30 ya Bongo Fleva, wakongwe watinga Arusha
Muktasari:
- Sasa, baada ya miaka hiyo, baadhi ya sauti zilizowahi kutawala redio, mitaani na kwenye kumbi za burudani zinarudi tena mbele ya mashabiki kupitia tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva, safari ambayo baada ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, sasa inatua Arusha Septemba 19, 2026.
Miaka 30 si michache, hasa kwenye muziki ambao kila kizazi huja na ladha yake, lakini kuna nyimbo ambazo muda umepita bila kuzifuta kwenye vichwa vya mashabiki.
Sasa, baada ya miaka hiyo, baadhi ya sauti zilizowahi kutawala redio, mitaani na kwenye kumbi za burudani zinarudi tena mbele ya mashabiki kupitia tamasha la miaka 30 ya Bongo Fleva, safari ambayo baada ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, sasa inatua Arusha Septemba 19, 2026.
SAFARI YA MIAKA 30 YAZUNGUKA TANZANIA
Baada ya kuzunguka Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma, safari inaelekea Arusha na mashabiki wa muziki huo watapata nafasi ya kukutana tena na baadhi ya majina yaliyowahi kuandika historia ya muziki wa kizazi hicho.
Tamasha hili limekuwa likizunguka mikoa mbalimbali kwa lengo la kusherehekea safari ya Bongo Fleva, muziki ambao kwa miongo mitatu umebadilika kutoka sauti za mitaani na redioni hadi kuwa sehemu kubwa ya utamaduni na burudani nchini.
Baada ya Dar es Salaam kuanzisha safari hiyo, Mwanza ilipokea tamasha Agosti 8 na Dodoma ikaendelea Agosti 22, sasa macho yote yanaelekezwa Arusha Septemba 19.
SI TAMASHA TU, NI KUMBUKUMBU
Kwa waandaaji, maadhimisho haya hayahusu burudani pekee. Ni nafasi ya kurudisha mbele ya mashabiki muziki uliowahi kutawala miaka ya nyuma na kuwakutanisha tena wasanii na mashabiki waliokua nao.
Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Hamad Ally ‘Madee’, amekuwa akisisitiza umuhimu wa mashabiki kujitokeza kushuhudia tukio hilo, huku tamasha likilenga kuenzi safari ya Bongo Fleva na watu walioifanya muziki huo kufika ulipo leo.
MWANA FA: BONGO FLEVA INA HISTORIA YAKE
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, ni miongoni mwa viongozi waliogusia umuhimu wa maadhimisho hayo.
Akizungumza wakati wa maandalizi ya tamasha la Mwanza, Mwana FA alisema Bongo Fleva ina historia kubwa katika tasnia ya muziki nchini na kwamba maadhimisho hayo yanapaswa kuakisi safari hiyo.
“Bongo Fleva ina historia yake na tunataka shughuli hii iakisi historia hiyo. Tunataka watu waje kuburudika na kupata burudani yenye ubora,” alisema Mwana FA.
WAKONGWE WARUDI JUKWAANI
Kinachofanya tamasha hili kuwa tofauti ni msisitizo wake kwa wasanii wa kizazi cha mwanzo ambao walikuwepo wakati Bongo Fleva ikianza kujenga jina lake. Majina kama Madee, Fid Q, Dudu Baya, Chid Benz na wengine wamekuwa sehemu ya safari hii, huku mashabiki wakipata nafasi ya kuwaona tena kwenye jukwaa baada ya miaka mingi kupita.
Hawa ni wasanii ambao nyimbo zao hazikuwa burudani tu, bali ziliambatana na maisha ya kizazi fulani.
NYIMBO ZA JANA BADO ZIKO VICHWANI
Miaka inaweza kupita, lakini mashabiki wameonyesha kwamba baadhi ya nyimbo za Bongo Fleva ya zamani hazijafutika kwenye kumbukumbu zao.
Msanii anapopanda jukwaani na kuanza wimbo uliowahi kutamba miaka mingi iliyopita, mashabiki hujikuta wakiimba pamoja naye. Wengine wanakumbuka mistari yote hata kama hawajawahi kuusikiliza wimbo huo kwa muda mrefu. Hapo ndipo nguvu ya muziki wa zamani inapojidhihirisha.
“Nyimbo hizi zilikuwa sehemu ya maisha yetu. Ukisikia tu intro yake, unakumbuka ulikuwa wapi na ulikuwa na nani. Ndiyo maana tunafurahia kuwaona tena hawa wasanii,” alisema mmoja wa mashabiki.
FID Q: BONGO FLEVA ILIKUWA NA UTAMBULISHO
Msanii Fid Q ameeleza pia umuhimu wa muziki wa kipindi hicho, akisisitiza namna Bongo Fleva ya zamani ilivyobeba maisha na utamaduni wa Mtanzania.
“Bongo Fleva ya zamani ilikuwa na utambulisho wa kipekee uliobeba lugha, tamaduni, na simulizi za maisha ya Mtanzania,” alisema Fid Q.
Kauli hiyo inaeleza kwa kiasi kikubwa kwa nini nyimbo hizo bado zina nafasi kwenye mioyo ya mashabiki. Zilikuwa zikisimulia maisha waliyoyaona na kuyapitia wenyewe.
VIZAZI VIMEPITA, HISTORIA IMEBAKI
Katika miaka hiyo 30, Bongo Fleva imepitia vizazi mbalimbali. Baada ya walioweka misingi, walikuja wengine waliobeba muziki huo na kuufikisha kwenye viwango vipya.
Lakini kwa tamasha hili, lengo si kushindanishwa kizazi cha zamani na wasanii wanaotawala sasa.
Badala yake, ni kuangalia walikotoka.
Wakongwe hawa ndio waliokuwa sehemu ya kipindi ambacho Bongo Fleva ilianza kupata utambulisho wake, kuzungumzia maisha ya Mtanzania na kujenga mashabiki waliokuja kuwa msingi wa soko la muziki wa ndani.
UELEKEO ARUSHA
Septemba 19, mashabiki wa jiji hilo watapata nafasi ya kuendelea na safari ambayo tayari imewakutanisha maelfu ya mashabiki na wasanii waliowahi kuwa sehemu ya historia ya Bongo Fleva.
Kwa waandaaji, ni kusherehekea miaka 30 ya muziki. Kwa wasanii, ni nafasi ya kurudi mbele ya mashabiki waliowahi kuwapa nguvu.
Kwa mashabiki, ni safari ya kurejea kwenye enzi ambazo nyimbo ziliweza kuwa gumzo la mitaani na kumbukumbu ya maisha.
Miaka 30 imepita, lakini ukweli mmoja unaendelea kuonekana wazi; Bongo Fleva imebadilika, vizazi vimepita, lakini nyimbo za wakongwe bado zinaishi.
Na sasa, Arusha inaingia kwenye mstari wa kuzikumbuka tena.