Tetema ilivyobadilisha muziki wa Rayvanny
Muktasari:
- Wimbo huo sio tu umeendelea kusikika na watu bali pia umeendelea kumpa mafanikio makubwa ndani na nje kimataifa ukiweka historia mbalimbali za mauzo, tuzo na kumpa shoo kubwa Ulaya.
UKISIKIA muziki mzuri unaishi ndio ilivyotokea kwa Rayvanny baada ya kuachia kibao cha Tetema mwaka 2019, wimbo huo umeendelea kuwa midomoni na masikioni mwa mashabiki kutokana na kutengenezwa kwenye ubora mkubwa.
Wimbo huo sio tu umeendelea kusikika na watu bali pia umeendelea kumpa mafanikio makubwa ndani na nje kimataifa ukiweka historia mbalimbali za mauzo, tuzo na kumpa shoo kubwa Ulaya.
Kwa Rayvanny, wimbo wa ‘Tetema’ umekuwa tiketi yake ya kuingia kwenye ramani ya muziki wa kimataifa, kila msanii ana njia zake za kupenya nje lakini kwa nyota huyo ambaye anamiliki lebo ya Next Level Music wimbo huo ndio umekuwa mafanikio yake.
Tangu alipoachia kibao hicho mwaka 2019 akiwa na Diamond Platnumz mkali huyo amekuwa na mafanikio makubwa kwenye muziki wake kutoka kufanya shoo Afrika Mashariki hadi kupata nafasi ya kupafomu duniani. Si mchezo!.
Alipouachia mwaka 2019 akimshirikisha Diamond Platnumz, wengi waliuona kama wimbo mwingine wa Bongo Fleva wenye nafasi ya kufanya vizuri Afrika Mashariki. Hakuna aliyedhani kuwa miaka sita baadaye, wimbo huohuo ungekuwa moja ya kazi za muziki kutoka Tanzania zilizofika mbali zaidi kimataifa, ukibadilishwa mara kadhaa na kuendelea kuishi katika masoko tofauti ya dunia.
REMIX TATU
Kibao hicho kilianza kufanya vizuri Tanzania kabla ya kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki na kuingia katika masoko mengine ya Afrika. Umaarufu wa wimbo huo uliwafanya mastaa wengine kutoka Nigeria, Patoranking na Zltan kuomba kolabo na kufanya remix ya wimbo huo mwaka 2019.
Miaka miwili baadaye akafanya tena Mama Tetema akimshirikisha staa wa Colombia, Maluma, na kuufikisha wimbo huo kwa mashabiki wa muziki wa Amerika Kusini.
Lakini kama kuna toleo lililobadili kabisa hadhi ya ‘Tetema’, basi ni ‘Oh Mama! Tetema’. Rayvanny aliingia ubia na kampuni kubwa ya muziki ya India, T-Series, akiwashirikisha Nora Fatehi, Shreya Ghoshal, Vishal Mishra na Sanjoy.
SHOO
Wimbo walioshirikiana na Maluma ulimfanya msanii huyo kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMAs), mwaka 2021 alipopanda katika jukwaa hilo akiwa na Maluma wa Colombia mwaka 2021.
Haikuishia hapo Machi 10, 2022 Rayvanny akapata nafasi tena ya kupafomu jukwaa moja na Maluma nchini Ufa ransa na hio ni kwa sababu ya ushirikiano na wimbo huo ambao umemletea mafanikio makubwa sio mkali huyo pekee hata kwa Maluma.
Vilevile wimbo huo ulimfanya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kushika namba moja chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo, Mama Tetema (2021), ikiwa ni mara ya pili kuingia chati hizo baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart akiwa na Dj Cuppy wa Nigeria.
GRAMMY
Remix na Maluma pia ilimfanya Rayvanny aingie kwenye vitabu vya kihistoria baada ya Mama Tetema kuwania tuzo za 66 za Grammy 2024 katika kipengele cha Best Latin Pop Album ingawa hakufanikiwa kuchukua tuzo hiyo.
Wimbo huo ulikuwa ndani ya albamu ya Maluma iitwayo Don Juan (2023) ambayo ndani ya albamu hiyo kulikuwa na ngoma mbalimbali ikiwemo Mama Tetema. Ikumbukwe Grammy ni tuzo kubwa duniani hivyo kitendo cha msanii kutajwa tu kuwania kinaongeza kitu kikubwa kwenye karia yake.
KOMBE LA DUNIA
Kilichofanya ngoma hiyo kuwa ya kipekee ni kwamba mafanikio yake hayakuishia kwenye majukwaa ya muziki. Wimbo huo ulimfungulia Rayvanny milango ya kufanya kazi kwa karibu na Nora Fatehi. Wawili hao wameachia ngoma nyingine iitwayo Champion ikiwa inayohusu soka, hata hivyo hiyo inakuwa kolabo ya tatu kwa wasanii hao baada ya Pepeta, Ooh Mama Tetema na sasa Champion. Mwaka 2026,
Rayvanny aliandika historia nyingine baada ya kupanda jukwaa la sherehe za Kombe la Dunia sambamba na Nora Fatehi. Kwa wengi, ilikuwa ni mwendelezo wa safari iliyoanza na ‘Tetema’ miaka kadhaa nyuma. Hivi sasa karibu kila hatua kubwa ya Rayvanny nje ya Tanzania imekuwa na alama ya ‘Tetema’. Wimbo huo ulimfungulia soko la Afrika, ukamfikisha Amerika Kusini kupitia Maluma, ukampeleka India kupitia T-Series, ukamrudisha kufanya kazi na Nora Fatehi na kumpeleka kwenye jukwaa la Kombe la Dunia. Ni safari ambayo si rahisi kuipata kwa msanii wa Bongo Fleva.
Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikitoa nyimbo nyingi zilizotikisa Afrika, lakini ni chache zilizofanikiwa kuendelea kuishi kwa miaka mingi kupitia matoleo tofauti na ushirikiano wa kimataifa. ‘Tetema’ imekuwa mfano wa kazi ambayo haikuishia kuwa hit ya muda mfupi, bali iligeuka kuwa chapa ya Rayvanny katika soko la dunia.
MSIKIE MWENYEWE
Msanii huyo amesema: “Kila tunachokifanya ni kwa sababu ya Bongo Fleva na kuipeperusha bendera yetu ya Tanzania kwa hiyo mimi nikipafomu kwenye matamasha makubwa yatasaidia muziki wetu na kuwasaidia na wasanii wengine.”