S2KIZZY, ABBAH, waja na 'New Generation Festival', wasanii 15 kukiwasha
Muktasari:
- Wakati S2Kizzy amewahi kuimba nyimbo nyingi za kushirikishwa na wasanii wengine ikiwemo Pochi Nene (Rayvanny ft S2Kizzy), Fashion (Chino Kidd ft S2Kizzy), Mama Zuri (Nikki Wa Pili ft S2Kizzy) na Turn Me On (Whozu ft S2Kizzy).
Watayarishaji maarufu wa muziki hapa nchini, S2Kizzy na Abbah, wanatarajia kufanya tamasha kubwa la muziki wa Bongo Fleva walilolipa jina la New Generation.
Akizungumzia hilo, Abbah ambaye jina laki halisi ni Sweetbert Mwinula, amesema tamasha hilo litafanyika Oktoba 30, 2026 katika ukumbi wa Dar Village ambapo wasanii 15 watashambulia jukwaa.
Abbah amesema malengo ya tamasha hilo ni katika kuendelea kuwapa burudani mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva.
Amewataja baadhi ya wasanii watakaotumbuiza siku hiyo kuwa ni Billnass, Dullah Makabila, Meja Kunta, Abigael Chams, Yammy, Al Xpo, Gnako, Kontawa, Darasa, Optimist, Jaiva, Lois na Chinno.
Amesema siku hiyo kutaimbwa nyimbo mbalimbali ikiwemo zilizowatoa wasanii hao hadi kujulikana.
"Kupitia tamasha hilo, historia inaenda kuandikwa katika kiwanda cha burudani, historia ambayo haiwezi kufutika kwa kuacha kumbukumbu ambayo itaishi kwa miaka mingi ijayo," amesema Abbah.
Abbah na S2Kizzy ni watayarishaji maarufu wa muziki ambao wametoa hits mbalimbali zikiwemo za wasanii maarufu kama Marioo, Nandy, Diamond, Ali Kiba na wengine wengi.
Moja ya Ngoma kali ni ile ya Finale, aliyoimba Ali Kiba na Bien kutoka nchini Kenya.
Abbah na S2kizzy kwa sasa wanajitambulisha kwa jina la "Watia Lami" kwenye Kiwanda cha Burudani.
Kufanya kwao kazi na wasanii wengi kunachochewa na ubunifu walionao unaotarajiwa kuonekana siku hiyo ya tamasha.
Mbali ya kuwa maprodyuza, wawili hawa huwa pia wanaimba.
Nyimbo ambazo Abbah amewahi kuimba ni Nishazama, My Gash, Kokoro, Mwagia Ndani na Wazungu.
Wakati S2Kizzy amewahi kuimba nyimbo nyingi za kushirikishwa na wasanii wengine ikiwemo Pochi Nene (Rayvanny ft S2Kizzy), Fashion (Chino Kidd ft S2Kizzy), Mama Zuri (Nikki Wa Pili ft S2Kizzy) na Turn Me On (Whozu ft S2Kizzy).