desemba bila kutoa maelezo.
Cardi B na Megan Thee Stallion watapambana katika tuzo ya Best Rap Performance, ambayo huangalia pumzi na kasi ya rapa.
Kundi la muziki wa pop la Korea Kusini, BTS limetajwa katika tuzo moja, lakini limepangwa kutumbuiza usiku wa kesho, sambamba na Rodrigo, Eilish, Batiste na H.E.R. pamoja na Lil Nas X.