Wakongwe wamfungulia milango ya dunia Diamond
Muktasari:
- Wimbo huo ni sehemu ya albamu mpya ya Kidjo, HOPE, iliyotolewa mwaka huu 2026 kupitia Parlophone na Warner Music.
SAFARI ya Diamond Platnumz katika kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa imeendelea kuchukua sura mpya, baada ya msanii huyo kushirikishwa na mwanamuziki mkongwe wa Benin, Angélique Kidjo, katika wimbo ‘Kakua’.
Wimbo huo ni sehemu ya albamu mpya ya Kidjo, HOPE, iliyotolewa mwaka huu 2026 kupitia Parlophone na Warner Music.
Albamu hiyo imewakutanisha baadhi ya majina makubwa katika muziki wa dunia, akiwemo Pharrell Williams, Quavo, Ayra Starr, Davido, Nile Rodgers, Charlie Wilson, Fally Ipupa na Diamond Platnumz.
Ushirikiano huo unaongeza ukurasa mwingine katika safari yake ya kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki na kuendelea kujenga nafasi kimataifa.
KWA KIDJO, HATUA NYINGINE KUBWA
Diamond ameshirikishwa katika wimbo wa tisa wa albamu hiyo, Kakua, ikiwa ni sehemu ya mkusanyiko unaoonyesha namna muziki wa Afrika unavyoendelea kupata nafasi kimataifa.
Kwa miaka kadhaa sasa, Diamond amekuwa akitumia ushirikiano na wasanii wa nje kama njia mojawapo ya kupanua kazi zake za muziki. Safari hiyo imemkutanisha na wanamuziki kutoka Marekani, Jamaica, Nigeria na sasa Benin.
NE-YO- NDOTO IKAWA KWELI
Mwaka 2016 Diamond na staa wa Marekani, Ne-Yo, walifanya kazi kwenye wimbo Marry You, ambao uliingizwa kwenye albamu ya Diamond, A Boy From Tandale. Wimbo huo ulikuwa sehemu ya hatua zilizomsaidia Diamond kuongeza usikivu wake nje ya Afrika Mashariki.
Katika mahojiano yake na GRAMMY mwaka 2020, Diamond alieleza furaha yake ya kufanya kazi na Ne-Yo, akisema mwanamuziki huyo alikuwa miongoni mwa wasanii aliowasikiliza na kuwatazama tangu alipokuwa akianza safari yake ya muziki.
ALICIA KEYS NAYE AKAINGIA KWENYE ORODHA
Diamond alishiriki katika wimbo Wasted Energy, uliowekwa kwenye albamu ya Alicia Keys,iliyotoka mwaka 2020.
Katika mahojiano yake na GRAMMY, Diamond alieleza nafasi hiyo ilijitokeza baada ya kwenda studio na kukutana na Alicia akiwa katika mchakato wa kurekodi muziki.
Kwa maelezo yake, Alicia alitaka kupata ladha halisi ya Bongo Fleva katika kazi hiyo, jambo ambalo Diamond aliliona kama fursa ya kuonyesha muziki wa Tanzania kwenye hadhira pana zaidi.
MORGAN HERITAGE
Safari ya Diamond pia imehusisha ushirikiano na wanamuziki kutoka Jamaica. Mwaka 2017, alifanya kazi na kundi maarufu la reggae, Morgan Heritage, kwenye wimbo Hallelujah.
Ushirikiano huo uliunganisha Bongo Flava na reggae, huku ukionyesha namna muziki kutoka Tanzania ulivyoweza kuingia kwenye mdundo wenye mizizi katika eneo la Caribbean.
Baadaye, Morgan Heritage walimshirikisha Diamond pamoja na Stonebwoy katika Africa X Jamaica, mradi uliowakutanisha wasanii kutoka Afrika na Jamaica kwa lengo la kuunganisha tamaduni kupitia muziki.
DIAMOND NA SAFARI YA KUVUKA MIPAKA
Mbali na majina hayo, Diamond amewahi pia kufanya kazi na wasanii wengine wa kimataifa, akiwemo Omarion na Rick Ross wa Marekani, pia kuna Fally Ipupa, marehemu Papa Wemba, Koffi Olomide na wengine wengi.
Ushirikiano huo umekuwa sehemu ya safari yake ya kujenga jina nje ya Tanzania na Afrika Mashariki. Badala ya kubaki katika mipaka ya muziki wa eneo moja, Diamond ameendelea kutafuta nafasi za kufanya kazi na wasanii wenye mitazamo, tamaduni na mitindo tofauti.