Vanillah awapa tano Apple Music
Muktasari:
- Vanillah ambaye video yake ya Wimbo wa Tamu Chungu aliyomshirikisha Alikiba imetazamwa mara milioni 1.5 katika YouTube ukipandishwa Januari 21, 2026, alisema hayo ikiwa ni siku chache tangu Apple Music ilipomtangaza staa huyo kama mwanamuziki pekee kutoka Tanzania kushiriki katika mpango huo.
STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Vanillah ameishukuru Kampuni ya kimataifa ya Apple Music kumweka katika orodha ya nyimbo 'playlist' ya pamoja na mastaa wakubwa ulimwenguni.
Vanillah ambaye video yake ya Wimbo wa Tamu Chungu aliyomshirikisha Alikiba imetazamwa mara milioni 1.5 katika YouTube ukipandishwa Januari 21, 2026, alisema hayo ikiwa ni siku chache tangu Apple Music ilipomtangaza staa huyo kama mwanamuziki pekee kutoka Tanzania kushiriki katika mpango huo.
Katika programu hiyo iitwayo Up Next Artist Development, Vanillah atapata nafasi ya kushiriki na wasanii wengine wakubwa duniani ambao baadhi wameshinda au kutajwa kwenye Tuzo za Grammy.
"Apple Music imenipa heshima kubwa sana, nawashukuru sana kwa kuniona kama msanii kutoka Tanzania. Tupo wengi, wangeweza kumchukua mwingine lakini wakaniona mimi.
“Najisikia furaha kuwa sehemu ya Apple Music’s Up Next, kwa sababu siyo kila mmoja anaweza kupata bahati kama hii.
"Ni kitu kizuri sana na inaonyesha ukuaji na ukomavu wa kazi yetu kufika kila kona ya dunia," alisema Vanillah.
“Kwa mashabiki zangu naomba watarajie muziki mpya mzuri wenye ladha ya kipekee. Jitayarishe, kwa sababu utapokea maudhui ambayo utafurahia kweli."
Vanillah alitambuliwa kwa mara ya kwanza kama mtunzi wa nyimbo, alipoweka mkono wake katika wimbo wa Alikiba "Utu."
Baada ya kushinda shindano la Super Nyota mwaka 2019, Vanillah alijiunga na Kings Music Records na hivyo kuashiria mwanzo wa kazi bora zilizomweka kwenye ramani ya muziki wa Bongo Fleva.