Sanaa zisizo na maadili ni kosa la mashabiki
Muktasari:
- Siku moja walikuwa wanamhoji msanii maarufu wa Bongofleva. Katikati ya mahojiano msanii akaulizwa, Tanganyika ilipata uhuru mwaka gani? Msanii alishindwa kujibu. Akaambiwa, imba wimbo wa Taifa mwanzo mwisho. Msanii alishindwa kujibu, akaishia kati. Na sio maswali hayo tu, alikosa vimaswali vingi vidogo vidogo vya mtindo huo.
CHANELI moja kubwa ya TV nchini ilikuwa na kipindi fulani cha mahojiano cha kipekee. Ilikuwa inawauliza wasanii maswali yasiyohusu sanaa zao. Kwa mfano, anaweza akaletwa msanii wa Bongo Fleva na kuulizwa Bendera ya Tanzania ina rangi ngapi?
Siku moja walikuwa wanamhoji msanii maarufu wa Bongofleva. Katikati ya mahojiano msanii akaulizwa, Tanganyika ilipata uhuru mwaka gani? Msanii alishindwa kujibu. Akaambiwa, imba wimbo wa Taifa mwanzo mwisho. Msanii alishindwa kujibu, akaishia kati. Na sio maswali hayo tu, alikosa vimaswali vingi vidogo vidogo vya mtindo huo.
Wakati naangalia kipindi ghafla hoja moja ikanigonga kichwani. Ikaniambia, muda mwingine mashabiki tunakuwa na uonevu kwa wasanii wetu. Ni uonevu kuwa na matumaini na mategemeo kwamba msanii wa aina hii anaweza kuimba nyimbo za ‘kuelimisha’.
Bila shaka umeshawahi kusikia kelele za kwamba wasanii wetu hawaimbi nyimbo za kuijenga jamii. Hawaimbi nyimbo za kuelimisha. Kama sio kusikia basi pengine wewe ni moja ya watu wanaolalamika kuhusu wasanii wa Bongo kwamba wenyewe wanaimba pombe, ngono, mapenzi, mihadarati na starehe.
Lakini tusichokijua ni kwamba, wataalaamu wanadai, msanii hutengeneza sanaa yake kulingana na kile anachokijua tu. Yaani mwandishi wa filamu hawezi kuandika filamu kuhusu kitu asichokijua, mwanamuziki hawezi kuandika nyimbo kuhusu vitu asivyokuwa na uelewa navyo. Yaani usitegemee msanii kama Dulla Makabila ambaye mwenyewe amekuwa akieleza bila kificho kwamba ‘shule imempiga chenga’ aandike wimbo kuhusu nadharia za fizikia.
Kwa mantiki hii nadhani mashabiki tunatakiwa kupunguza au kubadilisha mtazamo wetu. Yaani badala ya kuwa na matarajio kwamba wasanii waimbe nyimbo za kujenga jamii, tushushe matarajio yetu na kusema, baadhi ya wasanii waimbe nyimbo za kujenga jamii.
Kwa sababu sio kwamba hakuna wasanii ambao hawaimbi nyimbo za namna hiyo, wapo ila sio wasanii ambao sisi tunapenda kuwasikiliza.
Kwa mfano, kwenye kipindi hicho hicho cha TV, alienda msanii wa Hip Hop na kila swali aliloulizwa alipata. Na ukienda kusikiliza nyimbo zake, utaelewa kwamba mashairi yameandikwa na mtu aliyeelimika. Na nikisema kuelimika simaanishi kuwa na degree kumi na sita tu, hapana, namaanisha kuelimika kuwa na uwezo wa kuongelea mambo yenye tija.
Ili tuwe na amani itabidi tukubali kwamba, kuna wasanii wataimba ngoma za pombe, ngono, starehe na kuhamasisha matumizi ya mihadarati, na kuna wasanii wataimba ngoma kuhusu hali ya kisiasa, hali ya uchumi na mambo mengine ya kulijenga taifa.
Na tukifanya hivi kitakachotokea ni kwamba, badala ya kulalamika wasanii wanaimba mambo ya ajabu, tutatakiwa kulalamika kwamba, mashabiki tunapenda kusikiliza vitu vya ajabu. Kwa sababu wasanii wanaoimba mambo ya msingi wapo, ila sisi tumechagua kuwasikiliza wanaoimba pombe, ngono na kupiga sherehe.