Aunt Ezekiel afichua siri ya pete mbili za dhahabu
Muktasari:
- Oktoba 2025, Mwanaspoti liliripoti Aunt alikuwa amebadili dini na kutumia jina la Rahma baada ya kufunga ndoa na Kusah kwa taratibu za Kiislamu.
STAA wa Bongo Movie, Aunt Ezekiel ameweka wazi maana ya pete mbili za dhahabu alizovishwa na mumewe, msanii wa muziki wa Bongo Fleva, ‘Kusah’, Oktoba 28, 2026, kwenye sherehe ya siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika Goba nyumbani kwake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aunt amefafanua Pete hizo moja ni ya uchumba na nyingine ni ya ndoa, kwani walipofunga ndoa yao ya siri awali, hawakuvalishana pete kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya wanandoa.
Tukio hilo limeibua kumbukumbu ya safari ya ndoa ya mastaa hao, ambao uhusiano wao umekuwa ukizungumziwa tangu walipoanza kuwa wapenzi na baadaye kupata watoto pamoja.
NDOA YA SIRI
Mei 23, 2025, Kusah aliliambia Mwanaspoti yeye na Aunt tayari walikuwa mke na mume, baada ya kufunga ndoa nyumbani kwao Bumbuli, mkoani Tanga.
Kusah amesema walifuata taratibu za dini ya Kiislamu na kuamua kufanya hivyo kimya kimya bila sherehe kubwa na jambo muhimu kwake lilikuwa kutimiza hatua ya kufunga ndoa badala ya kufanya sherehe.
Ndoa hiyo ilikuja baada ya Kusah, Januari 2025 kuliambia Mwanaspoti picha za wawili hao wakiwa katika mavazi ya harusi mwaka 2021 hazikuwa uthibitisho wa ndoa, bali zilihusiana na utangazaji wa wimbo wake wa ‘I Wish’. Wakati huo amesema hawakuwa wameoana, lakini aliahidi kumuoa Aunt mwaka huo.
Oktoba 2025, Mwanaspoti liliripoti Aunt alikuwa amebadili dini na kutumia jina la Rahma baada ya kufunga ndoa na Kusah kwa taratibu za Kiislamu.