Usiri siku za mwisho za maisha ya Dolly Parton
Muktasari:
- Miongoni mwa mambo ambayo wengi wanajiuliza ni usiri wa miezi yake ya siku za mwisho, ugonjwa wa saratani ambao hata yeye hakuwahi kuuzungumzia na masuala kadhaa wa kadhaa.
Tennessee, Marekani: KILA msiba haukosi sababu. Lakini, kila msiba watu hawakosi cha kuzungumza. Ndivyo ilivyo kufuatia kifo cha mwanamuzi maarufu wa muziki wa country, Dolly Parton ambapo siku zake za mwisho zilighubikwa na usiri unaocha maswali kwa sasa katika mijadala mbalimbali duniani.
Miongoni mwa mambo ambayo wengi wanajiuliza ni usiri wa miezi yake ya siku za mwisho, ugonjwa wa saratani ambao hata yeye hakuwahi kuuzungumzia na masuala kadhaa wa kadhaa.
Dolly alifariki dunia jana katika Kituo cha Vanderbilt-Ingram Cancer kilichopo Nashville, Tennessee, Marekani akiwa na umri wa miaka 80. Kifo chake kimeacha pigo kubwa katika muziki wa country, na katika maisha ya mamilioni ya watu waliokua enzi hizo wakisikiliza nyimbo zake kama Jolene, 9 to 5 na I Will Always Love You.
Familia yake ilitangaza kuwa alifariki kwa ugonjwa wa saratani katika kile ilichoeleza kuwa ni mapambano mafupi dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni siku nne tu tangu alipoonekana hadharani na kuzungumza akisema "nimekuwa kimya kidogo kutokana na changamoto ndogo ya kiafya".
Lakini, kilichowashangaza wengi ni kwamba, hadi muda mfupi kabla ya kifo chake, Dolly aliendelea kuonekana hadharani kwa namna iliyomfanya mtu aamini kwamba bado alikuwa na mipango mingi ya maisha.
Siku chache kabla ya kifo chake, Dolly aliwaambia mashabiki kwamba bado alikuwa na mambo mengi aliyotaka kuyafanya. Kauli hiyo sasa imekuwa ya kusikitisha zaidi kwa sababu ilikuwa miongoni mwa ujumbe wake wa mwisho kwa umma. Lakini, ni yapi mengine ambayo yanajadiliwa na mashabiki wa muziki duniani juu ya nyota huyo?
Ugonjwa aliuficha kwa kiasi gani?
Taarifa za sasa zinaonyesha kwamba Dolly alikuwa akipambana kwa siri na saratani kabla ya kifo chake. Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha ukweli uliothibitishwa na madai yanayosambazwa na mitandao ya udaku ya Marekani.
Lakini, vyombo vikubwa vya habari ikiwamo Reuters na AP vimethibitisha kwamba alifariki duni baada ya mapambano mafupi dhidi ya saratani, ingawa taarifa zao hazitoi maelezo ya kina kuhusu aina ya saratani, hatua ya ugonjwa au matibabu aliyopitia.
Kwa hiyo, madai kwamba “alijua maisha yake yamekwisha”, kwamba aliwaambia watu fulani siri hiyo, au kwamba alikuwa akijificha kwa makusudi kutokana na hali yake, yanachukua mjadala kwa sasa hadi familia au watu wa karibu watakapoeleza pengine siku za usoni juu ya tatizo hilo la kiafya.
Miezi sita ya kujitenga
Sehemu inayovutia zaidi katika simulizi juu ya maisha ya nyota huyo ni madai kwamba alikuwa akijitenga na maisha ya kawaida kwa takribani miezi sita ya mwisho.
Na hapa ndipo inapoibua wasiwasi kuwa huenda alikuwa mgonjwa na pengine ugonjwa aliokuwa nao ulikuwa umefikia hatua mbaya zaidi.
