Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZUBERY: Safari ya muziki yenye siri nzito bado inaendelea...

Muktasari:

  • Safari yake muziki imejaa siri nzito, kuanzia kuimba sauti zilizobeba tamthilia kubwa za televisheni nchini, kuandikia mastaa wakubwa wa Bongo Fleva huku wakimnyima kile kinachoitwa ‘maua yake’, hadi kuja kutingisha taifa kupitia kibao chake cha ‘Dear Ex’.

WAKATI wimbi la vijana wa sasa likikimbilia mitindo ya kisasa ya Bongo Fleva na Singeli, kijana mmoja kutoka Temeke ameamua kwenda kinyume na mkumbo na kuichachafya gemu ya muziki wa dansi nchini. Ni Zubery Ndaki, anayefahamika zaidi kama ‘Gen Z wa Twanga Pepeta’.

Safari yake muziki imejaa siri nzito, kuanzia kuimba sauti zilizobeba tamthilia kubwa za televisheni nchini, kuandikia mastaa wakubwa wa Bongo Fleva huku wakimnyima kile kinachoitwa ‘maua yake’, hadi kuja kutingisha taifa kupitia kibao chake cha ‘Dear Ex’.

Dakika 5 Na... lilifanya naye mahojiano kufahamu machache ikiwamo kilicho nyuma ya mafanikio yake, , kuingia Twanga Pepepta iliyo na wakongwe, Kwa Mkubwa Fella hadi kuchukuliwa na Asha Baraka anayeimiliki Twanga Pepeta.

Mwanaspoti: Kwa nini umechagua muziki wa dansi wakati vijana wengi wa kizazi chako wanakimbilia Bongo Fleva na Singeli?

Zubery: Kwanza, dansi ni muziki unaoishi na kusikilizwa na kila mtu, kuanzia wazee hadi vijana. Pili, ni muziki ambao unaweza kunipatia shoo kila siku, si lazima nisubiri miezi kadhaa ndipo nipate shoo moja. Pia muziki wa bendi si wa msimu. Unahitaji kipaji cha kweli, si ujanja ujanja.

Mwanaspoti: Ni nini mashabiki hawakijui kuhusu wewe?

Zubery: Wengi hawajawahi kujua mimi ndiye niliyeimba sauti katika tamthilia nyingi zilizorushwa na televisheni kubwa hapa nchini. Miongoni mwa tamthilia hizo ni Sarafu, ambayo imeigizwa na mastaa wengi wa Bongo Movie, pamoja na Chanda, Yalait na Turufu. Pia nimeandikia baadhi ya wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, ingawa hawajawahi kunitaja. Niliwaandikia kwa moyo wangu, si kwa kutaka fadhila. Siku wakiamua watanitaja.


Mwanaspoti: Twanga Pepeta, ni changamoto gani kubwa unazokutana nazo unapofanya kazi na wakongwe?

Zubery: Sioni changamoto yoyote, ni faida kwangu kwa sababu napata nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwao na kuendelea kuiva kimuziki. Hilo limenifanya nijiamini zaidi na kufanya vizuri ndani ya bendi yangu. Hata mwaka juzi nilishinda tuzo ya msanii bora chipukizi wa muziki wa dansi. Kwa hiyo, kuimba na wakongwe kwangu ni kujengeka na kukua zaidi.

Mwanaspoti: Ni wasanii gani wa dansi na Bongo Fleva unawakubali zaidi?

Zubery: Kwa upande wa dansi namkubali sana mzee wangu Ali Choki kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ukizungumzia Twanga Pepeta huwezi kukosa jina lake, kwa sababu nyimbo nyingi tunazoimba ni tungo zake na ni miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa katika bendi hiyo. Kwa Bongo Fleva namkubali Barnaba na natamani siku moja tufanye kazi pamoja. Ni mwimbaji mzuri, anaimba live na ana uwezo wa kuimba na bendi.



Mwanaspoti: Katika safari yako ya muziki, ni tukio gani lililowahi kukukuta jukwaani ambalo hutalisahau na kwa nini?

Zubery: Ni siku ambayo wimbo wangu Dear Ex ulipotambulishwa. Nilijiona kama nimezaliwa upya katika ulimwengu wa muziki wa dansi. Watu walikuwa wengi siku hiyo na ilikuwa siku yenye matukio mawili muhimu kwangu, kwanza siku yangu ya kuzaliwa na pili ni utambulisho wa wimbo huo ambao ni utunzi wangu. Kikubwa zaidi, nilipata fedha nyingi.

Mwanaspoti: Kwa upande wa soka, wewe ni shabiki wa timu gani na ni mchezaji gani unayemkubali zaidi?

Zubery: Mimi ni shabiki wa timu yenye historia kama bendi yangu ya Twanga Pepeta. Kwa kifupi, mimi ni mwana Yanga lia lia. Kwa upande wa wachezaji namkubali sana namba 10, tishio Tanzania, Aziz Ki.



Mwanaspoti: Kwa upande wa maisha binafsi, Zubery wa jukwaani na Zubery wa nyumbani wana tofauti gani?

Zubery: Zubery akiwa jukwaani ni mburudishaji anayependa kazi yake, lakini nyumbani ni baba anayependa familia yake. Ninaishi vizuri na kila mtu na ninamheshimu kila mtu, ila sipendi dharau.


Mwanaspoti: Nini ujumbe wako kwa vijana wanaotamani kuingia kwenye muziki wa dansi lakini wanaona muziki huo ni wa kizazi cha zamani?

Zubery: Ushauri ni wawe na moyo wa uthubutu. Muziki huu sisi vijana ndiyo tunatakiwa kuupambania kwa kuleta vitu vipya vitakavyopendwa na vijana wenzetu pamoja na watu wa rika zote. Tunatakiwa kutumia sanaa na vipaji vyetu kuleta kazi bora zinazoendana na soko la sasa. Tuangalie mashabiki wanakosa nini, kisha tukifanyie kazi. Muziki ni biashara, hivyo unahitaji ubunifu ili uweze kumvutia mteja wako. Kikubwa ni uthubutu.


Mwanaspoti: Kwa nini uliamua kutunga wimbo wa Dear Ex?

Zubery: Niliamua kutunga wimbo huo baada ya kuangalia soko la muziki linataka nini. Pia nilitafuta jina ambalo hata kijana akilisikia atatamani kujua kilichomo ndani ya wimbo. Ukweli ni mwanamke akiupenda wimbo, mara nyingi huo ndiyo mwanzo wa safari ya wimbo kufanya vizuri.

Nikaangalia nikagundua wengi wameumizwa kwenye mapenzi, hivyo nikatumia njia hiyo kugusa hisia zao. Wimbo ulifanya vizuri na kunipandisha daraja katika muziki. Zuberi wa mwanzo si Zuberi wa Dear Ex.

Hata hivyo, Zubery anasema safari yake haiishii hapo, kwani anaandaa kazi mpya ambayo anaamini itakuwa bora zaidi ya Dear Ex na kuendelea kumtambulisha kwa mashabiki wa muziki wa dansi.