Tanzania kuandaa mashindano ya urembo ya Miss East Africa 2021

Dar es Salaam. Mashindano ya kumsaka mrembo wa Afrika Mashariki, Miss East Africa 2021 yatafanyika jijini Dar es salaam mwezi wa Novemba mwaka huu.
Makamu wa Rais wa mashindano hayo, Jolly Mutesi amesema kuwa maandalizi ya awali ya mashindano hayo makubwa ya urembo yameanza na kuwataka warembo kuanza kujiandaa.
Mutesi ambaye yupo nchini kwa ziara ya wiki mbili alisema kuwa wanatarajia kuwa na mashindano makubwa yenye mvuto wa kipekee kabisa.
Alisema kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuangaliwa na watu wengi Dunia nzima kupitia kwenye matangazo ya moja kwa moja ya Televison (Live) na hivyo kutoa nafasi nzuri ya kutangaza utalii wa Tanzania pamoja na kuonyesha fursa mbalimbali za uwekezaji
“Hii ni fursa kwa makampuni mbalimbali yanayohitaji kutangaza biashara zao kwa ndani nan je ya mipaka ya Tanzania kupitia katika mashindano haya makubwa ya urembo,” alisema Mutesi.
Alisema kuwa jumla ya nchi 16 zitashiriki katika mashindano haya. Nchi hizo ni  ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea na Djibouti.
Nchi nyingine ni Somalia, Madagascar, Malawi, Seychelles, South Sudan, Comoros, Reunion na Mauritius.
Mashindano ya Miss East Africa yalianzishwa na Mtanzania  Rena Callist na kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1996 kwa mafanikio makubwa katika Hoteli ya Sheraton (Serena kwa sasa).
Mashindano hayo pia yamewahi kufanyika katika nchi ya Burundi kwa udhamini wa Rais wa Burundi wa wakati huo hayati rais Piere Nkurunzinza

Mashindano ya mwisho kufanyika ilikuwa ni mwaka 2012 ambapo yalifanyika katika ukumbi wa Mlimani City Jijini dar es salaam na kuangaliwa na mamilioni ya watu Duniani kote kupitia matangazo ya moja kwa moja mubashara ambapo yalitangaza utalii wa Tanzania kwa kiasi kikubwa.
Alisema kuwa kuanzia sasa mashindano ya Miss East Africa yatakuwa yakifanyika kila mwaka ambapo yatasaidia sana katika kudumisha umoja wa Afrika mashariki.
Pia mashindano haya yatasaidia kukuza utalii, kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji hasa katika nchi inayoandaa mashindano hayo na pia kutoa elimu na kusaidia katika changamoto mbalimbali hasa zinazowakabili wanawake na watoto wa ukanda huu wa Afrika ya Mashariki.
Mashindano hayo yanaandaliwa na kampuni ya Rena Events Limited ya Jijini Dar es salaam, Tanzania.