Lakini, taarifa zinazopatikana sasa hazielezi kwa uhakika kwamba alitumia miezi yote sita akijua kwamba angekufa. Kinachoweza kuthibitishwa ni kwamba katika kipindi chake cha mwisho kulikuwa na changamoto za kiafya, huku yeye mwenyewe akiwa kueleza kwamba baada ya kifo cha mumewe, Carl Dean, alikuwa akijaribu kujijenga tena kiroho, kihisia na kimwili. Dean alifariki dunia Machi 2025 baada ya karibu miaka 60 ya ndoa na Dolly. Hivyo, huzuni ya kumpoteza mume wake na changamoto zake za kiafya vilikutana katika kipindi kigumu cha maisha yake.
Je, Miley alijua kuhusu saratani?
Miongoni mwa watu waliokuwa karibu sana na Dolly ni Miley Cyrus, ambapo inadaiwa kwamba mkongwe huyo wa muziki wa country alikuwa kama 'godmother' wa Miley, na uhusiano wao haukuwa wa kawaida wa msanii mkubwa na msanii mdogo waliyefahamiana tu, bali Dolly alikuwa sehemu ya maisha ya familia ya Cyrus kwa miongo kadhaa.
Sasa kuna madai yanayoenea kwamba Miley hakujua mapema kuhusu saratani ya Dolly na kwamba, taarifa hizo zimemletea mshtuko mkubwa baada ya kifo chake. Lakini hadi sasa, hakuna chanzo cha kuaminika au taarifa rasmi ya familia inayothibitisha kwamba Miley hakujua kuhusu ugonjwa huo, wala kwamba alipata kile kinachoelezwa kuwa mshtuko baada ya taarifa hizo.
Kwa hiyo, si sahihi kueleza kwamba Miley alikuwa hajui kabisa au alipata taarifa fulani kutoka kwa watu wa ndani, isipokuwa kama familia au Miley mwenyewe atathibitisha. Kinachojulikana ni kwamba Billy Ray Cyrus, baba yake Miley ametoa heshima kihisia kwa Dolly baada ya kifo chake na kueleza ukubwa wa uhusiano wao wa muda mrefu. Pia amegusia namna Dolly alivyokuwa sehemu ya familia yao, hasa kutokana na kuwa karibu na Miley.
Alipoteza nywele zote?
Hili ni dai lingine linaloonekana kuanza kujadiliwa na baadhi ya vyombo vya habari, lakini nalo halina uthibitisho kutoka vyanzo vya kuaminika kwamba Dolly alipoteza nywele zake zote kutokana na matibabu ya saratani.
Inawezekana madai hayo yanatokana na taarifa za watu wanaodai kuwa aliugua muda mrefu saratani. Na hili si muhimu kwa sababu kupoteza nywele siyo lazima kutokee kwa kila mgonjwa wa saratani, bali hutegemea na aina ya saratani na aina ya matibabu anayopokea mgonjwa.
Ujumbe wake wa mwisho
Mojawapo wa mambo yanayofanya kifo chake kuwa cha kusikitisha zaidi ni kwamba Dolly alikuwa akifikiria kuhusu kazi, watu na miradi yake hadi mwishoni. Miongoni mwa ujumbe wake wa mwisho kwa umma kulikuwa na video aliyorekodi kumshukuru Taylor Swift na Travis Kelce kwa mchango wa Dola 2 milioni kwa ajili ya mradi wake wa 'Imagination Library', taasisi yake inayolenga kuwapatia watoto vitabu bure. Ujumbe huo ulitolewa Julai 3, 2026. Hii inaonyesha kwamba, hata wakati afya yake ilikuwa ikizorota, bado alikuwa akifikiria kuhusu urithi wake na kazi ya kuwasaidia watoto.
Kwa sasa, jambo la msingi ni kwamba Dolly Parton alifariki baada ya mapambano mafupi dhidi ya saratani, lakini maelezo mengi kuhusu miezi yake ya mwisho bado hayajawekwa wazi hadharani.
Dolly alikuwa mmoja wa waimbaji waliotunukiwa zaidi katika historia na aliingizwa katika 'Rock and Roll Hall of Fame' 2022. Alishinda tuzo 10 za Grammy, 13 za Academy of Country Music, Emmy pamoja na uteuzi wa Tony na uteuzi mara mbili wa tuzo za Oscar. Mwaka 2025, aliheshimiwa na Academy kwa tuzo ya 'Jean Hersholt Humanitarian'.