Harmonize, Abigail Chams kuwakilisha The Headies 2026
Muktasari:
- Wawili hao wameingia kwenye orodha ya wasanii watano wanaowania tuzo hiyo pamoja na Bien wa Kenya, Bruce Melodie wa Rwanda na Joshua Baraka wa Uganda.
BONGOFLEVA imepewa nafasi nyingine ya kujiweka mbele katika tuzo kubwa za muziki Afrika baada ya Harmonize na Abigail Chams kutajwa kuwania tuzo ya Best East African Artiste katika The Headies 2026.
Wawili hao wameingia kwenye orodha ya wasanii watano wanaowania tuzo hiyo pamoja na Bien wa Kenya, Bruce Melodie wa Rwanda na Joshua Baraka wa Uganda.
Uteuzi huo umeifanya Tanzania kuwa nchi yenye idadi kubwa ya wawakilishi, ikiwa na wasanii wawili katika kipengele hicho cha wasanii watano wa Afrika Mashariki.
Hii si mara ya kwanza Tanzania kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho, wala si mara ya kwanza kuondoka na tuzo. Diamond Platnumz aliandika historia mwaka 2022 baada ya kutwaa tuzo ya Best East African Artiste katika toleo la 15 la The Headies lililofanyika Atlanta, Marekani.
Ushindi huo uliipa Tanzania nafasi kubwa zaidi katika mjadala wa muziki wa Afrika Mashariki kwenye jukwaa ambalo kwa kiasi kikubwa linahusishwa na Nigeria.
Mwaka 2025, Juma Jux aliendeleza rekodi ya Tanzania akitwaa tuzo ya Best East African Artiste kupitia wimbo wa Enjoy, akiwashinda, miongoni mwao, Diamond Platnumz na Bien wa Kenya.
Pia, ushindi huo ukawa uthibitisho mwingine kwamba wasanii wa Tanzania wana uwezo wa kushindana kwenye jukwaa kubwa la muziki linalotoka nje ya nchi.
Muziki wa Tanzania sasa hauishii kwenye mashabiki wa ndani pekee. Wasanii wamekuwa wakishirikiana na mastaa wa nchi nyingine, kufanya matamasha nje ya Tanzania na kutafuta hadhira katika masoko ya Afrika.
Kwa Harmonize, uteuzi huo ni nafasi ya kurejea kwenye kilele cha ushindani Afrika Mashariki, wakati Abigail Chams ni fursa ya kuthibitisha kuwa kizazi kipya cha Bongo Fleva kinaweza kusimama kwenye meza moja na majina yaliyojenga ushawishi mkubwa barani.
Kama mmoja wao ataibuka mshindi, Tanzania itakuwa imeendeleza mfululizo wa ushindi ulioanzishwa na Diamond na kuendelezwa na Juma Jux.
The Headies ni moja ya tuzo kubwa na maarufu za muziki nchini Nigeria. Zilianzishwa mwaka 2006, wakati huo zikiwa zinajulikana kama Hip Hop World Awards kwa lengo la kutambua na kuwatuza wasanii, watayarishaji na wadau mbalimbali waliofanya vizuri katika muziki wa Nigeria.
Baadaye, mwaka 2011, tuzo hizo zilibadilishwa jina na kuitwa The Headies, na tangu wakati huo zimeendelea kuwa miongoni mwa tuzo muhimu zaidi katika tasnia ya muziki nchini Nigeria na Afrika kwa ujumla.
Mwaka huu ni toleo la 18. Tuzo hizo zitafanyika jijini Toronto, Canada, Oktoba 25, 2026, zikiwa na kaulimbiu ya “Africa to the World,” zikilenga kuendelea kuonyesha na kusherehekea mafanikio ya muziki wa Afrika katika jukwaa la kimataifa.