Rayvanny: Touch sasa yazungumza yenyewe
Muktasari:
- Wiki mbili tu baada ya kuachiliwa, Touch ilivunja rekodi kwa kupata uteuzi kwenye tuzo za EAEA, ikiwa ni miongoni mwa nyimbo zilizofika hatua hiyo mapema tangu kutolewa.
MWEZI mmoja umetimia tangu Msanii wa Bongo Flava na mmiliki wa lebo ya Next Level, Rayvanny, aachie video ya wimbo wake Touch, ambao mwanzoni ulikutana na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya mashabiki, lakini sasa umeanza kuonyesha sura nyingine.
Wiki mbili tu baada ya kuachiliwa, Touch ilivunja rekodi kwa kupata uteuzi kwenye tuzo za EAEA, ikiwa ni miongoni mwa nyimbo zilizofika hatua hiyo mapema tangu kutolewa.
Rayvanny alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa video ya Touch inawania tuzo ya Video Bora ya Mwaka, huku hatua hiyo ikiendelea kuongeza hamasa kwa mashabiki wake.
Katika kipindi hicho, Touch imeendelea kupata watazamaji wengi kwenye mtandao wa YouTube, huku video yake ikifikisha zaidi ya views milioni 4.2.
Kwa upande wa YouTube, Touch nayo haijaachwa nyuma, ikiwa imetinga hadi nafasi ya 12 kwenye orodha ya video zinazotrend Tanzania na kuendelea kuvuta macho ya watazamaji.
Hata hivyo katika kuitangaza Touch, Rayvanny alitumia njia tofauti kuwafikia wasikilizaji, ikiwemo kuwapa zawadi baadhi ya watu aliowakuta wakisikiliza wimbo huo, wakiwemo madereva wa bajaji.
Moja ya mambo yaliyoifanya video hiyo kuonekana kwa jicho tofauti ni namna ilivyotengenezwa, baada ya Rayvanny kusafiri na kufanya baadhi ya upigaji picha katika nchi tatu, ambazo ni Dubai, Malaysia na Thailand.
Kutokana na kufanyika kwa upigaji picha katika maeneo hayo tofauti, Touch imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa video zilizotumia gharama kubwa katika utengenezaji, ingawa kiasi halisi cha fedha kilichotumika hakijawekwa wazi.
Mabadiliko hayo yameufanya wimbo huo kuanza kuzungumzwa kwa namna tofauti na ilivyokuwa siku za mwanzo baada ya kuachiwa.
Wakati wa mwanzo baadhi ya mashabiki walikuwa na maoni hasi, lakini Rayvanny aliendelea kuisukuma kazi hiyo na kuwapa nafasi mashabiki kuisikiliza na kuitazama zaidi.
Kwa sasa, uteuzi huo umeifanya Touch kuwa miongoni mwa kazi zinazofuatiliwa katika safari ya kuelekea tuzo hizo.