SO FIRE: BSS imempeleka Miaka 30 ya Bongo Flava!
Muktasari:
- Safari yake imepitia hatua mbalimbali, lakini BSS imekuwa moja ya majukwaa muhimu yaliyompa utambulisho na kumfungulia milango ya fursa nyingine ndani na nje ya muziki.
KUTOKA kwenye mashindano ya Bongo Star Search (BSS), kushika nafasi ya pili katika ushiriki wake wa kwanza hadi kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava, msanii Sophia Benson a.k.a So Fire ni miongoni mwa majina yanayoendelea kujitengenezea nafasi katika muziki huo.
Safari yake imepitia hatua mbalimbali, lakini BSS imekuwa moja ya majukwaa muhimu yaliyompa utambulisho na kumfungulia milango ya fursa nyingine ndani na nje ya muziki.
So Fire anasema kushiriki kwake kwa mara ya kwanza kwenye BSS na kuibuka mshindi wa pili ni mafanikio makubwa, hasa akilinganisha na washiriki waliowahi kushiriki mashindano hayo kwa miaka mingi bila kufika fainali.
“Kwa upande wangu mimi kuwa mshindi wa pili nilifurahi sana, nilijivunia kwa sababu kwa mara yangu ya kwanza kushiriki BSS, ni kitu kikubwa sana.”
“Kuna watu wameshiriki BSS miaka mitano, 10 na hawakuingia fainali,” anaongeza So Fire.
Anasema hiyo pia imekuwa nafasi kwake ya jina kujulikana na sasa anapata fursa fursa mbalimbali za kujipatia kipato.
“Mbali na zawadi ya Bongo Star Search walichonipatia kikubwa zaidi ni jina. Watu wananifahamu sasa hivi, ninaweza nikafanya matangazo ya biashara za watu kwa sababu tayari nina jina.
“Naweza nikapata pesa kutokana na jina langu tu, mtu akaniambia bwana nina biashara yangu nifanyie tangazo na nikapata pesa,” anasema.
BLACK QUEEN AMPA NAFASI YA KUCHANA
Anasema amekuwa akipambana kutafuta nafasi ya kuonyesha kipaji chake na kuwaonyesha mashabiki anaweza kurap na katika mitandao ya kijamii amekuwa akiwasiliana na wasanii mbalimbali.
Moja ya matunda ya kujituma huko ni kolabo yake na rapa wa kike, Black Queen.
“Sisi ni wasanii, hususani mimi hapa napenda sana kuwatafuta wasanii wenzangu. Huwa na-DM wasanii wengi sana kwa sababu siwezi kuwa eti kila siku nikafanya kazi pekee yangu, ni kitu ambacho hakiwezekani.
“Kwa hiyo naendelea kuwatafuta wengi ili niwe na connection na watu wengi,” anasema.
“Mimi ndiye niliyemtafuta akanijibu, tukatumiana namba, hivyo tukachati, tukakubaliana kuonana studio na kazi ikafanyika,” anasema.
MASHABIKI WAUPOKEA
Akizungumzia mapokezi ya wimbo huo, anasema amefurahishwa na namna mashabiki walivyoipokea kazi hiyo, hasa wale waliokuwa wakisubiri kumuona akionyesha makali yake kwenye upande huo wa muziki.
“Mapokezi ya nyimbo ni makubwa, siyo madogo na watu wengi walikuwa wanatamani kumuona So Fire akichana na kweli kwenye huo wimbo mimi nimechana,” anasema.
So Fire hataki kujifunga kwenye aina moja ya muziki na anaamini msanii anatakiwa kuwa na uwezo wa kubadilika na kuonyesha vipaji vyake katika mitindo mbalimbali.
Anasema baadhi ya watu walikuwa na matarajio ya kumuona akifanya rap pekee, lakini yeye anatamani mashabiki wamfahamu kama msanii anayeweza kufanya zaidi ya mtindo mmoja.
“Wengi walitegemea nitakuja pale nitaanza kurap hivyo, lakini sikufanya hivyo kwa sababu mimi sitamani kufanya muziki mmoja, napenda kubadilika badilika.”
MIAKA 30 YA BONGO FLAVA YAMPA JUKWAA
Kutoka kwenye mafanikio ya BSS, hatua nyingine iliyoo ngeza ukurasa mpya katika safari ya So Fire ni kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava lililofanyika Mbeya.
Tofauti na ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiria kuwa nafasi hiyo ilimjia kupitia mwaliko wa kawaida, So Fire anasema yeye mwenyewe alichukua hatua ya kwenda kuomba nafasi hiyo kupitia kituo cha redio cha UFM cha Azam.
Anasema wakati akifanya mahojiano kwenye kituo hicho, alitumia nafasi hiyo kueleza nia yake ya kutaka kupanda jukwaani, huku Mtangazaji Jabir Saleh akimsaidia kusisitiza ombi hilo.
Nilienda kwenye maojiano pale Azam kwenye redio ya UFM, nikaenda kuomba pale nafasi ya ku-perform. Namshukuru Mungu na kakangu Jabir pia akakazia pale, akasema, Bwana Madii, unamuona binti yetu hapa ni mtu wa Mbeya, mpatie nafasi.
“Kweli Madii ni mtu mwenye moyo safi sana, hakuninyima nafasi, akanipatia fursa nikaenda ku-perform,” anasema na kuongeza.
“Sikuwahi kutarajia kama naweza nikapata hiyo nafasi, lakini mimi naamini hakuna kitu kinachokuja kwenye maisha ya mtu kwa bahati mbaya.
“Ni Mungu alipanga na Madii aliona ‘the way’ mtoto wake navyojipambania na kuamua kunisapoti,” anasema.
Pamoja na furaha ya kushiriki tamasha hilo lililobeba historia ya muziki wa Bongo Fleva, So Fire alisema bado anajiona kama msanii anayehitaji kuendelea kujifunza na kutafuta nafasi zaidi, bila kujilinganisha na wengine waliokuwa na ndoto kama yake.
“Haina maana mimi kwenda kushiriki Miaka 30 ya Bongo Flava mimi nilikuwa bora zaidi ya wengine? Hapana. Au mimi nilikuwa labda na kipaji kikubwa sana kuzidi wengine? Hapana. Naendelea kuwa mnyenyekevu ili kupata nafasi nyingi zaidi maeneo mbalimbali,” anasema.