TuneCore kunufaisha wasanii Afrika Mashariki
Kampuni ya usambazaji wa muziki kidigitali na kukusanya mirabaha ya wasanii huru, TuneCore imezindua shughuli zake katika nchi za Afrika Mashariki na barani Afrika kwa jumla.
Tayari Jade Leaf ameajiriwa kama Mkuu wa TuneCore wa Afrika ya Kusini na atashiriki majukumu ya nchi kuu zilizo Afrika Mashariki na Chioma Onuchukwu, ambaye ameajiriwa kama Mkuu wa TuneCore wa Afrika Magharibi.
Leaf na Onuchukwu wataripoti kwa Faryal Khan-Thompson, Makamu wa Rais wa Kimataifa katika TuneCore.
Onuchukwu atakuwa Nijeria na atasimamia nchi zilizomo Afrika Magharibi ikiwemo Nigeria, Ghana, Liberia, Siera Leon na Gambia.
Aidha, Onuchukwu atasimamia pia Tanzania na Ethiopia zilizomo Afrika Mashariki.
Himaya ya Leaf inajumuisha Afrika ya Kusini, ikiwemo Afrika Kusini, ambayo itakuwa makao yake makuu, na hata pia Namibia, Botswana, Zimbabwe, Zambia, Malawi na Lesotho.
Leaf atasimamia pia shughuli za TuneCore katika nchi za Afrika Mashariki, Kenya na Uganda.
“Ni faraja kwangu kufanya kazi na kampuni huru ya usambazaji wa muziki, hasa katika karne hii ya ajabu sana kwa wabunifu wa muziki barani Afrika wakati ambao tunapata kutambuliwa kimataifa na tunaongezea bidii,” alisema Onuchukwu.
Kabla ya kujiunga na TuneCore, Onuchukwu alikuwa Meneja wa Masoko wa uduX Music ya Nigeria ambapo alifanya kazi kwa mwaka mmoja na wasanii maarufu kama Davido, Yemi Alade, Patoranking, Kizz Daniel na wengine wengi.
Kwa upande wake, Leaf alisema kuwa ana furaha kubwa kufanya kazi na kampuni hiyo kubwa ya masuala ya muziki na kuahidi kufikia malengo yaliyowekwa.
Kampuni ya TuneCore inafungua ulimwengu wa uwezo kwa wasanii huru katika kila ngazi ya kazi zao.
Afrika ni makao ya wasanii mbalimbali wanaotafuta huduma thabiti ya usambazaji inayoelewa mahitaji yao ya nchini na inaweza kuwapa nafasi ya kubadilisha sanaa yao kuwa ufanisi wa kibiashara.
Awali, Leaf alifanya kazi katika kampuni kubwa zaidi Afrika ya TV ya kulipia, Multichoice kama Meneja wa Masoko wa Vituo vya Vijana na Muziki, ambapo aliongoza katika kuipa kampuni hiyo sura mpya na katika juhudi za masoko kwa kituo kikubwa cha Muziki wa TV cha Channel O.
Kabla ya hiyo, alifanya kazi Sony Music Entertainment Afrika, akilenga wasanii na maudhui ya Kiafrika, na hata kampeni nyingi za masoko na miradi ya wasanii wa nchini na wa kimataifa.
Kumekuwa na ongezeko la kukubalika kwa huduma za utiririshaji barani Afrika, ukuaji huu umesababishwa na mambo kadhaa kama vile kuongezeka kwa ufikiaji wa intaneti kupitia simu mahiri, kuingia kwa majukwaa ya utiririshaji ya kimataifa na ya nchini katika himaya kuu na idadi ya vijana - zaidi ya asilimia 60 ya Waafrika wamo chini ya umri wa miaka 25.
Katika mwaka wa 2020, TuneCore ilishuhudia ongezeko katika matoleo ya muziki kimataifa, huku wasanii wengi wa Kiafrika wakichagua kutumia wasambazaji wa DIY - DJ Spinall na Small Doctor nchini Nigeria, Spoegwolf nchini Afrika Kusini, Mpho Sebina nchini Botswana na Fena Gitu nchini Kenya.
“Afrika ni soko linalosisimua sana la muziki lenye uwezo mkubwa wa kukua," alisema Khan-Thompson.
TuneCore, inayomilikiwa na Believe ya Paris, imekuwa ikipanua kwa haraka shughuli zake za kimataifa, kuanzia nchi tano mwaka wa 2020 hadi nchi nane na maeneo matatu makuu katika mwaka 2021.
Kampuni hii iliongezea India, Urusi na Brazili mwaka uliopita na mwaka huu ikaongezea LATAM, Asia ya Kusini Mashariki na Afrika.