Riyama afunguka kukacha uigizaji
Muktasari:
- Riyama ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo kimoja cha redio nchini, ameliambia Mwanaspoti amekuwa akipigiwa na kupokea simu nyingi kutoka kwa mashabiki wakihoji kulikoni kuacha kuigiza au amepigwa 'kipapai', lakini ukweli ni kwamba ameipotezea fani hiyo kwa muda kwa sababu ya masilahi tu na si vingine.
MWIGIZAJI mkongwe nchini, Riyama Ally amesema amekuwa kimya katika fani hiyo kwa sababu ya ishu ya kimasilahi tu na wa sio kitu kingine kama inavyoelezwa huko mtaani.
Riyama ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo kimoja cha redio nchini, ameliambia Mwanaspoti amekuwa akipigiwa na kupokea simu nyingi kutoka kwa mashabiki wakihoji kulikoni kuacha kuigiza au amepigwa 'kipapai', lakini ukweli ni kwamba ameipotezea fani hiyo kwa muda kwa sababu ya masilahi tu na si vingine.
"Nimekaa pembeni kwa ishu za kuigiza sababu hizo hizo, hayo mengine yanayosemwa ni hisia zao tu. Kwa msanii anayejielewa, hawezi kukukubali kuigiza na kulipwa kiduchu kwa kazi kubwa unayoifanya. Sifanyi kazi kwa mazoea, naangalia masilahi, kuna unaofanya kazi anaona anakulipa fedha nyingi, lakini sio kweli," alisema mwanadada huyo na kuongeza;
"Sasa ilikuwa unachukuliwa kimazoea, yaani mtu anakuja anakwambia nisaidie kuigiza kipande fulani halafu pesa anayokupa hata theluthi ya faida anayoipata mwenyewe, ndipo nikaona ya nini kwani nimezaliwa kuigiza tu? Ndio nikaamua kufanya mambo mengine, miaka mitano sasa siigizi na maisha yanaenda."Riyama
Hata hivyo, Riyama alisema, baada ya kukataa ofa zao za kuigiza, baadhi yao waliaamua kufanya kampeni ya kumshusha na kuwatengeneza watu wawe kama yeye Riyama katika faini, lakini ukweli hakuna wa kumfikia kwa vile yeye ni yeye na wengine ni wengine tu.
"Hakuna kificho kuna baadhi ya waandaaji walifanya sana kampeni za kutaka kunishusha wakaanza kuninyima Tuzo za Mwigizaji Bora wa Kike, pia waliwatengeneza watu wawe kama Riyama,kitu ambacho kipaji chake. Nashukuru kwa kipaji na uwezo alionijalia Mungu na nitaendelea kubaki kama nilivyo," alisema.