Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sura ya mtoto wa Jux, Priscilla yaanikwa kwa mara ya kwanza

JUX Pict

Muktasari:

  • Wawili hao wamemuonyesha mtoto wao, Prince Rakeem Mkambala, kwa umma kwa mara ya kwanza leo, Agosti 24, 2026, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea kutimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwake.

MWANAMUZIKI maarufu nchini Tanzania, Juma Jux pamoja na mkewe mwanamitindo kutoka Nigeria, Priscilla Ojo, wameweka hadharani picha zinazoonyesha sura ya mtoto wao Rakeem, baada ya kutimiza mwaka mmoja.

Wawili hao wamemuonyesha mtoto wao, Prince Rakeem Mkambala, kwa umma kwa mara ya kwanza leo, Agosti 24, 2026, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea kutimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwake.

Kupitia chapisho la Instagram, picha hizo zimeambatanishwa na ujumbe uliosomeka: "Tulipepesa macho, na mwaka mzima ukapita. Kwa mwanetu wetu mpendwa.

JU 01

"Kukuona ukikua imekuwa baraka kubwa zaidi kwetu. Wewe ni mtoto wetu mchangamfu, mwenye furaha, akili nyingi na utundu wa kupendeza. Unaangaza kila unapopita, na tunajivunia sana kuwa wazazi wako.

"Siku 365 za kukupenda, kukubeba, kukukumbatia na kushuhudia utu wako mzuri ukizidi kung'aa. Wewe ni mdadisi, mwenye furaha, mwenye akili na umejaa maisha. Kila siku unaifanya iwe nzuri zaidi kwa kuwa wewe tu.

"Hatuamini jinsi ulivyokua kwa haraka, mwanga wetu mdogo wa jua. Tunakuombea maisha yako yajazwe na furaha nyingi kama ile ambayo umetupatia katika mwaka huu wa kwanza.

JU 02

"Tunamuomba Mungu akujalie afya njema, furaha na maisha yenye kusudi. Tunamuomba akuongoze katika kila hatua na ainyoshe njia yako. Tunamuomba ujue kila siku jinsi unavyopendwa kwa dhati na kwa moyo wote. Tunamuomba kicheko chako kisikome kamwe, na moyo wako mzuri ubaki safi siku zote.

"Wewe ni jibu letu kubwa zaidi la maombi. Heri ya kutimiza mwaka mmoja wa kuzaliwa, mwanga wetu wa jua! Tunakupenda bila kikomo, leo, kesho na milele."

Tangu alipozaliwa nchini Canada Agosti 24, 2025, wazazi hao waliamua kuficha sura ya mtoto wao huyo katika mitandao ya kijamii kwa lengo la kulinda faragha yake na kumpa nafasi ya kukua mbali na shinikizo la umaarufu wa wazazi wake.

Uamuzi huo uliwafanya mashabiki wao kusubiri kwa hamu kuona sura ya mtoto huyo, huku Jux na Priscilla wakiendelea kushirikisha picha na matukio mbalimbali ya familia bila kuonyesha uso wake.

JU 03

Hata hivyo, kufikisha mwaka mmoja kwake kumekuwa tukio maalum kwa familia hiyo, ambapo wazazi wake wameamua kuvunja ukimya na kumtambulisha Rakeem kwa umma kupitia picha zilizoshirikishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Picha hizo zimepokelewa kwa hisia mbalimbali na mashabiki wao, ambao wamejitokeza kutoa salamu za pongezi na kumtakia Prince Rakeem maisha marefu, afya njema na mafanikio katika maisha yake.

Jux na Priscilla wamekuwa miongoni mwa wanandoa maarufu wanaofuatiliwa kwa karibu Afrika Mashariki na Magharibi, kutokana na shughuli zao za muziki, mitindo na maisha yao ya kila siku wanayoshirikisha kwenye mitandao.

Kuzaliwa kwa Rakeem mwaka mmoja uliopita kuliongeza zaidi umaarufu wa familia hiyo, huku mashabiki kutoka Tanzania, Nigeria na mataifa mengine wakifuatilia kwa karibu safari yake.