Sandra awalaza Diamond, Zuchu nyumba moja
Muktasari:
- Mwanaspoti limeambiwa kuwa wawili hao wameamua kuishi pamoja ili kuhakikisha binti yao, aliyezaliwa Agosti 2, 2026, anapata malezi ya karibu kutoka kwa baba na mama, tofauti na mfumo waliokuwa wakiutumia awali.
UJIO wa mtoto wao, Sandra, umeonekana kubadili mfumo wa maisha ya mastaa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Zuchu, ambao sasa wanaishi nyumba moja baada ya kipindi kirefu cha kila mmoja kuwa na makazi yake licha ya kuwa ndani ya ndoa.
Mwanaspoti limeambiwa kuwa wawili hao wameamua kuishi pamoja ili kuhakikisha binti yao, aliyezaliwa Agosti 2, 2026, anapata malezi ya karibu kutoka kwa baba na mama, tofauti na mfumo waliokuwa wakiutumia awali.
Chanzo cha habari kilicho karibu na mastaa hao, kimeiambia Mwanaspoti kuwa uamuzi huo umetokana na dhamira yao ya kushirikiana katika kumlea mtoto wao, huku kila mmoja akitimiza wajibu wake kama mzazi.
"Kwa sasa wanaishi nyumba moja, wanamlea mtoto wao pamoja ili apate malezi ya baba na mama, siyo ile staili waliyokuwa nayo wakiishi tofauti, ingawa walikuwa na amani katika ndoa yao," kilisema chanzo hicho.
Hatua hiyo inaleta sura mpya katika maisha ya Diamond na Zuchu, ambao kwa muda walikuwa wakitumia makazi tofauti licha ya kuwa wanandoa. Awali, Diamond alikuwa akiishi Mbezi Beach, huku Zuchu naye akiwa na nyumba yake katika eneo hilo hilo.
Mfumo huo wa maisha uliwahi kuzua maswali miongoni mwa mashabiki, lakini Zuchu aliwahi kuweka wazi kuwa uamuzi wa kuishi nyumba tofauti haukutokana na ugomvi, kutengana wala matatizo ya ndoa, bali ulikuwa mpangilio waliokubaliana wenyewe.
Hata hivyo, ujio wa Sandra umeonekana kuwa sababu ya kubadili utaratibu huo, huku sasa wawili hao wakichagua kuishi nyumba moja na kushirikiana katika malezi ya mtoto wao.
Januari 2025, Diamond na Zuchu walifunga ndoa ya Kiislamu kwa siri, lakini taarifa za ndoa hiyo zilikuja kujulikana zaidi Juni 2025, baada ya Sheikh Walid Kawambwa kueleza kuwa ndiye aliyewafungisha ndoa.
Tangu hapo, maisha yao binafsi yameendelea kuvuta hisia za mashabiki kutokana na umaarufu wao katika tasnia ya muziki, huku kila hatua ya uhusiano wao ikifuatiliwa kwa karibu.
Sasa, baada ya kupata mtoto wao wa kwanza pamoja, Diamond na Zuchu wameonekana kuingia katika ukurasa mpya wa maisha ya familia, huku uamuzi wao wa kuishi nyumba moja ukiweka msisitizo katika kushirikiana kulea Sandra.