Zuchu & Diamond Miaka saba, ngoma saba!
Muktasari:
- Wawili hao waliotangaza kufunga ndoa mwaka uliopita, kwa sasa wanafanya vizuri na wimbo wao mpya, Mvua ya Baraka (2026) ambao umetayarishwa na Mr. LG, huku video yake ikiongozwa na Director Joma ambaye Diamond amesifia uwezo wake.
Mastaa wanandoa, Zuchu na Diamond Platnumz wanaendelea kuonyesha ukubwa na ubunifu wao katika muziki wa Bongo Fleva, kitu ambacho kinaipa upekee 'kapo' yao ukilinganisha ni zile za mastaa wengine ambao wapo nao katika tasnia moja.
Wawili hao waliotangaza kufunga ndoa mwaka uliopita, kwa sasa wanafanya vizuri na wimbo wao mpya, Mvua ya Baraka (2026) ambao umetayarishwa na Mr. LG, huku video yake ikiongozwa na Director Joma ambaye Diamond amesifia uwezo wake.
Mvua ya Baraka ni wimbo unaoelezea furaha ya kupokea baraka ambayo imebadilisha maisha ya mtu, ambapo Zuchu na Diamond wameamua kuja na aina hiyo ya wimbo baada ya kujaliwa kupata mtoto wao wa kwanza ambaye wamempa jina la Sandrah, jina ambalo pia limetajwa mwishoni mwa ngoma hiyo.
Wimbo huo wa kuchezeka umeimbwa katika msingi wa shukrani baada ya maombi yao kujibiwa, pia unasheherekea mwanzo mpya wa maisha yao binafsi kuanzia upande wa ndoa, familia na mafanikio katika muziki na miradi yao mbalimbali ya kibiashara.
Muda mfupi baada ya wimbo huo kutoka ulishika namba moja katika chati ya YouTube katika nchi za Tanzania, Kenya, Qatar, na Falme za Kiarabu (UAE), na ndani ya siku nne video yake ikawa imetazamwa (views) zaidi ya mara milioni 4 katika mtandao huo na wana mashabiki wengi.
Kwa wawili hao, Mvua ya Baraka unakuwa ni wimbo wa saba kushirikiana wakifanya hivyo ndani ya miaka saba ambayo Zuchu amekuwa chini ya usimamizi wa WCB Wasafi, rekodi lebo yake Diamond ambaye alianza kuwatambulisha wasanii mwaka 2015 na hadi sasa imeshawasaini wanamuziki nane ambao kazi zao zinajulikana.
Zuchu, mziwanda wa mwimbaji wa Taarabu, Khadija Kopa, hadi sasa yeye na Diamond wamefanya vizuri kupitia kolabo hizi saba zifuatazo, Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024), Wale Wale (2024), Inama (2025) na Mvua ya Baraka (2026).
Na mara zote nyimbo zao zimekuwa zikipata mapokezi makubwa, mathalani wimbo wao, Inama (2025) ndani ya kipindi cha takriban miezi 10 video yake imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 38 ikiwa ni kazi ya saba yake Zuchu kufanya vizuri zaidi (most viewed) katika mtandao huo.
Kwa matokeo hayo, Zuchu na Diamond wanazidi kuongoza kama mastaa wanandoa au wapenzi ambao wameshirikiana katika nyimbo nyingi zaidi na ndani ya miaka saba wameshirikiana katika nyimbo saba wakiwa wao wawili pekee, yaani bila kushirikiana na msanii mwingine wa tatu.
Wanaowafuatia ni Nandy na mumwe Billnass, rapa aliyetoka kimuziki kupitia wimbo wake, Raha (2014) uliotengenezwa na Mesen Selekta huku akiwashirikisha TID na Naziz, mwanachama wa kundi la Necessary Noize kutokea Kenya ambalo lilitamba katika Hip Hop, Reggae na Dancehall.
Utakumbuka kuwa Nandy na Billnass tayari wamefanya kolabo sita lakini za wao wawili pekee ni tano ambazo ni Bugana (2019), Do Me (2020), Bye (2022), Totorimi (2024), na Hallo (2026). Wawili hao ambao wamekuwa pamoja tangu mwaka 2016, walifunga ndoa mnamo Julai 2022, na mtoto wao wa kwanza, Naya sasa ana umri wa miaka minne.
Diamond ambaye alitoka kimuziki mwaka 2009 na sasa ikiwa ni miaka 17 tangu aliposikika kwa mara ya kwanza, hakuna msanii wa kike awe wa ndani au nje ya Tanzania ambaye amerekodi naye nyimbo nyingi kama Zuchu ambaye amekuja kubadili sura ya mchezo katika Bongofleva hasa upande wa wasanii wa kike.
Kipindi Diamond ana uhusiano na mwanamitindo na mwanamuziki, Tanasha Donna kutokea Kenya, hadi wanaachana walikuwa wametoa wimbo mmoja tu 'Gere' ambao ulijumuishwa katika Extended Playlist (EP) ya Tanasha, Donna Tell (2020) ambayo aliwakutanisha pia Mbosso na Khaligraph Jones, mshindi wa AFRIMMA 2018.
Mbali na ndoa, ni wazi kuwa Diamond anashirikiana mara kwa mara na Zuchu kwa sababu ni mwanamuziki wa lebo yake. Pia alifanya kitu kama hicho kwa Mbosso, Lava Lava, Rayvanny ambaye wameshirikiana katika nyimbo zaidi ya 10.
Ikumbukwe Zuchu alitambulishwa na WCB Wasafi kupitia EP yake, I Am Zuchu (2020) ambayo ilikaa katika chati za YouTube Music Tanzania kwa wiki zaidi ya 100. Katika EP hiyo wimbo uliofanya vizuri zaidi unaitwa 'Wana' ambao unatajwa kama wimbo uliomtoa Zuchu kimuziki miaka saba iliyopita.