Romeo Beckham anavyotingisha kwenye mitindo
Muktasari:
- Huyu ni Romeo Bechkham ambaye katikati ya sakata hilo lililotokea kati ya 2014 na 2023, alitajwa kwamba anapenda kuingia kwenye fani ya mitindo na kwamba, kuna nyakati alikuwa haendi katika mazoezi ya timu akiwa amejifungia ndani akifanya mazoezi ya ‘Catwalk’ za majukwaa ya mitindo.
MIAMI, MAREKANI: WAKATI flani aliwahi kucheza soka kwenye timu za vijana za Arsenal na Inter Miami, lakini akaona haimpi. Akaacha.
Huyu ni Romeo Bechkham ambaye katikati ya sakata hilo lililotokea kati ya 2014 na 2023, alitajwa kwamba anapenda kuingia kwenye fani ya mitindo na kwamba, kuna nyakati alikuwa haendi katika mazoezi ya timu akiwa amejifungia ndani akifanya mazoezi ya ‘Catwalk’ za majukwaa ya mitindo.
Lakini, ikiwa ni takriban miaka miwili tangu alipoachana na timu ya baba’ke, Inter Miami, hivi sasa anafanya balaa kwenye fani ya mitindo akitesa majukwaani nchini Marekani na Uingereza.
Unaambiwa dogo huyo aliyezaliwa Westminster huko London ana dili kibao za mitindo pamoja na mialiko kutoka kampuni kubwa za mitindo katika mataifa mengi ikiwamo Ujerumani, Italia na Ufaransa.
Mbali ya Romeo aliyezaliwa katika familia ya bilionea David Beckham na Victoria Beckham kutesa katika mitindo, lakini utambulisho wake kote duniani unafuata nyayo za baba yake aliyewahi kujitosa katika mitindo kwa muda mfupi.
Romeo amekuwa akipendelea uonyeshaji mitindo akiwa amechia kifua wazi, huku baadhi ya michoro (tatoo) aliyojichora mwilini ikionekana hadharani. Staili hiyo aliwahi kuitumia baba yake. Na hivi karibuni alipiga picha kali kwa ajili ya jarida la V Magazine ambalo ni maarufu kwa mitindo na wanamitindo.
Romeo mwenye umri wa miaka 22 alionyesha kifua chake chenye tatoo akiwa amepozi kwenye vazi la Jean Paul Gaultier. Pia alionekana akitingisha koti la ngozi la Burberry na mwonekano wa kifahari wa Dolce & Gabbana. Wakati mashabiki wakifurahia picha zake, familia ya Beckham imeendelea kuzungumziwa kutokana na mgogoro na mtoto mkubwa, Brooklyn. Hivi karibuni Brooklyn na mkewe Nicola Peltz waliapa upya viapo vya ndoa bila kuialika familia ya Beckham – jambo lililoibua gumzo kubwa. Inadaiwa Brooklyn alimwaga chozi wakati akitoa hotuba ukumbini iliyogusa hisia akiishukuru familia ya mkewe, Peltz, huku wazazi wake David na Victoria akiwaacha bila kuwataja. Wakati huo David na Victoria walionekana wakifurahia likizo na watoto wao wengine kusini mwa Ufaransa na Italia. Drama hii imezua mijadala mitandaoni na Brooklyn anadaiwa kuvunjika moyo kutokana na namna mkewe Nicola anavyopakwa matope kwenye kile kinachodaiwa kuwa ni tofauti za kifamilia.