Neddy Music ashindwa kujizuia na Simba
Muktasari:
- Ingawa amesema ni mapema kusema moja kwa moja Simba inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kiwango wanachokionyesha wachezaji kinawapa matumaini makubwa ya kuyaona mataji mbele yao.
MSANII wa Bongo Fleva, Neddy Music, amesema kucheka na kulia ni kupokezana, kwa sasa ni zamu ya mashabiki wa Klabu ya Simba sura zao kuwa na tabasamu baada ya kukaa kwa muda mrefu bila matumaini ya ubingwa.
Ingawa amesema ni mapema kusema moja kwa moja Simba inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini kiwango wanachokionyesha wachezaji kinawapa matumaini makubwa ya kuyaona mataji mbele yao.
“Mimi ni shabiki wa Simba damu, kipindi ambacho timu ilikuwa inachukua ubingwa mfululizo sisi ndiyo tulikuwa tunatamba mji, Yanga ikaja ikapindua meza, imetamba kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026, mashabiki wao walikuwa na tambo na kuona hakuna timu ambayo inaweza ikawapa ushindani,” amesema Neddy Music na kuongeza;
“Simba inapokuwa inarejesha makali yake, inakuwa vizuri kuanzia kwenye ligi hadi Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa wakati wao wanalalamika, sisi tunacheka ndiyo maana nimesema kulia na kucheka ni kupokezana.”
Amesema kuna kipindi Simba ilikuwa inapitia changamoto ya kufungwa na Yanga, alikuwa anajikuta anaumia pamoja na hilo hakuwahi kujutia kuishabikia timu hiyo, badala yake alijipa uvumilivu wa kusubiri kicheko.
“Ushabiki wa timu hizo mbili hapa nchini ni ngumu kukwepa raha na karaha, Simba inavyocheza inakupa raha ya kuiangalia namna wachezaji wanavyotoa burudani,” amesema.