Shilole aingilia kati ndoa ya Diamond, Zuchu

Muktasari:
- Wiki iliyopita Diamond alifunga ndoa na Zuchu ambaye ni msanii kutoka katika lebo yake ya WCB na Shilole alisema licha ya watu kushangaa kufanya kisirisiri, ni jambo la kawaida kwa wanandoa walioridhiana.
WAKATI ndoa ya mastaa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na mkewe Zuchu bado haijapoa, msanii na mjasiriamali, Shilole amewapongeza wawili hao huku akiwataka wasikubali kuendeshwa na watu wa nje, wawe wavumilivu na kuacha utoto.
Wiki iliyopita Diamond alifunga ndoa na Zuchu ambaye ni msanii kutoka katika lebo yake ya WCB na Shilole alisema licha ya watu kushangaa kufanya kisirisiri, ni jambo la kawaida kwa wanandoa walioridhiana.
“Kuoa ni jambo la kheri bwana na ni hatua kubwa sana. Nampongeza sana Diamond kwani siyo jambo la mchezo hilo na watu wanatakiwa kuelewa kuoa kisirisiri ni jambo la kawaida tu. Neno langu kwa Diamond na Zuchu ni wakitaka kudumu kwenye ndoa waache utoto na wawe wavumilivu na wasikubali ndoa yao kuendeshwa na watu nje."
"Najua ninavyosema hivi. Wapo watu watasema mimi mbona sikuweza kuyafanya hayo kwenye ndoa zangu nilizoachika. Niwaambie tu hakuna mtu mvumilivu na mwenye sifa za kuwa mke kama mimi, ila linapotokea hadi naachika ujue zipo sababu zimetaka iwe hivyo na sijawahi kuzizungumza hadharani," alisema Shilole.